Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wananchi tujihadhari na kipindupindu, kinaua

Desemba 10, 2024, baadhi ya vyombo vya habari nchini viliripoti hofu ya kuibuka ugonjwa wa kipindupindu mikoa ya Mbeya na Dodoma na mamlaka zikiwataka wananchi kuchukua tahadhari kwa kufuata kanuni za usafi wa mazingira na chakula.

Wataalamu wa afya wanaeleza chanzo cha ugonjwa wa kipindupindu ni uchafu wa mazingira na kusababisha bakteria wanaojulikana kitaalamu kama (vibriocholerae) kuwa na uwezekano wa asilimia 20 hadi 70 kusababisha kifo endapo itakosekana huduma inayostahili, hasa kwa walioathirika zaidi.

Uchafu wa vyanzo vya maji, utupaji ovyo wa taka, pia kujisaidia ovyo na miundombinu duni ya maji safi na maji taka yanatajwa kuchangia magonjwa ya milipuko, ikiwemo wa kuhara na kipindupindu.

Mara ya mwisho kuripotiwa kwa ugonjwa wa kipindupindu kwa mujibu wa vyanzo vya habari ilikuwa wilayani Chato, Mkoa wa Geita ambako watu wanane walidaiwa kubainika na ugonjwa huo, mmoja kati yao kutajwa kufariki na Serikali ilichukua hatua za haraka kuweka kambi maalumu ya wagonjwa.

Taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) Machi 2024, imesema idadi ya wagonjwa wa kipindupindu imeongezeka kwa miaka ya hivi karibuni na kuua watu 5,900 na kuripotiwa wagonjwa 825,000 kwa nchi 30 na kuuweka ugonjwa huo daraja la tatu hatari.

Idadi hiyo ya vifo na wagonjwa kwa nchi 30 na Tanzania ikiwemo, jamii itambue kuwa ugonjwa huo ni hatari na kuacha kupuuza maelekezo ya mara kwa mara ya wataalamu wa afya juu ya kudumisha usafi wa mazingira na chakula.

Taarifa ya kuibuka kwa hofu ya kipindupindu iwazindue maofisa afya kote nchini kutoa elimu kwa jamii na watoa huduma ya chakula, mama na baba lishe kudumisha usafi maeneo yao na vyombo vyao pamoja na kunawa mikono kabla ya kuandaa chakula.

Kuwepo hofu ya ugonjwa huo wa kipindupindu kwa mikoa hiyo, kila mmoja kutakiwa kuchukua tahadhari binafsi hasa kipindi hiki cha msimu wa matunda kwa baadhi ya maeneo kuacha kula kabla ya kuosha na kunawa mikono kwa maelezo kwamba wadudu hupendelea sehemu iliyoiva au kuoza.

Zipo taarifa zilizoeleza Jiji la Mbeya kusajili watu wenye maambukizi ya ugonjwa huo na kutengewa eneo maalumu, hivyo ni vyema hatua za tahadhari zichukuliwe ili kuzuia kusambaa maeneo mengine.

Kipindi hiki cha mvua kwa baadhi ya maeneo, wakurugenzi wa halmashauri za majiji na miji watoe mwongozo kwa maofisa afya kata na wilaya wawe wasimamizi wakuu wa usafi mazingira kwa kushirikiana na viongozi wa Serikali za mitaa.

Wataalamu wa afya wanautaja ugonjwa wa kipindupindi ambao ni wa kuambukiza, chanzo chake ni mazingira machafu, hivyo kwa ushirikiano huo uwasukume kuhakikisha kipindi hiki cha mvua kwa baadhi ya maeneo, masoko yanakuwa katika hali ya usafi muda wote na taka katika madampo kusombwa kila siku.

Septemba 10, 2024, Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga iliripotiwa mtu mmoja kufariki na wengine 16 kulazwa hospitali baada ya kile kilichoelezwa kuwa ni maambukizi ya ugonjwa wa kipindupindu.

Serikali wilayani humo iliweza kuudhibiti na kuutokomeza ugonjwa huo, lakini jamii inatakiwa kutobweteka kwa kuamini umetokomea na badala yake idumishe kanuni za afya na usafi wa mazingira kuwa ndio utamaduni na uwepo mkazo wa matumizi bora ya choo kwa wote mjini na vijijini.

Ugonjwa wa kipindupindu unatajwa kuwa hatari, unaoweza kusababisha kifo, ndiyo maana Shirika la Afya Duniani (WHO) likauweka kuwa wa daraja la tatu, hivyo ni vyema jamii kujengewa uelewa wa kutambua dalili zake na hatua za kuchukua ili kutopata madhara.

Licha ya kuwa hadi sasa hakuna taarifa ya vifo kwa ugonjwa huo, lakini ziwepo hatua za kuielimisha jamii kujua ugonjwa upo, unaweza kuzuka muda wowote ikiwa tu mazingira yatakuwa katika hali hatarishi.

Kama nilivyosema kipindi hiki cha mvua kwa baadhi ya maeneo ni vyema Serikali kupitia mamlaka za halmashauri za miji na majiji kutoa elimu kupitia matangazo (mobile cinema) ili kila mmoja ajue madhara ya ugonjwa huo na dalili zake pamoja na jinsi ya kujikinga.

Kwa mkakati huo wa WHO, dhamira hiyo inaweza kufikiwa endapo tu viongozi wa mataifa husika watakuwa na sauti moja ya kuona ni janga kwa kuchukua hatua zaidi, ikiwemo elimu kwa jamii.

0655 902929