Bacca aibeba Yanga Sokoine

Muktasari:
- Ushindi huo unakuwa wa pili kwa Yanga katika Ligi Kuu Bara katika michezo miwili iliyocheza hadi sasa baada ya mechi ya kwanza dhidi ya Kagera Sugar iliyopigwa kwenye Uwanja wa Kaitaba Bukoba Agosti 29, mwaka huu kushinda mabao 2-0
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara timu ya Yanga, imeendeleza vyema kampeni zake za kutetea ubingwa wa michuano hiyo kwa msimu huu baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0, dhidi ya KenGold katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Yanga ilipata bao la kwanza dakika ya 13 kupitia kwa beki wa kati wa kikosi hicho, Ibrahim Hamad 'Bacca' aliyepokea pasi safi iliyopigwa na kiungo mshambuliaji, Stephane Aziz Ki na kupiga kichwa kilichomshinda kipa wa KenGold, Casto Mhagama ambaye alionyesha kiwanfo cha juu kwenye mchezo huu.
Kikosi hicho cha Kocha Mkuu, Miguel Gamondi kiliingia katika mchezo huo kikitoka kushinda kwa ushindi mnono wa mabao 6-0, dhidi ya CBE SA kutoka Ethiopia kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo kilitinga hatua ya makundi ya michuano hiyo.
Ushindi huo unakuwa wa pili kwa Yanga katika Ligi Kuu Bara katika michezo miwili iliyocheza hadi sasa baada ya mechi ya kwanza dhidi ya Kagera Sugar iliyopigwa kwenye Uwanja wa Kaitaba Bukoba Agosti 29, mwaka huu kushinda mabao 2-0.
Pia, Yanga imeendeleza rekodi yake nzuri ya kutopoteza ugenini katika mchezo wa Ligi Kuu Bara kwani tangu mara ya mwisho ilipofungwa na Ihefu ambayo inajulikana kama Singida Black Stars mabao 2-1, Oktoba 4, 2023, haijapoteza tena hadi sasa.
Mchezo wa mwisho kwa Yanga kupoteza wa mashindano ulikuwa ni wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya robo fainali dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ilipochapwa kwa penalti 3-2, baada ya suluhu michezo yote miwili Aprili 5, mwaka huu.
Baada ya mchezo huo, Yanga imecheza jumla ya michezo 22 ya mashindano tofauti tofauti ambapo kati ya hiyo imeshinda 21 na kutoka suluhu mmoja tu uliokuwa dhidi ya Maafande wa JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo Aprili 24, 2024.
Kwa upande wa KenGold ambao ni wageni wa Ligi Kuu Bara imeendeleza unyonge kwani katika michezo mitano iliyocheza tayari imepoteza yote, jambo linaloonyesha wazi kikosi hicho cha Kaimu Kocha Mkuu, Jumanne Challe kina kazi kubwa ya kufanya ingawa kwenye mechi hii kimeonyesha mabadiliko makubwa.
KenGold ilianza Ligi Kuu Bara kwa kichapo cha mabao mabao 3-1, dhidi ya Singida Black Stars Agosti 18, 2024, ikachapwa tena 2-1 mbele ya Fountain Gate Septemba 11, ikafungwa bao 1-0 na KMC, kisha kuchapwa na 'Wanankurunkumbi' Kagera Sugar 2-0.
Timu hiyo ilikuwa na mwenendo mzuri katika Ligi ya Championship msimu uliopita ambapo ilitwaa ubingwa huo kwa kukusanya jumla ya pointi 70, katika michezo 30 iliyocheza ambapo kati yake ilishinda 21, sare saba na kupoteza miwili kwa msimu mzima.
Katika mchezo wa mapema uliopigwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo Mbweni, wenyeji JKT Tanzania ilipata ushindi wa kwanza msimu huu wa mabao 2-1, dhidi ya Coastal Union ikiwa ni kichapo cha nne mfululizo kwa kikosi hicho cha Tanga.
JKT ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Hassan Dilunga kwa mkwaju wa penalti dakika ya 14, kisha Coastal ikachomoa kupitia kwa mshambuliaji wa timu hiyo Mkenya, John Makwata dakika ya 26 na Shiza Kichuya akafunga la pili dakika ya 48.
Coastal Union inayonolewa na Kaimu Kocha Mkuu, Joseph Lazaro imecheza jumla ya michezo mitano ya Ligi Kuu Bara kwa msimu huu huku ikiwa haijaonja ladha ya ushindi baada ya kufungwa minne na kutoa sare mmoja tu wa bao 1-1, dhidi ya KMC Agosti 29.
Kwa upande wa JKT Tanzania imecheza michezo minne ambapo ushindi wa jana ni wa kwanza baada ya awali kutoka sare mechi tatu mfululizo.