Prime
UCHAMBUZI WA MJEMA: Mnaonaje tukipiga picha matukio yote ya ukamataji holela?
Nimekuwa nikifuatilia simulizi za watu waliotekwa au kupotezwa na katika baadhi ya matukio hayo, wapo Watanzania wenzetu waliyashuhudia au kuyahisi, lakini hawakuchukua hatua yoyote hata tu kupiga picha au kurekodi video.
Ninatamani sana tuwaige jirani zetu wa Kenya ambapo kila tukio wanaloliona la mtu kukamatwa, iwe na askari wenye sare au wasio na sare, akili ya kwanza inayowajia ni kuchukua simu janja na kurekodi matukio ya aina hiyo haraka.
Hii kwa kiasi kikubwa imesaidia na kuwezesha vyombo kama Independent Policing Oversight Authority (IPOA), ambacho ni huru kinachochunguza mauaji, ukiukwaji haki za binadamu na matendo mabaya ya Polisi, kutekeleza majukumu yake
Kwa mwaka 2024, IPOA ambayo imeundwa kwa sheria ya Bunge, mamlaka ilipokea na kushughulikia malalamiko 1,943 , ilihitimisha uchunguzi 597, ilikagua vituo 723 vya polisi, na kufuatilia operesheni 38 zilizofanywa na Polisi.
Tumeona hivi sasa wapo askari Polisi wa Kenya, wako mahakamani wakikabiliwa na mashitaka ya kusababisha vifo vya waandamanaji na kilichofanya wabainike, ni CCTV footage, picha za mnato na video zilizopigwa na raia au vyombo vya habari.
Kwa maneno mengine, picha hizi zimesaidia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa wahalifu au magenge ya kihalifu na ndio maana nasema kwa hali ambayo Tanzania tunapitia kwa sasa, mnaonaje tukawa tunarekodi matukio haya ya ukamataji?
Wala tutakuwa hatuvunji sheria yoyote kwa sababu ukamataji usiofuata sheria unageuka kuwa uhalifu, kwa sababu ya uzubavu wetu umefanya umechangia leo hii kuna wapendwa wetu hatujui wako hai au wamekufa, tuweke msiba au matanga.
Mwaka 1995, Polisi walimkamata mwandishi wa habari Edna Ndejembi na kumnyang'anya kamera kwa madai aliwapiga picha polisi wakiwa kazini, wakati wanapiga mabomu msafara wa Augustino Mrema alipokuwa akielekea Kiraracha.
Walimfungulia mashitaka ya jinai kwa kuwapiga picha Polisi wakiwa kazini lakini kesi ilikufa kifo cha mende kwani hakimu alimpa mkuu wa upelelezi (OC-CID), kitabu cha Kanuni ya Adhabu na kumtaka aonyeshe hilo kosa liko kifungu gani cha sheria.
Alishindwa, na kesi hiyo ilifutwa siku ya kwanza tu ilipofikishwa mahakamani, kwa hiyo na sisi tutakuwa hatufanyi kosa kuwapiga picha watu wanaojitambulisha ni polisi, wamevaa kiraia, hawatoi vitambulisho kwa sababu ukamataji huo hauna uhalali kisheria.
Ukamataji halali umeelezwa umefafanuliwa katika Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022 inasema mtu yeyote atakamatwa na kuwekwa mahabusu ikiwa tu alikamatwa kihalali.
Ukiisoma CPA na Kanuni za utendaji kazi wa Jeshi la Polisi, zinaeleza vizuri namna ya ukamataji ikiwamo Askari Polisi kujitambulisha (hii ni pamoja na kutoa vitambulisho kama wako kiraia) na kumweleza mshukiwa kosa analotumiwa nalo.
Huo ndio utaratibu, sasa ukisikiliza simulizi za watu waliotekwa, utasikia ndugu au marafiki wanasema walikuja na gari Toyota Landcruiser nyeupe au rangi nyingine, wana bunduki (hizi SMG, AK 47 au bastola) na kujitambulisha wao ni polisi.
Hawatoi vitambulisho vyovyote na wakati mwingine wanatumia nguvu kupitiliza, huu sio ukamataji unaoelezwa kuanzia kifungu kile cha 11 hadi cha 37 cha CPA na kama ukamataji wa aina hii hauzingatii vifungu hivyo unageuka kuwa utekaji.
Hatuwezi kuendelea kushuhudia ndugu zetu wakikamatwa kiholela na watu wanaojitambulisha kuwa ni Polisi, lakini hawafiki vituo vya Polisi, zinapita siku, wiki, miezi hadi miaka hawajulikani walipo, ni lazima Watanzania tubadilike.
Nilifurahishwa sana na kauli ya Kamanda wa Polisi wa Geita, Safia Jongo aliyoitoa Aprili 9, 2025 akiwataka wananchi kutokubali kukamatwa na mtu yeyote anayedai kuwa askari polisi bila kuonyesha kitambulisho na kueleza kituo gani alichotokea.
Kwa mujibu wa RPC Safia, kumekuwepo na matukio ya utekaji, yanayodaiwa kufanywa na watu waliovaa sare za polisi, wakiwa kwenye magari yanayodaiwa kuwa ya Serikali, lakini hawatoi uthibitisho wowote kwa wananchi.
Alisema jambo hilo linatia hofu wananchi na kuathiri imani kwa vyombo vya dola.
"Askari wa kweli anapokwenda kukamata mtu lazima ajitambulishe kwa jina, awe na kitambulisho na aseme anatoka kituo gani. Kama hana hivyo, huyo si askari ni mtu wa kawaida ambaye anaweza kuwa jambazi au mhalifu," alisema Safia.
Pamoja na ushauri mzuri wa RPC Safia, lakini simulizi za wengi waliopotezwa na watu waliojitambulisha ni polisi, zinaeleza namna nguvu kubwa kupita kiasi inavyotumika na vitisho kwa ndugu wanaojitokeza kuhoji ukamataji huo.
Lakini ili kuepuka kuingia matatizoni, ndio maana nashauri ndugu, jamaa, marafiki au hata wapita njia wanapoona sokomoko lolote au watu wanamkamata ndugu yake wachomoe simu zao janja na kurekodi na kupiga picha za wahusika.
Ripoti ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ya Robo ya mwaka inayoishia Juni 2025, inaonyesha simu janja ziko milioni 25 hapa Tanzania na hii ina maana kubwa sana, kwamba kati ya watu 10, hawezi kukosekana mwenye simu janja.
Lakini woga wa watanzania na kutojali hata tu kupiga picha au video mtu anaposukwa sukwa na watu, kunafanya leo kuna ndugu zetu wametekwa na kupotezwa na hawajulikani walipo, hapa watanzania tujitafakari sana.
Hebu fikiria kama sio raia mwema aliyerekodi video ya jaribio la kumteka mfanyabiashara Deogratius Tarimo katika eneo la Kiluvya wilayani Ubungo Jijini Dar es salaam, wale watu wangefahamikaje? Watanzania tuamke.
Mara zote polisi wamekana kuhusika na utekaji unaoendelea nchini, kwa msimamo huu tu unatosha kutupa uhalali wa kuhoji vitambulisho kwa wanaowakamata ndugu zetu na kuwapiga picha kwa wazi au kwa siri.
Ili ndugu au marafiki zetu wasipoonekana, tuseme waliomchukua ni hawa hapa na walikuja na gari hili hapa, na wala tusisubiri tu wakati wanapomkamata ndugu yako, hapana. Tutilie shaka tukio lolote lile la ukamataji wa askari wasio na sare.
Kama nilivyotangulia kusema, kwa majirani zetu Kenya wananchi wana mwamko mkubwa na mfano mzuri ni tukio la kutekwa kwa mwanaharakati Maria Sarungi nchini humo, ambapo video zilipigwa na gari lililomteka likawekwa wazi.
Siamini kama Watanzania wanahitaji somo la kupiga picha za mnato au video, kwa sababu tunazipiga sana huko kwenye tafrija za kumbukumbu za kuzaliwa (birthday party) na tunachukua picha za matukio mbalimbali ya kijamii huko mitaani.
Ninatamani kuona kila Mtanzania mwenye simu janja anarekodi tukio lolote analoliona sio la kawaida iwe ni nyumbani kwake, barabarani au mtaani hasa aya ya ukamataji holela kwani picha yako moja inaweza kuokoa uhai wa mtu au watu.
Kwa sababu tukio hilo likishaelezwa ni utekaji, unachofanya ni kurusha mitandaoni video au picha ulizorekodi, kitendo hicho kitasaidia kufahamu gari na sura za watu waliohusika na tukio hilo, tofauti na hivyo tutaendelea kuwapoteza ndugu zetu.
Lakini lingine ambalo ni muhimu sana, ni kufunga kamera za usalama (CCTV) nyumbani na angalau moja au mbili iangazie barabarani, kwa sababu kama katika mtaa wenye nyumba 10 au 20, hata nyumba nne zikiwa na CCTV inasaidia.
Ni lazima kuna kamera itawanasa tu hao watekaji kuanzia wanapofika na kuondoka na usafiri walioutumia.
0656600900