Chan kufanyika Februari mwakani

Muktasari:
- Fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan) zimefanyika mara nane tofauti na bingwa mtetezi ni Senegal.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf) jana limezihakikishia Kenya, Uganda na Tanzania kuandaa fainali za Chan 2024 huku likitaja tarehe za kufanyika kwake.
Akizungumza muda mfupi baada ya kumalizika kwa kikao cha kamati ya utendaji cha Caf jijini Nairobi, Kenya, Rais wa shirikisho hilo, Patrice Motsepe alisema Chan itafanyika Februari Mosi hadi 28 mwakani.
“Kenya ni nchi inayopenda mpira wa miguu na napenda kuwashukuru wajumbe wote wa kamati ya utendaji. Nina shukrani kwa Rais Ruto (William) kwa jitihada zake.
“Nina uhakika kwamba fainali za mwakani za Chan ndani ya Kenya, Uganda na Tanzania zitakuwa bora zaidi kuliko kuwahi kutokea,” alisema Motsepe.
Motsepe alisema ana imani kubwa fainali za Chan 2024 zitakuwa na manufaa kwa wachezaji.
“Cha itachangia kwa kiasi kikubwa wachezaji kutoka katika hii nchi na nina uhakika mpira wa miguu katika nchi huu utakua,” alisema Motsepe.
Motsepe alipongeza pia jitihada za Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na Rais wa Uganda, Yoweri Museven kwa namna wanavyojitahidi kuhakikisha nchi zao zinakidhi vigezo vya kuandaa Chan na fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) 2027.
Kwa mujibu wa Motsepe, mechi za raundi ya kwanza ya kuwania kufuzu Afcon zitachezwa kuanzia Oktoba 25 hadi 27 mwaka huu.
Hii ni mara ya pili kwa fainali za Chan kufanyika ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo mara ya kwanza zilifanyika Rwanda mwaka 2016.
Timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ imeshiriki mara mbili fainali hizo ambapo mara ya kwanza ilikuwa ni 2009 na ya pili ni 2020.
Mara zote mbili ambazo Taifa Stars imeshiriki Chan, iliishia katika hatua ya makundi.
Mabingwa wa kihistoria wa fainali za Chan ni DR Congo na Morocco ambazo kila moja imetwaa ubingwa wa mashindano hayo mara mbili.
Timu inayotetea ubingwa wa fainali za Chan ni Senegal ambayo ilibeba Kombe kwa kuifunga Algeria kwa mikwaju ya penalti 5-4 baada ya timu hizo kumaliza dakika 120 kwenye mechi ya fainali zikiwa hazijafungana.