Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanafunzi thibitisheni vyuo mapema

Udahili wa wanafunzi wa Shahada ya Kwanza kwa mwaka wa masomo 2025/2026 umeingia katika hatua muhimu baada ya awamu ya kwanza kufungwa rasmi.

Jumla ya waombaji 116,596 wamechaguliwa kujiunga na taasisi mbalimbali za elimu ya juu, kukiwa na ongezeko la wanaodahiliwa mwaka hadi mwingine.

Hatua ya Serikali kuongeza nafasi za masomo hadi 205,652 kutoka nafasi 198,986 mwaka uliopita, pamoja na ongezeko la programu hadi 894 kutoka 856 ni ushahidi wa wazi wa juhudi za kupanua na kuboresha elimu ya juu nchini.

Ni hatua ya kupongezwa kwa jitihada za Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) pamoja na Serikali katika kuhakikisha fursa za elimu ya juu zinaongezeka na kuwafikia Watanzania wengi zaidi.

Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo, bado kuna changamoto zinazohitaji kushughulikiwa kwa umakini na kwa haraka.

Moja ya changamoto hizo ni ile ya waombaji kuchaguliwa katika chuo zaidi ya kimoja au programu zaidi ya moja, hali inayowalazimu kujithibitisha katika chuo na programu mojawapo kati ya walizochaguliwa ili kutoa fursa kwa wengine.

Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa, jumla ya waombaji 67,576 wamechaguliwa katika chuo zaidi ya kimoja, hivyo wametakiwa kujithibitisha kuanzia Septemba 2 hadi 21, mwaka huu.

Hatua hii ya kujithibitisha ni ya lazima na ya msingi kwa ustawi wa mfumo mzima wa udahili. Kutofanya hivyo kunasababisha urundikaji wa nafasi ambazo zingetolewa kwa waombaji wengine, hasa wale ambao hawakupata nafasi katika awamu ya kwanza.

Kwa maana hiyo, uamuzi wa TCU kuwataka wanafunzi kujithibitisha mapema haupaswi kuchukuliwa kama utaratibu wa kawaida tu, bali kama wajibu wa kimaadili na kijamii kwa kila mwombaji.

Takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya nafasi 89,000 bado ziko wazi kwa ajili ya awamu ya pili ya udahili, lakini idadi hiyo inaweza kuongezeka ikiwa waombaji waliochaguliwa kwenye chuo zaidi ya kimoja watajithibitisha kwa haraka na kwa uwazi.

Hili linapaswa kuwa fundisho kwa kila kijana anayetarajia kujiunga na elimu ya juu kuwa udahili si tu mchakato wa kupata chuo, bali ni mchakato unaohitaji uwajibikaji binafsi kwa ajili ya kuwaruhusu na wengine kupata fursa.

Hata hivyo, licha ya umuhimu huo, uhalisia ni kuwa kuchaguliwa kwa idadi kubwa ya wanafunzi kwenye vyuo zaidi ya kimoja ni ishara kuwa mfumo wa sasa bado unahitaji maboresho.

Hii inamaanisha kuwa pamoja na kuwawajibisha wanafunzi kujithibitisha, pia kuna haja ya kuangalia upya namna mfumo wa udahili unavyofanya kazi, ili kuhakikisha kuwa nafasi zinagawiwa kwa haki na kwa ufanisi zaidi, bila kuathiri muda au haki ya waombaji wengine.

Ni muhimu pia kwa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu kuchukua hatua madhubuti katika kutangaza programu ambazo bado zina nafasi. Hili litasaidia waombaji wapya pamoja na wale ambao hawakupata nafasi katika awamu ya kwanza kufanya uamuzi sahihi na ya haraka.

Kupitia uhamasishaji wa kutosha, vyuo vinaweza kusaidia kupunguza msongamano wa maombi katika programu chache maarufu, hivyo kusambaza wanafunzi katika maeneo mengine yenye nafasi, bila kupoteza ubora wa elimu.