Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Anayedaiwa kuua mke, kuteketeza mwili alivyojibu maswali ya mawakili

Muktasari:

  • Mshtakiwa Hamisi Luwongo anadaiwa alimuua mkewe Mei 15, 2019 nyumbani kwao kisha akauchoma mwili wake kwa moto kwa kutumia magunia mawili ya mkaa ndani ya banda la kuku, majivu na masalia ya mwili akayazika shambani na kupanda mgomba juu yake.

Dar es Salaam. Mshtakiwa Hamisi Luwongo, anayeshtakiwa akidaiwa kumuua mkewe na kuuteketeza kwa moto mwili wake, amefunga ushahidi kwa kuhojiwa na waendesha mashtaka kuhusu utetezi wake, akiutaka upande huo umweleze alipo mkewe.

Luwongo ambaye pia anaitwa Meshack alitoa utetezi Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam, mbele ya Jaji Hamidu Mwanga, baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi. Mahakama ilimuona ana kesi ya kujibu.

Katika kesi ya jinai namba 44/2023, mshtakiwa mkazi wa Gezaulole, wilayani Kigamboni, Dar es Salaam anakabiliwa na shtaka la mauaji ya mkewe, Naomi Marijani kinyume cha kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, kama ilivyorejewa mwaka 2019.

Anadaiwa alimuua mkewe Mei 15, 2019 nyumbani kwao kisha akauchoma mwili wake kwa moto kwa kutumia magunia mawili ya mkaa ndani ya banda la kuku na majivu na masalia ya mwili akayazika shambani kwake Mkuranga na kupanda mgomba juu yake.

Akiongozwa na wakili wake Hilda Mushi, mshtakiwa Luwongo pamoja na mambo mengine alikiri kuwaeleza polisi kuwa ndiye aliyemua mkewe na kuuchoma moto mwili wake na kwenda kuwaonyesha alikofanyia mauaji hayo na mahali alikozika majivu na masalia yake.

Hata hivyo alisema maelezo hayo hayakuwa ya kweli, bali aliwadanganya polisi ili kujiepusha na mateso ya kipigo wakimtaka awaonyeshe iliko maiti ya mkewe.

Alidai masalia ya mifupa aliyowaonyesha hayakuwa ya mkewe, bali ya mtu mwingine yaliyosalia kwenye kaburi lililohamishwa kwenye shamba alilonunua pamoja na ya mzoga wa mnyama.

Baada ya ushahidi haya ni majibu ya baadhi ya maswali ya dodoso aliyoulizwa na mawakili akianza Wakili wa Serikali Mwandamizi Ashura Mnzava:

Wakili: Shahidi, ilikuwaje ukawa mtuhumiwa namba moja?

Shahidi: Yule ni mke wangu na hata kama mimi nisingeonekana yeye angekuwa mtuhumiwa wa kwanza.

Wakili: Nitakuwa sawa kuwa wewe ulishawahi kupelekwa Mirembe kuchunguzwa akili?

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili: Kwa nini hukuiambia mahakama kuwa ulikwenda huko?

Shahidi: Kwa sababu taarifa iko mahakamani.

Wakili: Umesema kuna kaburi ulilikuta shambani, hilo kaburi ni la nani?

Shahidi: Sijui ni la nani.

Wakili: Hata hiyo mifupa uliyoitoa kwenye hilo kaburi hujui ni ya nani?

Shahidi: Nilisema lile shamba baada ya makubaliano (na waliomuuzia) niliwaambia hili kaburi mnalifanyaje, wakasema watalihamishia kwenda shamba lingine na wakaleta watu ambao hawakufanya kazi yao vizuri.

Wakili: Uliwahi kumwandikia Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), barua ya kuomba kukiri kosa la kuua bila kukusudia?

Shahidi: Uko sahihi.

Wakili: Una tatizo kama tukiiomba mahakama iipokee kama kielelezo?

Shahidi: Aah! hili suala sipendi litolewe kama kielelezo sijui uliitolea wapi baki nayo tu wewe mwenyewe.

Wakili: Wakati huo (tukio la mauaji anayotuhumiwa) ilikuwa unatumia simu gani?

Shahidi: Siikumbuki.

Wakili: Na zile zilizoletwa mahakamani hapa ni zako?

Shahidi: Kwanza nashangaa mimi nilikuwa na simu nyingi lakini simu zangu nyingine hapa sikuziona.

Wakili: Nilikusikia ukisema kuwa Naomi hajafa, una uthibitisho gani kuwa Naomi siyo marehemu?

Shahidi: Kwa sababu mke wangu hajafariki.

Wakili: Mara ya mwisho wewe kuwasiliana naye ni lini?

Shahidi: Siikumbuki.

Wakili: Kwa nini ulikaa kimya kwa miezi yote hiyo miwili tangu ulipomuua (mkewe Naomi) marehemu?

Shahidi: Mimi sijamuua.

Wakili: Uliiambia mahakama kuwa kile kielelezo cha tisa cha upande wa mashtaka, mabaki ya marehemu Naomi si yake, sasa hayo mabaki mengine ya huko porini unayosema umeyaleta hapa mahakamani?

Shahidi: Hayo mabaki niliyoya-fabricate (ya kutunga) sikuyaleta mahakamani, si niliwakabidhi polisi ndiyo waliyaleta sasa mimi ningeyatoa wapi?

Akijibu maswali ya wakili wa Serikali Mkuu, Yasinta Peter alisema:

Wakili: Shahidi, uliwahi kusema mbele ya mheshimiwa Rugemalira (Mahakama ya Kisutu) kuwa uko tayari kunyongwa lakini unyongwe kwa haki sikukusudia kuua, ni sahihi?

Shahidi: Sikumbuki.

Wakili: Ulisema Naomi alikushika sehemu za siri, hebu ionyeshe Mahakama ulisimamaje mpaka akakushika hizo?

Shahidi: Hiyo scenario siikumbuki, nilisema alinishika … sehemu za siri lakini kwamba alikata style gani siikumbuki.

Wakili: Baada ya scenario ya wewe kushikwa sehemu za siri mpaka leo unasimama hapa mahakamani Naomi hajawahi kuonekana, ni sahihi?

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili: Kwa mujibu wa ushahidi wa upande wa mashtaka aliyesababisha mpaka uchunguzi ukafanyika mpaka leo tuko mahakamani hapa ni wewe uliyetoa taarifa kwamba Naomi ameuawa na Hamisi Said Luwongo, ni sahihi?

Shahidi: Siyo sahihi.

Wakili: Kwa mujibu wa ushahidi aliyewaonyesha askari mahali masalia ya Naomi yalikozikwa ni Hamisi Said Luwongo, ni sahihi?

Shahidi: Hayakuwa ya Naomi.

Wakili: Na kwa ushahidi huo ni Hamisi Said Luwongo aliyewapeleka askari sehemu alikouliwa Naomi?

Shahidi: Kwa mujibu wa ushahidi ni sahihi.

Wakili: Kwa mujibu wa ushahidi wote ilimchukua miezi miwili Hamisi Said Luwongo kusema ukweli kuwa ndiye aliyemuua Naomi, ni sawa?

Shahidi: Kwa mujibu wa ushahidi wote mimi pia nimetoa ushahidi kwa hiyo siyo kweli.

Wakili: (Anamkabidhi mshtakiwa nakala ya maelezo yake aliyoyatoa polisi ambayo yamepokewa na mahakama na kuwa kielelezo cha upande wa mashtaka, mshtakiwa anayasoma kisha anamuuliza: Huo mwili wa huyo mtu ambaye huko nyuma tulisoma (kwenye maelezo hayo), kuwa alikuwa ametapakaa damu ulifanywa vipi?

Shahidi: Ulichomwa moto, kwa mujibu wa hii stori.

Wakili: Hayo mabaki ya huo mwili uliochomwa yalipelekwa wapi?

Shahidi: Kwa mujibu wa hii yalipelekwa kwenye gari yakapelekwa shambani.

Wakili: Hamisi, tuko hapa kwa ajili ya kutenda haki, kuna shida yoyote Mheshimiwa (jaji) kupokea barua hii (aliyomwandikia DPP ya kutaka kukiri kosa) aisome ili wakati akiandika hukumu aweze kuelewa kulichotokea? Kwa hiyo hutaki Mheshimiwa aisome?

Shahidi: Wewe zungumza vitu vya msingi, sema mke wangu yuko wapi.

Wakili: Ulijuaje kuwa sasa hapa Naomi amefariki ukaenda kumchoma?

Shahidi: Wewe mbona unaniuliza maswali ambayo siyaelewi?

Wakili: Nakuuliza baada ya kumpiga akaanguka ulijuaje kwamba sasa Naomi amefariki sasa ukamchome?

Shahidi: Kifupi mke wangu hajafariki, labda wewe ndio uithibitishie mahakama.

Wakili: Unahitaji uthibitisho gani kuwa Naomi amekufa?

Shahidi: Uthibitisho wa kisayansi, mkemia ndio aje aseme athibitishe kuwa udongo ule ulioletwa hapa ni wa Naomi lakini mkemia hajasema hivyo.

Wakili: Ulivyomchoma hivyo mpaka akawa majivu ulitegemea uthibitisho gani?

Shahidi: Mimi sijamchoma.

Wakili: Ulikuwa unatumia gari gani?

Shahidi: Nilikuwa na magari mengi.

Wakili: Hii Subaru uliimiliki kuanzia lini?

Shahidi: Mimi nimeanza kumiliki gari wewe hata shule hujaanza.

Jaji: Umesemaje hapo?

Shahidi: Mheshimiwa mimi nimeanza kumiliki gari huyu hata shule hajaanza.

Jaji: Amekuuliza hii Subaru.

Shahidi: Siikumbuki mheshimiwa.

Wakili: Umeushutumu ushahidi wa Jamhuri kwamba umeshindwa kuthibitisha kuwa mke wako amekufa, sasa wewe una uthibitisho gani kuwa hajafariki wakati tangu alipokushika sehemu za siri hajawahi kuonekana?

Shahidi: Ndio maana nilifungua kesi kuwa mke wangu amepotea.

Wakili: Ulisema ulinunua shamba na kaburi, ni sahihi?

Shahidi: Nilinunua shamba likiwemo kaburi tukakubaliana walihamishe.

Wakili: Kama walishalihamisha hiyo mifupa ilitoka wapi?

Shahidi: Waliohamisha hawakutekeleza wajibu wao vizuri.

Wakili: Huyo marehemu alikuwa anakuhusu?

Shahidi: Alikuwa hanihusu.

Wakili: Kwa nini hukuwaeleza wao wakaja kuichukua?

Shahidi: Sikuona umuhimu.

Wakili: Wewe ulileta uthibitisho gani mahakamani kuwa ulifukua mabaki ya mifupa hiyo?

Shahidi: Sikuleta mheshimiwa.

Wakili: Kwa hiyo kwa mujibu wa ushahidi wako wewe ndio mtu wa mwisho kuwa na Naomi kabla hajafariki, ni sahihi?

Shahidi: Kwa mujibu wangu mimi mara ya mwisho nilimuona Mei 15 sijui kwa watu wengine huko.


Wakili wa Serikali Eric Kamala aliendelea kumhoji shahidi:

Wakili: Shahidi, katika maelezo yako hujapinga kuwa ulipelekwa kwa Hakimu wa Mwanzo kuandika maelezo, wala hujaeleza kama kwa hakimu alikulazimisha kutoa maelezo.

Shahidi: Niliekezwa kuwa nieleze kilekile nilichokieleza na kwamba, vinginevyo mateso yangeendelea.

Wakili: Nakuuliza wakati ukiwa kwa hakimu yeye mwenyewe hajasema kuwa alikulazimisha.

Shahidi: Kweli.

Wakili: Wala hujasema kuwa maelezo yale ni ya uwongo

Shahidi: Nilisema.

Wakili: Ulisema ulinunua shamba huko Mwongozo na wakati mafundi wakichimba msingi wakakuta mifupa, ni sahihi?

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili: Utakubaliana na mimi kuwa hao mafundi hujawaleta hapa mahakamani kutoa ushahidi?

Shahidi: Ndiyo.

Wakili: Unakubaliana na mimi kuwa ile mifupa uliyochoma ndio uliyopandia migomba?

Shahidi: Hapana, kulikuwa na matakataka mengi

Wakili: Nani aliichoma ile mifupa?

Shahidi: Ni kijana niliyempa kazi.

Wakili: Utakubaliana na mimi kuwa huyo kijana hujamleta hapa mahakamani kutoa ushahidi?

Shahidi: Ndiyo


Akiongozwa na wakili wake kufafanua majibu aliyoyatoa kwa baadhi maswali ya waendesha mashtaka alisisitiza kuwa aliwaeleza polisi kuwa hayo maneno aliyokuwa amewaeleza (ya kumuua mkewe Naomi) ni ya kweli ili waweze kuamini lakini hayakuwa kweli.

Kuhusu jibu lake kuwa hakuona mabaki ya mwili wa Naomi yakitolewa alieleza alijibu hakuyaona yanatolewa mahakamani kwa sababu swali lilikuwa linahusu mabaki kama meno na mifupa lakini yaliyotolewa mahakamani na upande wa mashtaka ni udongo.

Wakili Mushi aliieleza mahakama kuwa upande wa utetezi walikuwa na shahidi huyo pekee ambaye ni mshtakiwa na kuomba kufunga ushahidi.

Jaji Mwanga ametoa amri ya kufunga ushahi huo wa utetezi.

Kiongozi wa jopo la waendesha mashtaka, Yasinta aliiomba mahakama chini ya kifungu cha 165(1) cha Sheria Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA), imuite daktari wa Taasisi ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, aliyemfanyia uchunguzi wa akili.

“Kutokana na ripoti iliyoko kumbukumbu za mahakama, kutoka Hospitali ya Mirembe ya mshtakiwa na kutokana na ambavyo mshtakiwa amejitetea tunaomba mahakama isaidie kumpata daktari aliyeiandaa Profesa Saqick Mandari kwa tarehe ambayo mahakama itapanga kwa ajili ya maswali ya dodoso,” aliomba Yasinta.

Aliomba kumuita daktari huyo kuhoji maswali ya dodoso kuhusu ripoti yake ili kuisaidia Mahakama kufikia uamuzi kulinga na hali ya ushahidi alioutoa.

Wakili wa utetezi Mushi alisema hana pingamizi kwa ombi hilo.

“Kwa sababu huyu daktari kwa amri ya Mahakama akichunguza afya ya akili ya mshtakiwa na taarifa ikaja kuwa mshtakiwa alikuwa na changamoto ya akili ni vema daktari huyu akaja ili upande wa mashtaka upate nafasi ya kumhoji. Kwa hiyo tutaendelea Jumatatu Novemba 25, 2024,” alisema Jaji Mwanga.