Prime
UCHAMBUZI WA MJEMA: Tungesikiliza ushauri huu wa majaji, haki ingeonekana inatendeka
Kuna maeneo mawili muhimu sana ambayo majaji wetu walitoa ushauri muhimu sana, lakini sijui ni kukosa utashi wa kisiasa au woga tu wa mabadiliko, hatukuwahi kuufanyia kazi.
Maeneo hayo mawili, moja ni kutohojiwa kwa matokeo ya urais baada ya Tume kumtangaza mshindi ambao mwaka 1995, jopo la majaji lilishauri kifungu hicho cha sheria (kwa wakati ule) kifanyiwe marekebisho ili matokeo yahojiwe kortini.
Ushauri wa pili ni uliotolewa Julai 2019 na aliyekuwa Jaji Mkuu wa Tanzania, sasa amestaafu, Profesa Ibrahim Hamis Juma, aliyependekeza makosa yote ya Jinai hapa Tanzania kuwa na dhamana kama ilivyo kwa majirani zetu, Jamhuri ya Kenya.
Nitaanza na hili la dhamana, kwamba kwa sheria zetu zinazuia dhamana kwa makosa kama mauaji, uhaini, utakatishaji fedha na usafirishaji dawa za kulevya na kuondoa dhana kuwa mtu anakuwa hana hatia hadi atiwe hatiani na mahakama.
Ukisoma ibara ya 13(6)(b) ya Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 inasema ni marufuku kwa mtu aliyeshtakiwa kwa kosa la jinai kutendewa kama mtu mwenye kosa hilo mpaka itakapothibitika kuwa anayo hatia ya kutenda kosa hilo.
Ukienda mbele na kusoma ile ibara ndogo ya (e) inasema ni marufuku kwa mtu kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazomtweza au kumdhalilisha. Huko vituo vya Polisi hali ikoje? Nitumie maoni yako.
Pamoja na maudhui mazuri hivyo, mtu anakamatwa hapewi dhamana polisi, anakaa mahabusu zaidi ya mwezi, anapelekwa mahakamani anakosa dhamana kwa mujibu wa sheria, anakaa mahabusu zaidi ya mwaka anaonekana hana hatia.
Wapo wanaosota zaidi ya miaka mitano baadaye Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP) anapeleka maelekezo kortini (nolle prosequi) kuwa hana nia ya kuendelea kumshitaki mtu huyo, wakati huo tumempoteza muda mrefu mahabusu.
Unamweka mtu mahabusu, tena wakati mwingine kwa makosa ya kumbambikia mtu iwe kisiasa au kijamii kwa lengo la kumkomoa, biashara zake zinakufa, hadhi yake katika jamii inashuka na ni kinyume kabisa na ile ibara ya 13 ya Katiba.
Ndio maana nimetangulia kusema kama ushauri ule wa Profesa Ibrahim Juma kuwa makosa yote yawe na dhamana au masharti ya dhamana yalegezwe japo yeye alisema itapunguza msongamano wa mahabusu, hii kwangu nadhani hata tungeondokana na watu kuwekwa korokoroni bila kupewa dhamana.
Wenzetu Kenya makosa yote yana dhamana na mtuhumiwa anafikishwa kortini ndani ya saa 24 tangu akamatwe na endapo Polisi wanataka kuendelea kumshikilia kwa sababu za kiupelelezi, wanawasilisha ombi mahakamani juu ya hilo.
Kwao hakuna kumshikilia mtu mahabusu kinyume cha sheria kama ilivyo Tanzania ambapo wapo watu wanakaa mahabusu za polisi hadi wanasahaulika na jamii. Wenzetu mtu akifikishwa tu kortini anapewa dhamana ya fedha taslimu.
Kama hana fedha taslimu (cash bond) anaambiwa alete cheti cha hisa anazomiliki au kuleta mtu atakayeleta hati ya mali yenye thamani kama nyumba au gari na anaachiliwa, huko ambapo natamani Tanzania ielekee huko. Hofu ya nini?
Yaani Katiba yetu inatoa hakikisho la haki kwamba mtu atachukuliwa hana hatia hadi atakapotiwa hatiani na mahakama, lakini tunatunga sheria ambazo tunawatendea washukiwa au watuhumiwa kana kwamba tayari ni wahalifu.
Eneo lingine ni ushauri uliotolewa Januari 31,1995 na jopo la majaji watatu wa mahakama ya rufani wakiongozwa na Jaji mkuu wa wakati huo, Francis Nyalali akiwa na majaji wenzake ambao ni Jaji Robert na Jaji Lameck Mfalila.
Siku hiyo walisoma hukumu ya rufaa iliyokatwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na wenzake wawili, dhidi ya Dk Aman Walid Kaborou kuhusiana na uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Kigoma mjini ambapo Azim Premji alishinda.
Dk Kaborou aliyegombea ubunge kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) alipinga ushindi wa Premji wa CCM na mahakama ikatengua ushindi huo, lakini AG na wenzake wakakimbilia mahakama ya rufani.
Huko nako walikwaa kisiki kwani mahakama ilithibitisha madai ya Kaborou.
Hoja yangu hapa wala si huo ushindi wa Dk Kaborou, la hasha ni namna Jaji mkuu wakati huo Nyalali na wenzake walivyoshangazwa na Sheria ya Uchaguzi ya 1985 kama ilivyofanyiwa marejeo 1992, kutoruhusu matokeo ya urais kuhojiwa kortini.
Nikinukuu hukumu, majaji hao walisema na hapa nitanukuu “Jambo la mwisho tunalohitaji kueleza, kwa kuzingatia uchaguzi ujao wa Rais na ubunge (Uchaguzi Mkuu 1995) ni pengo katika sheria ya uchaguzi kuhusu uchaguzi wa Rais”.
Wakasema kifungu 108 cha sheria hiyo kilihusu tu kwamba matokeo ya ubunge yanaweza kupingwa kortini, lakini hapakuwepo kifungu kinachoruhusu matokeo ya urais kuweza kupingwa kortini wakisema hawaelewi ni kwa nini.
Majaji hao wakashangaa kwa nini pengo hilo halikuzibwa wakati kunafanyika marekebisho ya sheria mwaka 1992 ili kuruhusu matokeo hayo kuhojiwa.
Nikiwanukuu majaji hao, walisema, “Pengo hilo linatatanisha tangu uchaguzi wa rais wa vyama vingi. Pengo kama hilo ni mwaliko wa machafuko ya kisiasa”
Kwa busara zao na kwa lugha laini, majaji hao wakasema. “Tunatumai marekebisho yanayofaa ya sheria (ya uchaguzi ya mwaka 1992) husika yatafanywa kabla ya uchaguzi ujao wa vyama vingi,”, unajua nini kilitokea?
Badala ya Serikali iliyokuwa ikiongozwa na CCM na yenye asilimia 99.9 ya wabunge, badala ya kurekebisha sheria hiyo, wao wakaenda kutunga Ibara za Katiba ambayo zinazuia kabisa matokeo ya urais kupingwa mahakamani.
Bunge likatunga Ibara ya 41 (7) inayosema iwapo mgombea ametangazwa na Tume kwamba amechaguliwa kuwa Rais kwa mujibu wa ibara hii, basi hakuna mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza kuchaguliwa kwake.
Pia Ibara ya 74 (12) ikawa na ibara ndogo inayosema hakuna mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza jambo lolote lililotendwa na Tume ya Uchaguzi katika kutekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba hiyo.
Miaka 31 leo, ushauri huo wa Jaji Mkuu Nyalali na wenzake haukuwahi kufanyiwa kazi na nina uhakika kama ungefanyiwa kazi pengine hata rabsha zile za Oktoba 29,2025 na siku zilizofuata zisingetokea kama tungefanya marekebisho hayo.
Ndio, ni kwa sababu moja ya madai makubwa ya wadau wa demokrasia ni kuwepo kwa Katiba Mpya itakayoruhusu kuhojiwa kwa matokeo hayo ya urais na majaji walitahadharisha miaka 31 nyuma kuwa hilo litakaribisha machafuko.
Leo hii Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) katika hukumu yake iliyoitoa Machi 6,2026 Jijini Arusha imerejea lile lile kuhusu Ibara inayozuia matokeo ya Rais kuhojiwa, ambapo Jaji Nyalali na wenzake waliliona.
Yaliyotokea Oktoba 29,2025 ni kilele cha mlundikano wa malalamiko ikiwamo madai ya Katiba mpya, Tume Huru ya Uchaguzi, Utekaji na kupotea kwa watu pamoja na mauaji na halikadhalika hisia za upinzani kukandamizwa.
Ukiacha hayo kuna hisia za ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaonyooshewa vyombo vyetu vya Dola ikiwamo kubambikia watu kesi lakini tungezingatia ushauri ule wa makosa yote kuwa na dhamana, pengine ingesaidia.
Matukio yale ya Oktoba 29 na siku zilizofuata ni dalili (wakeup call) kwamba tukicheza na haki za watu hata hii amani tunayoiimba haiwezi kuwapo.