Tuzo Caf sio rahisi, tumepiga hatua kubwa

Katikati ya wiki iliyomalizika, Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf) lilitoa orodha ya washindani wa vipengele tofauti vya tuzo zake kwa mwaka 2023.
Vipengele hivyo ni mchezaji bora Afrika, mchezaji bora Afrika anayecheza ndani ya Afrika, kocha bora wa mwaka, kipa bora wa mwaka na klabu bora Afrika ya mwaka.
Tanzania hatujaachwa nyuma katika orodha ya washindani ambayo Caf waliitoa ambapo klabu za Simba na Yanga na kipa Djigui Diarra wametajwa kuwa miongoni mwa washindani.
Mafanikio ya Yanga na Simba kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2023/2024 yameonekana kuzibeba na kuzifanya ziingizwe katika orodha ya washindani wa kipengele cha klabu bora Afrika mwaka 2024.
Katika kipengele hicho, Yanga na Simba zinashindania tuzo dhidi ya Al Ahly na Zamalek za Misri, Petro Atletico (Angola), TP Mazembe (DR Congo), Dreams (Ghana), RS Berkane (Morocco), Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini) na Esperance ya Tunisia.
Kipa wa Yanga, Djigui Diarra yeye ameingia katika kinyang’anyiro cha kuwania tuzo ya kipa bora wa mwaka Afrika.
Diarra anawania dhidi ya Oussama Benbot (Algeria / USM Alger), Andre Onana (Cameroon / Manchester United), Yahia Fofana (Ivory Coast / Angers), Lionel Mpasi (DR Congo / Rodez), Mostafa Shobeir (Misri / Al Ahly), Munir El Kajoui (Morocco / RS Berkane), Stanley Nwabali (Nigeria / Chippa United), Ronwen Williams (Afrika Kusini/ Mamelodi Sundowns) na Amanallah Memmiche (Tunisia / Esperance).
Kiuhalisia sio jambo rahisi kwa Yanga, Simba na Diarra kupata tuzo wanazowania kwa vile washindani wengine waliopo katika vipengele hivyo wanaonekana kuwa na vigezo vingi vya kuwaweka kipaumbele kulinganisha na wetu.
Ukianzia katika kipengele cha klabu bora ya mwaka, kuna ugumu kwa Yanga au Simba kupata ushindi mbele ya timu kama Al Ahly, Zamalek, Esperance, Mamelodi Sundowns na RS Berkane.
Timu hizo zimepata mafanikio makubwa ndano ya nchi zao na mashindano ya klabu Afrika kulinganisha na Yanga na Simba hivyo zenyewe zina nafasi kubwa ya mojawapo kutwaa tuzo.
Ahly imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Misri na ligi ya mabingwa Afrika wakati Zamalek imechukua Kombe la Shirikisho Afrika na pia imetwaa taji la Caf Super Cup.
Ikumbukwe kwamba Yanga na Simba katika msimu uliopita ambao ulimalizika mwaka huu, ziliishia katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika huku timu za Mamelodi na Esperance zikifika juu zaidi yao.
Ukitathmini kipengele ambacho Diarra anawania tuzo, utaona ni kwq namna gani nyota huyo wa Mali anategemea zaidi miujiza ili aweze kushinda tuzo hiyo.
Ronwen Williams wa Mamelodi na timu ya taifa ya Afrika Kusini, hivi karibuni aliandika historia ya kuteuliwa kuwa miongoni mwa wachezaji wanaowania tuzo ya kipa bora wa dunia katika tuzo za Ballon d’Or lakini pia aliiongoza Afrika Kusini kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 huku pia akiiongoza Mamelodi Sundowns kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Afrika Kusini na kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Huo ni mfano tu lakini pia yupo kipa kama Mostafa Shobeir ambaye ametoa mchango mkubwa katika kuiwezesha Al Ahly kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na taji la Ligi Kuu Misri.
Lakini hata ikitokea Simba, Yanga na Djigui Diarra wamekosa tuzo, Tanzania hatupaswi kujiona wanyonge na badala yake tunatakiwa kujipa pongezi kubwa.
Kuteuliwa kwao kuingia katika ushindani wa kuwania tuzo za Caf kuna maana na heshima kubwa kwa wahusika wenyewe na Tanzania kiujumla na kuna faida kwa nchi yetu.
Ni ishara na uthibitisho kwamba soka letu limepiga hatua jambo linalopelekea klabu zetu kupata mafanikio katika mashindano ya klabu Afrika ambayo mwanzoni timu za Tanzania zilikuwa zinasindikiza tu.
Kupata mafanikio katika mashindano ya klabu Afrika kunaipandisha timu thamani lakini pia mchezaji mmojammoja anapata fursa ya kujiweka sokoni kwa vile mashindano hayo yanafuatiliwa na idadi kubwa ya timu ndani na nje ya Afrika.
Thamani ya klabu na ligi yetu ikipanda, inavutia kampuni na taasisi mbalimbali kuwekeza fedha kupitia udhamini na hivyo kupunguza gharama ambazo timu zinatumia katika kujiendesha lakini pia kuboresha hali ya maisha kwa wachezaji na maofisa wa benchi la ufundi.
Kwa upande mwingine mafanikio haya tunayopata, yanatakiwa kuwa chachu ya kurekebisha mapungufu ambayo tunayaona katika mpira wetu ambayo kama tukiyaacha yaendelee, yanaweza kufanya tupoteze hizi sifa tunazopata sasa.
Baadhi ya mapungufu hayo ni uwepo wa viwanja kadhaa ambavyo bado havikidhi vigezo na viwango vya kutumika kwa mechi za ligi lakini pia uchezeshaji usioridhisha wa marefa.
Tunatakiwa kujivunia hiki kinachotokea kwenye tuzo lakini kisitusahaulishe wajibu wetu.