Benfica yaiweka mtegoni Liverpool kwa Nunez

Muktasari:
- Usajili wa straika huyo kutoka Uruguay uliripotiwa kuwa na thamani ya Pauni 85 milioni kama ada ya uhamisho, lakini kiasi cha pesa kinalipwa kwa vipengele ikitegemea na kiwango cha mchezaji.
LIVERPOOL, ENGLAND: Liverpool itatakiwa kuilipa Benfica kiasi cha ziada cha Pauni 4.3 milioni ikiwa straika Darwin Nunez ataanza tena mechi ya Ligi Kuu England msimu huu, imeripotiwa.
Usajili wa straika huyo kutoka Uruguay uliripotiwa kuwa na thamani ya Pauni 85 milioni kama ada ya uhamisho, lakini kiasi cha pesa kinalipwa kwa vipengele ikitegemea na kiwango cha mchezaji.

Inaelezwa wakati anasajiliwa Liverpool ililipa Pauni 64 milioni na kiasi kilichosalia kinalipwa kidogo kidogo kulingana na kiwango chake ambapo kumewekwa vipengele ikiwa ataanza kiasi fulani cha mechi, kufunga idadi fulani ya mabao na kila kipengele kina kiasi chake cha pesa, lakini vyote ukivijumlisha ndio unapata ada kamili ya Pauni 85 milioni.
Hata hivyo, muda wake katika viunga vya Anfield unaonekana kuwa unakaribia kumalizika. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 ameanza mechi moja ya ligi tangu kuanza mwaka huu dhidi ya Southampton, na anahusishwa kuondoka mwisho wa msimu.

Baadhi ya taarifa zinaeleza kutoanzishwa kwake katika mechi za EPL kunaweza kuwa ni ishu ya kifedha inazoweza kulipa Liverpool kwa kumtumia.
Taarifa zinaeleza kwamba ikiwa Nunez ataanza katika mechi 50 za Ligi Kuu England, Liverpool itatakiwa kulipa Pauni 4.3 milioni hiyo ikiwa ni mara ya tatu baada ya kuwa tayari imeshalipa kiasi cha pesa kwa staa huyo kuanza kwenye mechi 10 na 25 za EPL.

Nunez ameanza mara nane katika mechi za ligi msimu huu, huku akicheza mara nyingine 17 kama mchezaji wa akiba.