Foleni tamasha la Simba balaa!

Muktasari:
- Ni wazi kwamba Simba Day inavutia umati mkubwa wa mashabiki, na hali hiyo inaonyesha jinsi tamasha hili linavyokuwa na athari kubwa.
Dar es Salaam. 'Ubaya Ubwela' hadi kieleweke zimesikika sauti za mashabiki wa Simba ambao wamekaa katika nguzo za umeme wakisubiri foleni ya kuingia uwanjani.
Nguzo hizo za chuma zimelazwa chini mita chache kutoka Uwanja wa Benjamin Mkapa ambapo kunafanyika shughuli ya kilele cha tamasha la Simba Day.
Unaambiwa, kutokana na msururu wa mashabiki wengi waliopanga mstari kuingia ndani ya uwanja wengine wakaona wapumzike kidogo kwenye nguzo hizo.
Mashabiki hao wamejazana kwenye nguzo hizo kama sehemu ya kunyoosha miguu baada ya kusimama kwa muda mrefu.
"Ubaya Ubwela hadi kieleweke hatuchoki hii ndio shughuli yetu, tukae tusimame lazima tuingie ndani kuiona Simba yetu mpya," alisema mmoja wa mashabiki.
Baadhi ya mashabiki wakilalamikia utaratibu mbovu wa kuingia uwanjani, kwani foleni imekuwa kubwa na milango ikiwa imefunguliwa baadhi na kuwapa kero waliojihimu mapema tamashani kupata burudani.
Mashabiki lukuki wakiwa wanje ya uwanja huo wameonekana kukosa subira kwa madai utaratibu unawachosha kabla ya kuingia uwanjani.

Kibanda cha kuuza matunda nje ya Uwanja wa Benjamin Mkapa. Picha na Loveness Bernard
Kila biashara inafanyika
Simba haina jambo dogo, achana na nyomi la watu walioingia uwanjani kushuhudia timu hiyo ikiadhimisha kilele cha siku ya Simba Day leo lakini nje ya Uwanjwa wa Mkapa ni kama pamegeuka gulio.
Nje ya uwanja huo ni kama umegeuka gulio kwa kuuza kila aina ya bidhaa kuanzia vyakula, maji na jezi mpya.
Pembezoni kidogo ya uwanja huo wakina mama wauza vyakula wameweka miamvuli wakiuza chakula kama wali, ndizi na vinywaji vya kila aina.
Kwa sasa ukitaka kila aina ya bidhaa unaikuta uwanjani hapo wale wa kuuza makava ya simu, chupa za maji ambazo zimepambwa na nakshi ya rangi nyekundu na nyeupe.
Wauza jezi nao wapo kila karibu ya eneo wakiuza lakini zikitawala zaidi nyekundu na nyeupe huku wengine wakichanganya na njano na kijano za Yanga.