Azam FC kwenye mtihani mzito Zanzibar

Muktasari:
- Rekodi zinaonyesha katika michezo ya Ligi Kuu Bara baina ya timu hizo iliyochezwa Septemba, Azam FC haijawahi kushinda kwa Simba zaidi ya kuambulia sare miwili na kuchapwa miwili jambo linalosubiriwa kuona kama wataivunja.
Macho na masikio ya mashabiki wa soka nchini yanaelekezwa katika mchezo wa Dabi ya Mzizima kati ya Azam na Simba utakaopigwa kesho kwenye Uwanja wa New Complex Amaan Zanzibar kuanzia saa 2:30 usiku, huku rekodi zikiwakataa matajiri wa Jiji la Dar.
Rekodi zinaonyesha katika michezo ya Ligi Kuu Bara baina ya timu hizo iliyochezwa Septemba, Azam FC haijawahi kushinda kwa Simba zaidi ya kuambulia sare miwili na kuchapwa miwili jambo linalosubiriwa kuona kama wataivunja.
Mchezo wa kwanza kukutana ulikuwa Septemba 11, 2010 uliopigwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga ambapo Simba ilishinda mabao 2-1 yaliyofungwa na nyota wa zamani, Nico Nyagawa na Mussa Hassan ‘Mgosi’. Bao pekee kwa Azam FC lilifungwa na aliyekuwa nyota wa timu hiyo, Ramadhan Chombo ‘Redondo’ huku ikikumbukwa aliyekuwa nahodha wa kikosi hicho, John Bocco alitolewa nje dakika ya 12 kwa kuonyeshwa kadi nyekundu.
Mchezo uliofuata ulipigwa Septemba 11, 2011 ambapo miamba hiyo ilitoka suluhu na uliofuata Septemba 17, 2016, Simba ilishinda bao 1-0 lililofungwa na aliyekuwa winga wa kikosi hicho, Shiza Kichuya dakika ya 69. Mchezo wa nne wa Ligi Kuu Bara kukutana ulipigwa Septemba 9, 2017 na kuisha kwa suluhu na baada ya miaka saba kupita zinakutana tena jambo linalosubiriwa kuona kama Simba itaendeleza ubabe au Azam FC itavunja mwiko.
Mbali na rekodi hizo, ila hata mchezo wa mwisho kukutana uliopigwa Uwanja wa New Amaan Zanzibar ulikuwa ni wa fainali ya Kombe la Muungano Aprili 27, mwaka huu na Simba ilishinda bao 1-0, lililofungwa na nyota wa zamani wa timu hiyo, Babacar Sarr.
Katika Ligi Kuu Bara, mchezo wa mwisho kwa miamba hiyo kukutana ulipigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Mei 9, mwaka huu ambapo Simba iliibuka kidedea kwa mabao 3-0, yaliyofungwa na Sadio Kanoute, Fabrice Ngoma na David Kameta ‘Duchu’.
Azam FC itakutana na Simba chini ya kocha mpya, Fadlu Davids ambaye ameshinda michezo yote miwili ya Ligi Kuu Bara hadi sasa aliyoiongoza baada ya kuifunga Tabora United kwa mabao 3-0, Agosti 18, kisha kuichapa Fountain Gate 4-0, Agosti 25.
Kwa upande wa Azam ambayo pia iko chini ya kocha mpya Mmorocco, Rachid Taoussi, ilianza Ligi Kuu Bara kwa suluhu mbili mfululizo dhidi JKT Tanzania na Pamba kisha kuzinduka kwa KMC kwa kuichapa mabao 4-0, na kuifunga Coastal Union bao 1-0.
Kwa mara ya kwanza kabisa kwa timu hizi kukutana katika mchezo wa Ligi Kuu Bara ilikuwa ni Oktoba 4, 2008 ambapo Azam FC ilishinda kwa mabao 2-0, yaliyofungwa na waliokuwa mastaa wa kikosi hicho, Jamal Mnyate na Shekhan Rashid kwa penalti.
Tangu mwaka 2008, Azam FC ilipoanza kushiriki Ligi Kuu Bara baada ya kulibadilisha jina hilo ikitoka kuitwa Mzizima FC chini ya Kocha, Mohamed Seif ‘King’, imekutana na Simba katika michezo 32, ikishinda sita tu, sare 12 na kuchapwa 14.
Akizungumzia maandalizi ya kikosi hicho, Kocha Mkuu wa Azam FC, Rachid Taoussi aliyechukua nafasi ya Youssouph Dabo aliyetimuliwa Septemba 3 kutokana na mwenendo mbaya wa matokeo alisema, morali ya wachezaji imeimarika zaidi.