Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Twiga Stars imeonyesha wanawake Tanzania wanaweza

Muktasari:

Twiga Stars inaingia katika mchezo huo ikiongoza kwa mabao 4-2, ushindi ilioupata kwenye mchezo wa kwanza uliofanyika Lusaka, Zambia.

Aprili 10, Timu ya Taifa ya Soka ya Wanawake (Twiga Stars) itaikabili Zambia kwenye mchezo wa marudiano wa kusaka tiketi ya kushiriki Michezo ya Afrika iliyopangwa kufanyika Kongo-Brazaville Septemba.

Twiga Stars inaingia katika mchezo huo ikiongoza kwa mabao 4-2, ushindi ilioupata kwenye mchezo wa kwanza uliofanyika Lusaka, Zambia.

Tunaipongeza timu hiyo kwa ushindi huo mnono tena wa ugenini ambao unaipa fursa nzuri ya kukata tiketi ya kushiriki katika michuano hiyo.

Hata hivyo, licha ya ushindi huo, ushiriki wa kina dada hawa katika michuano hiyo mikubwa ya kimataifa bado ni kitendawili.

Kitendawili hili kinatokana na migongano ambayo tumeiripoti kwenye gazeti hili Jumamosi iliyopita ikihusisha wizara inayosimamia michezo pamoja na vyama washirika wake, Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Hatupendi kuingia kwenye undani wa suala hilo, lakini tunaingiwa na wasiwasi kutokana na kauli ya Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi kwamba ofisi yake ambayo ndiyo inayoratibu Michezo ya Afrika haina habari za ushiriki wa timu hiyo. Tunaamini msuguano huo ambao gazeti hili liliiuripoti utakuwa umepatiwa suluhisho ifikapo au kabla ya Aprili 10 wakati wa mchezo huo wa marudiano.

Tunashauri suala hilo litafutiwe suluhu mapema ili lisiwaathiri vijana wetu hao.

Tunaamini kwamba kushiriki kwake kungesaidia kujenga msingi wa mchezo huo. Tunasema, timu hiyo haina msingi kwa sababu soka ya wanawake katika nchi yetu licha ya kutambuliwa na TFF kiasi cha kuwa na chama chake, lakini ni kama haina mwenyewe.

Tunasema hivyo, kwani hakuna klabu za kutosha kuwezesha kuwapo kwa ligi za aina yoyote ambazo zingetumika kusaka au kupata wachezaji wanaofaa kuichezea Twiga Stars.

Wachezaji hao wa kuokoteza kila yanapotokea mashindano na ukosefu wa ligi ya soka ya wanawake, ndicho kilio kinachotufanya tufikiri kwamba mafanikio yake katika hatua kama hii ingekuwa chache ya kuuendeleza mchezo huo.

Ni katika muktadha huo, tunakitaka chama hiki kinachosimamia mchezo huo kwa wanawake na TFF kwa jumla, kusimama kidete kuhakikisha timu hii inashiriki katika michuano hiyo.

Baada ya hapo, tunapenda kukikumbusha chombo hicho kinachosimamia soka kwamba, umefika wakati wa kujenga msingi wa kuendelea mchezo huo kwa kina mama hivyo kianze maandalizi tangu ngazi za chini waliko wasichana, shule za msingi, sekondari hadi vyuo.

Tunaamini kuwa tunao wasichana wenye vipaji vikubwa vya kucheza soka, wanachohitaji ni kuandaliwa kuwa wanamichezo. Waandaliwe kucheza soka kwani wanaweza pia kuondokana na umaskini kwa kucheza soka ya kulipwa nje ya nchi ma kujiingizia kipato.

Tunazishauri klabu zetu za soka zikiwamo Simba, Yanga, Azam na nyinginezo, kufikiria pia kuwekeza kwenye maendeleo ya soka ya wanawake.

Tunaamini, klabu hizo zinaweza kuiga au kujifunza kutoka klabu kama za England, Ufaransa, Ujerumani na kwingineko duniani ambazo zina klabu za soka za wanawake ambazo zinafanya vyema kwa kushiriki ligi mbalimbali ndani ya nchi hizo na kimataifa.

Tunawashauri viongozi wa Chama cha Soka cha Wanawake Tanzania (TWFA) waongoze harakati na mipango endelevu ya kukuza soka nchini, wasitegemee kubebwa na TFF, wanaposhiriki vikao au mkutano, wazinduke na kujitambua. Lakini kwa kuanzia, wahakikishe Twiga Stars inakwenda Brazaville, kwani wameonyesha kuwa wanaweza.