Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Arsenal yamaliza maandalizi kibabe, sasa ni Premier

Muktasari:

  • Huu ni ushindi mkubwa zaidi wa Arsenal kwenye mechi za maandalizi ya msimu mpya, baada ya kutoka Marekani ilipocheza michezo minne.

London, England. Arsenal imeendeleza umwaba wake kwenye michezo ya maandalizi ya msimu baada ya kuichapa Bayern Leverkusen 4-1 kwenye Uwanja wa Emirates, London.

Huu ni ushindi mkubwa zaidi wa Arsenal kwenye mechi za maandalizi ya msimu mpya, baada ya kutoka Marekani ilipocheza michezo minne.

Bukayo Saka pamoja na  Declan Rice ambao walikuwa na timu ya taifa ya England kwenye mashindano ya Euro waliungana na wenzao kwa mara ya kwanza kwenye mchezo huo ikiwa ni wiki moja kabla Ligi Kuu England, Premier haijaanza.

Arsenal imefunga mabao yake kupitia kwa wachezaji wake wanne Alexandr Zinchenko, Leandro Trossard, Gabriel Jesus na Kai Havertz huku Leverkusen ikifunga kupitia kwa Adam Hlozek kwenye mchezo ambao kila timu ilifanikiwa kuonyesha kiwango cha juu.

Huu ulikuwa mchezo wa kwanza Arsenal inacheza kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Emirates baada ya kukosa ubingwa wa Ligi Kuu England siku ya mwisho uliochukuliwa na Manchester City.

Hata hivyo, kuna mambo matano ambayo shabiki wa Arsenal anatakiwa kuyafahamu kabla ya kuanza msimu mpya wa Ligi Kuu England, Premier.


Zinchenko haendi kokote

Taarifa ya juzi ambayo iliyoonyesha kuwa beki wa Arsenal Zinchenko amebadilisha jezi kutoka namba 35 hadi 17, inaonyesha kuwa sasa beki huyo hawezi tena kuondoka kwenye timu hiyo katika dirisha hili la usajili.

Awali ilielezwa kuwa baada ya usajili wa Riccardo Calafiori na kurejea uwanjani kwa  Jurrien Timber kutoka kwenye majeraha kulianza kutia shaka uwepo wa Zichenko kwenye kikosi hicho.

Pamoja na jezi hiyo, uwezo wake kwenye mchezo huu umeonyesha kuwa bado anataka kubaki kwenye kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao wa ligi.

Mashabiki wa Arsenal walimshangilia beki huyo raia wa Ukraine na kuonyesha kuwa wanataka kumuona akibaki kwenye kikosi hicho.

Hata hivyo, ni beki mwingine ambaye anaweza kucheza kama winga kutokana na uwezo wake wa kupiga krosi na kuingia ndani ya boxi.


Arsenal kuendelea kumtumia Jesus

Kiwango cha fedha ambacho Arsenal imekitumia kwa Calafiori kinaonyesha kuwa timu hiyo haiwezi kuingia tena sokoni kwenye dirisha hili ili kutafuta mashambuliaji.

Hata hivyo, kitendo cha kufunga mabao 91 kwenye msimu uliopita, kinaonyesha kuwa Arteta anachotakiwa kwa sasa ni kuhakikisha anakuwa na safu bora tu ya ulinzi kwenye kikosi chake ili kufanikiwa kuwania ubingwa wa Premier tena msimu ujao na kitendo cha kumsajili Calafiori kinaonyesha kuwa huu ni mwanzo mzuri.

Baada ya Gabriel Jesus kuingia kwenye mchezo huo kuliifanya timu hiyo kubadilika kwenye eneo la ushambuliaji, hali ambayo inampa imani Mikel Arteta kuwa timu hiyo inaweza kufanya vizuri kwenye msimu ujao wa ligi bila kuongeza mshamuliaji mwingine.

Arsenal inaamini kama mchezaji huyo akiwa fiti kwa asilimia 100 bado anaweza kuongoza eneo la ushambuliaji la timu hiyo, bao alilofunga ni kielelezo kwa bado anaweza kufanya mambo makubwa kwenye timu hiyo.


Marafiki wakutana pamoja

Mechi hii ilimshuhudia kiungo wa zamani wa Arsenal, Granit Xhaka akirejea tena kwenye Uwanja wa Emirates na kufurahia pamoja na wachezaji wengi aliowaacha klabuni hapo sehemu aliyokaa kwa miaka saba.

Lakini ilikuwa ni siku nyingine ya kukutana kwa marafiki wawili Xabi Alonso pamoja na Mikel Arteta wa Arsenal, ambao waliwahi kuwa na urafiki mkubwa wakati wa makuzi yao.

Hakukuwa na tofauti kubwa sana ya jinsi wanavyoziongoza timu zao huku kila moja ikionekana kucheza soka la kisasa, msimu uliopita Leverkusen, ilitwaa ubingwa wa Ujerumani bila kupoteza huku miaka 20 nyuma Arsenal nayo ikiwa imefanya hivyohivyo.

Huu utakuwa mchezo wa mwisho kabla ya timu hizo kuingia kwenye maandalizi ya mwisho kabisa ya ligi hiyo, huku Arsenal ikitarajiwa kupata ushindani kutoka kwa Liverpool, Manchester United na Man City, lakini Leverkusen yenyewe inategemea upinzani kutoka kwa Bayern Munich na Borrusia Dortmund.


Saka na Rice warejea kamili

Kitendo cha kuingia kwa Bukayo Saka na Declan Rice ilikuwa ni mara yao ya kwanza kuonekana wakiwa na jezi mpya ya Arsenal baada ya kupata mapumziko walipomaliza michuano ya Euro wakiwa na England.

Wachezaji hao pamoja na David Raya na Aaron Ramsdale, baada ya kuwa kwenye Euro hawakusafiri na timu hiyo kwenye kambi ya maandalizi nchini Marekani.

Hata hivyo, kiwango cha Rice kilionyesha kuwa ana kazi kubwa ya kufanya kabla ya mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu England dhidi ya Wolves.

Kwa upande wa Saka alionekana kuanzia pale alipoishia msimu uliopita akitoa pasi safi ya bao kwa Kai Havertz.


Gabriel na Saliba kama kawaida

Mchezo wa maandalizi ya msimu dhidi ya Liverpool uliwasababishia majeraha wachezaji wawili mahiri wa timu hiyo Gabriel pamoja na Saliba, lakini kwenye mchezo huu walionekana kuwa fiti na wote kuanza.

Safu hii ya ulinzi ndiyo ambayo iliiwezesha Arsenal kuwania ubingwa hadi mwishoni kabisa mwa msimu.

Kiwango chao waliichoonyesha kwenye mechi hii kilitosha kuonyesha kuwa bado timu hii itakuwa na safu imara ya ulinzi kuelekea kwenye mchezo wa ligi wiki ijayo .

Washambuliaji wengi wa Leverkusen walishindwa kumfikia kwa karibu kipa wa Arsenal kutokana na ubora walioonyesha walinzi hao wa kati kwenye mchezo huu.