Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Francis Ngannou alivyovishinda vikwazo kutimiza ndoto yake

Muktasari:

  • Katika safari yake ya kwenda Ufaransa, alipitia Hispania, huko akakamatwa na kuwekwa ndani kwa muda wa miezi miwili akikabiliwa na kosa la kuvuka mpaka kinyume cha sheria.

Paris, Ufaransa. Mwigizaji kutoka Canada, Jim Carrey aliwahi kusema: "Ni bora kuhatarisha maisha yako kuliko kujisalimisha. Ikiwa utakata tamaa katika kufukuzia ndoto zako, ni nini utakuwa umebaki nacho?" Hii inatufundisha kwamba tunapokuwa katika mapambano ya kuzifikia ndoto zetu, usiruhusu kitu chochote kukukwamisha halafu ukakubali iwe hivyo.

Alichokisema mwigizaji huyo, pengine ndicho kilichomfanya mwanamasumbwi kutoka Cameroon ambaye hivi sasa makazi yake yapo Paris nchini Ufaransa. Huyu anaitwa Francis Zavier Ngannou ambaye alizaliwa Septemba 5, 1986.

Ngannou ni mpiganaji wa masumbwi na mchezaji wa MMA (mixed martial art). Kwa sasa anashiriki katika divisheni ya Uzito wa Juu ya Professional Fighters League (PFL), ambapo ni bingwa wa kwanza wa PFL Super Fights Uzito wa Juu.

Kabla ya hapo, alishiriki katika divisheni ya uzito wa juu ya Ultimate Fighting Championship (UFC) kutoka 2015 hadi 2022, ambapo alikuwa bingwa wa UFC Uzito wa Juu.

Ngannou alikuwa akionekana kama mpiganaji mwenye nguvu zaidi katika divisheni ya uzito wa juu ya UFC, alimaliza mapambano saba kati ya 14 ya UFC kwa knockout kabla ya dakika mbili kufikia mwisho wa raundi ya kwanza.


Alifikaje hapo?

Ngannou alizaliwa na kukulia katika Kijiji cha Batié, Cameroon. Alikuwa anaishi katika umaskini na hakuwa na elimu rasmi wakati wa ukuaji wake. Wazazi wa Ngannou walitalikiana alipokuwa na umri wa miaka sita, akapelekwa kuishi kwa shangazi yake. Katika umri wa miaka 10, Ngannou alianza kufanya kazi kwenye machimbo ya mchanga ya Batié kutokana na ukosefu wa fedha.

Kama mtoto, alikabiliwa na kushawishiwa na makundi kadhaa kijini kwao, lakini alikataa kuingia huko na badala yake aliamua kutumia sifa mbaya za baba yake kama mpiganaji wa mitaani kumpa motisha ya kufanya kitu kizuri na kufuata ndoto yake ya kuwa mpiganaji wa masumbwi.

Akiwa na umri wa miaka 22, Ngannou alianza mafunzo ya masumbwi, licha ya upinzani wa awali kutoka kwa familia yake. Baada ya mwaka mmoja wa mafunzo, alisitisha kutokana na kupata maradhi. Alifanya kazi mbalimbali ili kujikimu, hadi alipofikia umri wa miaka 26 alipoamua kuhamia Paris nchini Ufaransa kufuata mafunzo zaidi ya masumbwi ili atimize ndoto zake.

Katika safari yake ya kwenda Ufaransa, alipitia Hispania, huko akakamatwa na kuwekwa ndani kwa muda wa miezi miwili akikabiliwa na kosa la kuvuka mpaka kinyume cha sheria. Baada ya kufika Paris, hakuwa na fedha, hakuwa na marafiki, pia hakuwa na mahali pa kuishi. Akawa anaishi mitaani.

Baada ya kuishi mitaani mjini Paris, Ngannou alipata nafasi katika klabu ya masumbwi ambapo alikutana na kocha Didier Carmont ambaye alielewa hali yake, akaamua kumsaidia.

Carmont alimuombea afanye mazoezi gym bila malipo, kisha akamtambulisha Ngannou kwenye mchezo wa MMA.

Huku akiwa anaendelea na mazoezi, pia Ngannou alikuwa akijitolea katika shirika lisilo la kiserikali mjini Paris liitwalo Lo Chorba.

Wakati gym ya masumbwi ilipofungwa kwa msimu wa kiangazi, mkurugenzi wa Lo Chorba, Khater Yenbou, alimkutanisha Ngannou na Fernand Lopez sambamba na kumtambulisha kiwanda cha MMA.

Akiwa shabiki wa Mike Tyson, Ngannou awali alitaka kujifunza masumbwi lakini Lopez aliona uwezo wake katika MMA na kumshawishi ajaribu kushiriki MMA.

Lopez alimpa Ngannou vifaa vya MMA na kumruhusu kujiandaa na kulala katika gym bila malipo. Safari yake katika MMA ikaanzia hapo rasmi.

Akizungumzia safari yake hadi kufika hapo, Ngannou amesema: “Nilipokuwepo, sikuwa na chochote. Nilihitaji kila kitu. Lakini unapoanza kupata fedha unaanza kukusanya vitu kwa kusema nataka hiki, nataka kile. Lengo ni kufanya kitu kikubwa ili kukamilisha ndoto."

Mwanga alioanza kuuona katika safari ya kutimiza ndoto zake ambapo hivi sasa amekuwa na urafiki mkubwa na staa wa Ureno anayecheza soka Klabu ya Al Nassr ya Saudi Arabia, Cristiano Ronaldo, Ngannou amewakumbuka watu wa nyumbani kwao Cameroon.

“Nataka kuwasaidia watu wa familia yangu kwanza, kisha nataka kuwapa watoto nchini kwangu fursa kama mimi, walio na ndoto ya kuwa madaktari au kitu kingine wanatakiwa kuzitimiza. Nikifikia ndoto yangu, itaniwezesha kuwasaidia waliopo nchini mwangu ambao wana ndoto zao na hakuna kingine cha kuwakamilishia.

“Nataka kuwapa watoto kama mimi nafasi ya kufuata ndoto zao za mchezo huu na hawana fursa kama mimi. Mara ya mwisho nilipokuwa Cameroon, nilileta vifaa vingi vya masumbwi na MMA kufungua gym. Sasa nimenunua sehemu kubwa ili kuanzisha gym hiyo.

“Watoto wengi nchini Cameroon kwa sababu yangu wana ndoto. Wanasema 'Nitakuwa bingwa katika MMA. Nitafanya masumbwi kama Francis,' kwa sababu waliniona nilipokuwa mdogo. Sikuwa na chochote. Sikuwa na fursa. Na leo, wananiangalia wakiwa na ndoto zao. Wanadhani kuwa kuna uwezekano. Hata wanapokuwa maskini, kuna uwezekano katika maisha. Ni kweli si rahisi. Ni ngumu sana, lakini inawezekana.”

Ngannou alianza kazi ya MMA mnamo Novemba 2013 na kupigana katika Kampuni ya Ufaransa ya 100% Fight, pamoja na mashindano mengine ya kikanda barani Ulaya.

Oktoba 19 mwaka huu, Ngannou alimchapa Renan Ferreira nchini Saudi Arabia katika pambano ambalo kabla hajakwenda kupigana, alikutana na Ronaldo ambaye alimpa maneno ya kumtia nguvu.

Hiyo ilitokana na jinsi Ngannou alivyokuwa akiliendea pambano hilo la kwanza kwake tangu alipotoka kumpoteza mtoto wake wa miezi 15, Kobe aliyefariki siku chache baada ya kutoka kupigwa na Anthony Joshua.

Ikumbukwe kwamba, Ronaldo amepitia majonzi kama hayo baada ya kumpoteza mwanawe wakati anazaliwa mwaka 2022.

Kocha wa Ngannou, Eric Nicksick, alizungumzia ishu hiyo akisema: "Wakati Francis akijiandaa kwa ajili ya pambano, Ronaldo alizungumza kuhusu jinsi alihisi nguvu ya Francis. Akasema: 'Nitampa tu maneno ya kutia moyo...' Alikuwa akizungumzia kuhusu kifo cha mtoto wake na jinsi alivyohusiana na hilo. Ilikuwa ni kitu cha ajabu. Najua ni nyota mkubwa, lakini kukaa naye na kuzungumza kwa karibu ilikuwa kama alikuwa sehemu ya timu kwa wakati huo.”

Ngannou alimpiga Ferreira kwenye raundi ya kwanza, katika pambano la kwanza la MMA kwa Ngannou tangu Januari 2022, aliposhinda taji la UFC kwa ushindi wa pointi dhidi ya Ciryl Gane.

Katika mahojiano baada ya pambano, Ngannou alisema: “Siku mbili zilizopita zilikuwa ngumu sana zikiwa na hisia nyingi. Sikuweza kufanya chochote bila kufikiria kuhusu kifo cha Kobe.

“Nilijaribu kubaki na nguvu na kujisema nifanye kila kitu ili mambo mengine yaendelee, lakini ni ngumu. Ni ngumu tu. Niliingia kwenye pambano hili kwa ajili yake.

“Ninataka watu wakumbuke jina lake kwa sababu bila Kobe, tusingekuwa hapa usiku wa leo, kwa kifupi nisingepigana. Asanteni nyote kwa kuja.”