Azam vs Simba: Vita ya wakubwa Amaan leo

Muktasari:
- Katika mchezo huo wengi wanasubiri kuona pale katikati ya uwanja patakavyokuwa patamu kutokana na aina ya wachezaji wa timu hizo zote mbili waliopo.
Walioona Septemba 26 ni mbali leo hii watajiuliza mbona imefika mapema. Wanasahau kwamba siku hazigandi.
Mzizima Dabi imepiga hodi na leo inachezwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar wakati Azam FC ikiwa mwenyeji wa Simba ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Bara, huku vita kubwa ikionekana kuwa kwenye eneo la kiungo na ufungaji.
Katika mchezo huo utakaoanza saa 2:30 usiku, wengi wanasubiri kuona pale katikati ya uwanja patakavyokuwa patamu kutokana na aina ya wachezaji wa timu hizo zote mbili waliopo.
Kama ilivyokuwa msimu uliopita ambapo Mzizima Dabi ya mzunguko wa kwanza ilipigwa ardhi ya ugenini pale CCM Kirumba jijini Mwanza, Februari 9, 2024, safari hii tena inapigwa Zanzibar.
Huu ni mchezo ambao Azam na Simba kila mmoja anataka kuona akifanya vizuri ikizingatiwa kwamba ni mwanzoni mwa ligi hivyo hesabu lazima ziwe mapema.
Hii itakuwa ni dabi ya pili kwa Kocha Fadlu Davids tangu atue nchini msimu huu kuiona Simba akianza na Kariakoo Dabi katika Ngao ya Jamii aliyopoteza kwa bao 1-0.
Richad Taoussi, ambaye ameiongoza Azam FC katika mechi tatu za ligi tangu akabidhiwe kikosi hicho baada ya kuondoka kwa Yousouph Dabo, anakwenda kucheza dabi yake ya kwanza.
Wakati mara ya mwisho Simba ilishuhudiwa ikitakata Mzizima Dabi kwa ushindi wa mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Mei 9, 2024, matarajio ya Azam FC leo ni kufanya vizuri chini ya kocha mpya.
Mechi yenyewe
Leo mashabiki watarajie kuona mchezo uliochangamka kutokana na aina ya wachezaji waliopo katika vikosi hivyo, huku pia uwanja wanaoutumia ukiruhusu kufanya mambo mengi mazuri dakika zote 90.
Sehemu ya kuchezea ya Uwanja wa New Amaan Complex ni rafiki sana kwa timu kucheza soka la pasi za chini na kufika kwa usahihi tofauti na ilivyokuwa Mzizima Dabi ya kwanza msimu uliopita pale CCM Kirumba.
Kama unakumbuka, Mzizima Dabi ya pili msimu uliopita iliyochezwa Benjamin Mkapa, watu walifurahia kuona soka safi kwa sababu ya uwanja kuruhusu mbinu nyingi kutumiwa na makocha.
Kinachoonekana leo ni kwamba, Azam iliyoanza msimu kwa taratibu baada ya suluhu mbili mfululizo na baadaye kuamka kwa kushinda mechi mbili zilizofuatia kwa jumla ya mabao matano huku nyavu zake zikiendelea kuwa salama hazijaguswa, kuna kitu wamekipania.
Chini ya kocha mpya, Rachid Taoussi raia wa Morocco, timu hiyo kuna baadhi ya wachezaji anawatumia kikosi cha kwanza ambapo anaamini wana uwezo mkubwa wa kumpa matokeo mazuri.
Pale eneo la mbele, kuna Idd Nado, Feisal Salum na Nassor Saadun ambapo Kocha Taoussi amekuwa akiwatumia na kumpa matokeo chanya katika mechi mbili za mwisho dhidi ya KMC na Coastal Union.
Licha ya kwamba Fei Toto bado hajafunga bao katika mechi nne alizocheza kwa dakika 270, lakini ana asisti tatu sawa na Jean Charles Ahoua wa Simba.
Saadun ni kama amewaka, ana mabao mawili ambayo yote ya kideoni huku Idd Nado akitumika kuzisumbua ngome za wapinzani kutokea pembeni akiwa ndiye mfungaji wa bao la kwanza la Azam katika ligi msimu huu akifanya hivyo dhidi ya KMC waliposhinda 4-0.
Nyota hao watatu ni wazi watakuwa wasumbufu kwa safu ya ulinzi ya Simba ambayo hivi sasa unaweza kusema Kocha Fadlu Davids anawaamini zaidi Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Che Malone Fondoh na Abdulrazack Hamza, wakati golini akikaa Moussa Camara ambaye bado hajaruhusu bao kwenye ligi.
Ukiachana na hilo, pale kati napo patakuwa bize kwa viungo watakaokuwa wakifanya kazi mbli kwa wakati mmoja, kwanza kupishana kupeleka mipira mbele kwa mpinzani na kuzuia isipenye kwao.
Kazi kubwa ya kuzuia mipira isipite upande wa Azam na kupelekwa itafanywa na James Akaminko na Adolf Mtasingwa ambao katika mechi nne za ligi timu hiyo ilizocheza viungo hao wamecheza zote wakianza kikosi cha kwanza.
Kukosekana kwa Sospeter Bajana na Yahya Zayd ambao walikuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kabla ya kurejea hivi karibuni wakianza mazoezi, kumetoa nafasi kubwa kwa Akaminko kutumika zaidi ambapo wakati mwingine akipishana na Yannick Bangala na Ever Meza wanaoingia baadaye.
Simba eneo lao la kiungo pale kati unaweza kusema lipo salama chini ya Deborah Fernandes Mavambo akishirikiana na Yusuph Kagoma. Wawili hao wameonekana wakicheza kwa kushirikiana vizuri na kuifanya timu hiyo kuwa imara.
Kagoma amepata nafasi ya kucheza baada ya Mzamiru Yassin kuumia, lakini pia naye mchezo uliopita dhidi ya Al Ahli Tripoli alipata majeraha akashindwa kumaliza mechi.
Kuna Fabrice Ngoma na Augustine Okejepha, nao wamekuwa tayari muda wote kuingia uwanjani kukichafua na wakipewa nafasi huwa wanafanya kweli
Ufundi mwingi aliokuwa nao Mavambo sambamba na uwezo wake mkubwa wa kupiga mashuti makali, yanaweza kuwa balaa kwa Azam ambayo leo inaweza kuendelea kumtumia kipa wake chipukizi, Zuber Foba ambaye amedaka mechi tatu za mwisho.
Foba katika mechi hizo tatu dhidi ya Pamba Jiji, KMC na Coastal Union, amefanikiwa kumaliza bila ya kuruhusu bao kitu ambacho ni kizuri kwake.
Eneo lao la ulinzi, Kocha Taoussi imani yake kubwa ipo kwa nahodha Lusajo Mwaikenda, Yoro Diaby, Yeison Fuentes na Nathaniel Chilambo ambaye mara ya mwisho alishindwa kumaliza mchezo dhidi ya Coastal Union baada ya kuumia, hivyo kuna uwezekano akakosekana leo akacheza Pascal Msindo eneo lake.
Msindo ambaye kiuhalisia ni beki wa kushoto, lakini Taoussi mara kadhaa amemtumia kama winga katika mechi mbili za mwisho ambazo zote wameshinda.
Ukiangalia viungo wa Azam, Akaminko na Mtasingwa, uchezaji wao unashabihiana na wale wa Simba, Mavambo na Kagoma, kwani Kagoma na Akaminko wana uwezo wa kukaa chini sana huku Mavambo na Mtasingwa wakicheza juu na chini.
Matokeo yataamua
Haijawahi kuwa mechi rahisi zinapokutana timu hizi kwani tulishuhudia katika fainali ya Kombe la Muungano iliyochezwa Aprili 27 mwaka huu hapohapo New Amaan Complex timu hizo zikitoa ushindani mkubwa kabla ya kiungo wa Simba, Babacar Sarr ambaye hivi sasa hayupo akifunga bao pekee la ushindi dakika ya 77. Simba wakashinda 1-0 na kuwa mabingwa.
Katika ligi msimu uliopita, Simba ilishinda mechi ya pili wakiwa wageni baada ya ile ya kwanza kutoka sare ya bao 1-1.
Rekodi zinaonyesha kwamba, Azam katika mechi zake tano za mwisho za kimashindano msimu huu, haijafanya vizuri sana kulinganisha na Simba.
Azam katika mechi hizo tano, imeshinda mbili, sare mbili na kupoteza moja. Wakati Simba ikishinda nne na sare moja.
Matokeo ya wenyewe kwa wenyewe mechi tano za mwisho ndani ya ligi kuu pekee, sare ni tatu, huku kila mmoja akishinda mechi moja.
Katika sare zilizopo mechi tano za mwisho, matokeo yamefanana yakiwa ni 1-1, Azam iliposhinda ilikuwa 1-0, wakati Simba ilishinda 3-0.
Matokeo ya leo yataamua nafasi kwa kila mmoja, ushindi kwa Azam utawafanya kufikisha pointi 11 baada ya mechi 15, wakati Simba yenyewe ikishinda itakuwa na pointi tisa katika mechi tatu na kuendeleza rekodi yao ya ushindi asilimia mia katika ligi msimu huu kwani mechi mbili za kwanza ilizocheza imeshinda zote na kufunga mabao saba, haijaruhusu nyavu zake kutikiswa.
Hadi sasa timu zote nyavu zao hazijatikiswa, leo tunaweza kushuhudia kwa mara ya kwanza wakiokota mpira nyavuni kwani kila mmoja ana safu nzuri ya ushambuliaji.
Ongezeko la mshambuliaji Leonel Ateba akishirikiana na Jean Charles Ahoua, Kibu Denis na Joshua Mutale pale mbele, safu ya ulinzi ya Azam ijipange kisawasawa kuzuia balaa lao kwani Al Ahli Tripoli walichokutana nacho wikiendi hawatakisahau.
Kauli ya makocha
Akizungumzia mchezo huo, Taoussi alisema: “Ni mchezo muhimu kushinda kwa sababu utatafanya tupande nafasi katika msimamo wa ligi. Tumefanya maandalizi na wachezaji wapo katika ari nzuri. Mazingira ni rafiki hapa. Endapo wachezaji watacheza kama vile ambavyo tumefanyia mazoezi basi naamini tutaondoka na ushindi.”
Fadlu alisema: “Tunakwenda kucheza mechi yetu ya tatu ya ligi dhidi ya mpinzani mgumu. Tunafahamu umuhimu wa mchezo huo hivyo tumejiandaa vizuri. Tumekuwa na siku mbili za mazoezi tangu tutoke katika mchezo wa mwisho. Nina wachezaji wengi ambao wanaweza kufanya vizuri katika mchezo huu bila kujali nani anakosekana.”