Prime
Arajiga na Sasii ishu yao huruma tu

KAMATI ya Waamuzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ipo kwenye mchakato wa kuwaombea nafasi ya kuchezesha mechi za Ligi Kuu Bara waamuzi zaidi ya 20 waliokuwa wamesimamishwa msimu uliopita.
Waamuzi hao walisimamishwa kutokana na sababu mbalimbali za kinidhamu na kikanuni hivyo kushindwa kumalizia ratiba zao kama walivyokuwa wamepangwa.
Miongoni mwa waamuzi hao ni Ahmed Aragija, Elly Sasii, Emmanuel Mwandembwa, Hussein Athman, Nassoro Mwinchui, Florentina Zabron, Amina Kyando, Raphael Ikambi, Jackson Parangyo na Hans Mabena.
Wengine ni Rashid Zongo, Kassim Mpanga, Frednand Chacha, Sudi Lila, Herbeth Malime, Ahmed Simba, Marry Mwakitalama, Hamis Chang’aru na Jesse Erasmo.
Katika mahojiano maalumu yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi, Nassoro Hamduni alisema jukumu lao ni kuwasaidia waamuzi katika changamoto wanazokutana nazo sehemu ya kazi lakini wao sio wenye maamuzi ya mwisho kwa mwamuzi ambaye amefungiwa kumrudisha kazini.
“Hivi sasa kwenye kazi ya uamuzi hata watu wanaona kuna heshima inarudi, msimu uliopita walisimamishwa waamuzi zaidi ya 20, ligi ilimalizika kwa uzuri kwani waliobaki walicheza vizuri na ndio maana wanawake walipewa nafasi kubwa kuchezesha mechi na walituheshimisha. “Kuna mambo mengi hutokea kwenye kazi, tulifanya uchunguzi wa kina maana makosa yalikuwa mengi na tulichukua hatua.”
“Tunawaombea nafasi ya kurudi kuchezesha msimu huu kwa sababu kamati ya waamuzi haina mashindano, mashindano ni ya Bodi ya Ligi na TFF kupitia Katibu Mkuu, kama katibu mkuu sababu tutakazompa na kama ataona wako tayari na bodi watakubali basi watapangwa kwenye ratiba, kama wenye ligi watakataa basi hatutakuwa na namna nyingine.” alisema Hamduni.
Kiongozi huyo alifafanua zaidi juu ya kazi hiyo inahitaji mtu mwenye nidhamu, kujituma na kuzingatia miiko yote wanayofundishwa.
“Sifa kubwa ya uamuzi lazima uwe na kazi kwa maana ajira inayokuingizia mshahara maana huku kwenye uamuzi hakuna mshahara ni posho tu, ajira ya huku ni pale unapopangwa kwenye ratiba na inaisha pale ratiba yako uliyopangwa imemalizika.”
Alisema kuwa anaamini kwasasa waamuzi wote wamepata funzo zaidi kupitia msimu uliopita kwani kamati haikufumbia macho hata kwa waamuzi wanaotambulika na FIFA kuwasimamisha mara wanapofanya makosa.