Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ahoua  katikati ya mtihani mzito wa Aziz Ki, Pacome

Muktasari:

  • Aziz Ki raia wa Burkina Faso, alitua ndani ya kikosi cha Yanga Julai 15, 2022 akitokea ASEC Mimosas ambapo tayari amecheza hapa nchini kwa misimu miwili huku mmoja akiwa Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara akifunga mabao 21 msimu uliopita 2023-2024.

Kuna kitu kikubwa kinasubiriwa na mashabiki wa soka hapa nchini msimu ujao wa 2024-2025 kuona nini kitaenda kutokea kutokana na usajili unaofanyika hivi sasa kwa timu mbalimbali hasa zile zitakazoshiriki Ligi Kuu Bara.

Kuna vurugu kubwa inafanyika sokoni kwa sasa huku wakongwe Simba na Yanga wakiteka hisia za wengi kutokana na wingi wa mashabiki walionao.

Yanga inapambana kuimarisha kikosi chake ili kuendelea kuonyesha ubabe wao katika Ligi Kuu Bara, Simba yenyewe inajenga kikosi cha kurudisha utawala wao uliopotea kwa misimu mitatu mfululizo kuanzia 2021-2022 hadi 2023-2024. Kumbuka kabla ya hapo Simba ilitawala misimu minne mfululizo 2017-2018 hadi 2020-2021.

Katika kuimarisha vikosi vyao, kila mmoja amekuwa akisajili wachezaji na kuwaongezea mikataba wale waliomaliza na kuona bado wana uhitaji nao.

Katika sajili hizo, tumeshuhudia Simba ikimshusha kiungo mshambuliaji Jean Charles Ahoua kutoka Stella Club d'Adjame ya nchini Ivory Coast ambayo msimu uliomalizika 2023-2024 imemaliza nafasi ya sita katika msimamo.

Nyota huyo anakuja nchini akiwa na mtihani wa kudhihirisha uwezo wake baada ya kufanya balaa nchini Ivory Coast.

Imekuwa ikielezwa kwamba ujio wa kiungo huyo Simba imefanya ikiwa ni kama kuziba pengo la Clatous Chama aliyehamia Yanga, lakini wenyewe wanasema haipo hivyo bali usajili wake ni sehemu ya kuimarisha kikosi na siyo kusaka mbadala wa mtu.

Inafahamika wazi kwamba, Chama ambaye alijiunga na Simba msimu wa 2018-2019 akitokea Lusaka Dynamos ya Zambia, amefanya makubwa sana kikosini hapo akicheza kwa misimu mitano na nusu.

Awali Chama alikuwa nyota wa Simba kuanzia Julai Mosi 2018 hadi Agosti 16, 2021 alipohamia RS Berkane kabla ya kurejea Januari 14, 2022, alikuwa sehemu ya kikosi cha timu hiyo kilichocheza robo fainali tano za michuano ya klabu Afrika ambapo Kombe la Shirikisho (1) na Ligi ya Mabingwa Afrika (4).

Achana na hilo la kutajwa kuwa mrithi wa Chama, kilichopo kwa Ahoua ni kupita njia walizopita watangulizi wake, Stephane Aziz Ki na Pacome Zouzoua ambao wapo Yanga.

Hiyo inatokana na kwamba nyota hao wote pindi walipokuwa wanatua katika ardhi ya Tanzania kucheza Ligi Kuu Bara walitoka Ivory Coast wakiwa na Tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu (MVP).

Aziz Ki raia wa Burkina Faso, alitua ndani ya kikosi cha Yanga Julai 15, 2022 akitokea ASEC Mimosas ambapo tayari amecheza hapa nchini kwa misimu miwili huku mmoja akiwa Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara akifunga mabao 21 msimu uliopita 2023-2024.

Msimu mmoja mbele baada ya Aziz Ki, Yanga ikamshusha Pacome Zouzoua kutoka ASEC Mimosas. Pacome ambaye ni raia wa Ivory Coast naye wakati anatua Yanga alikuwa na Tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Ivory Coast msimu wa 2022-2023. Tayari ana msimu mmoja Ligi Kuu Bara.

Ndani ya msimu wa 2022-2023, Pacome aliyewahi kucheza timu ya vijana ya Sparta Prague ya Jamhuri ya Czech, alifunga mabao 7 na kutoa asisti 4 ambapo uchangiaji wake huo wa mabao 11 ukafanikisha kubeba Tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu Ivory Coast.

Ndani ya msimu wa 2022/23, Pacome aliyeanza maisha yake ya soka kwenye timu ya vijana ya Sparta Prague ya Jamuhuri ya Czech, amefunga mabao 7 na kutoa Asisti za mabao 4. Mbali na tuzo hiyo, pia Pacome alikuwa Mchezaji Bora wa Klabu ya Asec Mimosas akimzidi Aubin Kramo aliyetua Simba.

Hakuna aliyebaki na maswali mengi kichwani baada ya kushuhudia uwezo mkubwa wa Pacome aliouonyesha msimu uliopita 2023-2024 kwenye ardhi ya Tanzania akiwa na jezi ya Yanga kwani ubora wake ukamfanya Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Ivory Coast, Emerse Faé, amjumuishe kikosini katika mchezo wa kirafiki waliocheza Machi 23 mwaka huu dhidi ya Benin. Kuitwa katika kikosi hicho ilikuwa ni mara ya kwanza kwake.

Pacome msimu uliopita alichangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya Yanga katika kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara akifunga mabao saba na Kombe la Shirikisho (FA), huku wakicheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza akifunga mabao matatu nyuma ya mfungaji bora Sankara William Karamoko aliyefunga manne.

Aziz Ki katika misimu yake miwili ndani ya Ligi Kuu Bara, amefunga jumla ya mabao 30 baada ya 2022-2023 kufunga 9 na 21 alifunga 2023-2024 akiibuka mfungaji bora.


Jean Charles Ahoua

Akiwa na miaka 22, nyota huyu amejiunga na Simba akitokea Stella Club d'Adjame ya Ivory Coast, nafasi yake uwanjani ni kiungo mshambuliaji. Takwimu zake msimu uliopita katika Ligi Kuu ya Ivory Coast zinaonyesha kwamba alichangia jumla ya mabao 21 kutokana na kufunga 12 na kutoa asisti 9.

Klabu ya Simba imefanikiwa kunasa saini ya kiungo huyo raia wa Ivory Coast malengo yakiwa ni kuhakikisha wanarejesha heshima ya klabu hiyo kutokana na kutofanya vizuri kwa misimu mitatu iliyomalizika, Huku kiungo Ahoua akionekana ni moja ya wachezaji ambao wataweza kurejesha makali ya Mnyama kuelekea msimu ujao.

Ahoua ambaye anafahamika kama kiungo wa ushambuliaji mwenye uwezo mkubwa wa kutengeneza mashambulizi, kuzuia pale ambapo timu yake inaposhambuliwa lakini bila kusahau uwezo wake mkubwa wa kufunga ana kazi kubwa ya kufanya kudhihirisha uwezo wake.

Utofauti wa Ligi Kuu ya Ivory Coast na Tanzania unaweza kuwa changamoto kwake, lakini kama amejipanga vizuri anaweza kutoboa kama ilivyokuwa kwa Aziz Ki na Pacome.


WAPO WALIOFELI

Wakati Aziz Ki anatua Yanga, Azam ilimshusha Muivory Coast, Tape Edinho ambaye wakati anakuja alikuwa ameshinda Tuzo ya Kiungo Bora wa Ligi Kuu Ivory Coast msimu wa 2021-2022 wakati akiitumikia ES Bafing FC.

Edinho hakuwa na wakati mzuri ndani ya Azam kwani amecheza kwa miezi sita pekee, akatolewa kwa mkopo kwenda Stella Club d'Adjamé baada ya kuonekana amefeli kufikia matarajio yao.

Hivyo kufeli kwa Edinho ambaye alikuja Tanzania akiwa ametoka kushinda Tuzo ya Kiungo Bora wa Ligi Kuu ya Ivory Coast huku Aziz Ki na Pacome wakifaulu inamuweka Ahoua katika pande mbili, kufanikiwa au kufeli moja kati ya hayo yanaweza kutokea.