Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Elliott afichua kuondoka Liverpool

Muktasari:

  • Kiungo huyu anataka kuanza maisha mapya, huku nafasi yake ikizidi kuwa finyu Anfield, hasa baada ya Liverpool kumnasa Florian Wirtz.

Harvey Elliott amekuwa mkweli kuhusu mustakabali wake. Huku akikiri kuwa muda wake Anfield unakumbwa na majaribu, nyota huyo wa England chini ya miaka 21 sasa yupo kwenye njia panda ama kusalia Liverpool na kukubali kuwa mchezaji wa akiba, au kutafuta njia mpya ya kuhakikisha kipaji chake kinang’aa.

Kwa mujibu wa Mail Sport, kiungo huyo mwenye umri wa miaka 22 anazivutia klabu tatu ambazo ni Brighton, West Ham na RB Leipzig ya Ujerumani huku Liverpool ikitaja kiasi cha kumsajili cha bei ya chini ni Pauni Milioni 40 (Sh135 bilioni). Hata hivyo, thamani hiyo inaweza kupanda zaidi kutokana na kiwango anachoendelea kukionyesha akiwa na timu ya taifa ya vijana.

Elliott, ambaye alipandishwa Liverpool akitokea Fulham mwaka 2019 kwa ada ya fidia ya Pauni Milioni 4.3, hakupata nafasi ya kuanza mechi katika Ligi Kuu hadi mwezi Mei msimu uliopita, na hiyo ilikuwa baada ya Liverpool kuwa tayari wameshakabidhiwa ubingwa. Katika msimu mzima, alicheza mechi mbili tu katika kikosi cha kwanza kwenye EPL dhidi ya Chelsea na Brighton.

Katika mahojiano yake akiwa kambini na timu ya taifa kabla ya Euro U21, Elliott amefunguka akisema:

“Sasa nina miaka 22, sitaki kuendelea kupoteza muda wa maisha yangu ya soka, maana huu ni muda mfupi sana. Natamani kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza na kucheza kila wiki. Najua haitakuja kirahisi, lakini lazima nitafute njia ya kufanikisha hilo.”

Kauli hiyo inaonyesha wazi nia ya kiungo huyo kuanza maisha mapya, huku nafasi yake ikizidi kuwa finyu Anfield, hasa baada ya Liverpool kutumia zaidi ya Pauni Milioni 200 kwenye dirisha la usajili ikimnasa Florian Wirtz aliyesajiliwa kwa Pauni Milioni 116 ambaye anacheza nafasi moja na Elliott.

Kwa sasa, Elliott amekuwa chaguo la nne kwa nafasi hiyo nyuma ya Wirtz, Dominik Szoboszlai na Curtis Jones. Aidha, hana nguvu ya kutosha kwa nafasi ya kiungo wa chini na amezuiwa kwenye wingi wa kulia na nyota kama Mohamed Salah huku upande wa kushoto ukishikiliwa na Luis Diaz na Cody Gakpo.

Ripoti zinaeleza kuwa kocha Arne Slot, licha ya kuvutiwa na Elliott mwanzoni mwa maandalizi ya msimu, alianza kuwa na mashaka baada ya mchezaji huyo kushindwa kuonyesha kiwango kikubwa mazoezini kufuatia jeraha la mguu lililomuweka nje kwa miezi miwili.

Licha ya Elliott kuonyesha mapenzi ya dhati kwa Liverpool klabu aliyoota kuichezea tangu utotoni mazingira ya sasa yanamlazimisha kutafakari upya.

“Naipenda klabu, napenda kucheza kwa ajili ya beji, lakini kwa wakati mwingine, ni lazima nijifikirie mimi mwenyewe,” alisema wakati wa ziara ya Liverpool jijini Philadelphia msimu uliopita.

Kwa sasa, matarajio ya kuondoka yanaonekana kuwa halisi. Elliott, ambaye amecheza jumla ya mechi 147 na kufunga mabao kadhaa ya kipekee yakiwemo mawili yaliyoipeleka England fainali ya Euro U21 dhidi ya Ujerumani alionekana akiwa katika simanzi kubwa baada ya mechi ya mwisho msimu uliopita, alipomkumbatia baba yake Scott huku akilia kwa uchungu.

Swali linalozuka ni je, Liverpool watamwachia Elliott na kisha wajute kama ilivyotokea Manchester City walipomruhusu Cole Palmer kujiunga na Chelsea? Palmer sasa ameibuka kuwa mmoja wa wachezaji bora zaidi wa kizazi kipya, na Elliott anaonekana kuwa na uwezo huo huo kama tu atapewa muda wa kucheza.

Joe Cole, aliyewahi kuzichezea Liverpool na Chelsea, amesema:

“Nampenda kijana huyu, anacheza mpira kwa njia sahihi. Ana kipaji cha juu, na timu yoyote nje ya sita bora, anaingia kikosi cha kwanza kirahisi. Na baada ya miaka miwili, anaweza kurudi na kushindana tena Liverpool.”

Alienda mbali zaidi akiisifia goli lake dhidi ya Ujerumani:

“Kama Messi angefunga lile bao la pili, dunia nzima ingetulia kumshangilia. Elliott ana kipaji hicho, na ni maumivu kuona anakosa nafasi ya kuonyesha mara kwa mara.”