Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tusipowekeza kwenye elimu tunajihujumu wenyewe

Katika jamii yoyote ile inayotamani maendeleo ya kweli, elimu ni msingi mkuu unaojenga dira ya mafanikio.

Elimu huongeza maarifa, ujuzi, na uwezo wa mtu binafsi na taifa kwa ujumla.

Kwa mantiki hiyo, uwekezaji katika elimu si hiari bali ni wajibu wa lazima kwa

Serikali, wazazi na jamii nzima.

 Ninaposema tusipowekeza kwenye elimu tunajidanganya, kauli hii isichukuliwe kiwepesi, bali kama onyo la wazi dhidi ya hatua yoyote inayoweza kuleta maafa kwa kizazi kijacho.

Uwekezaji kwenye elimu hauhusiani tu na kujenga madarasa au kununua madawati, bali ni pamoja na kuhakikisha walimu wanapata motisha, wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunzia, na kwamba shule zinapokea fedha za ruzuku kwa wakati ili kuendesha shughuli zao za kila siku.

Fedha hizi ni muhimu kwa uendeshaji wa shule za msingi na sekondari, hasa hivi sasa ambapo Serikali yetu inatekeleza sera ya elimu bila malipo.

Nimefuatilia ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali iliyotolewa hivi karibuni, na kuonyesha kiasi cha Sh1.25 bilioni za kugharimia elimu bila malipo hazikufikishwa katika mamlaka 15.

Hii inamaanisha katika maeneo hayo kuna nakisi na bila shaka athari yake itajidhihirisha tu katika utoaji wa elimu bora.

Kwa fedha hizo kutofika, kwanza, shule hukosa fedha za kununua vifaa muhimu vya kufundishia na kujifunzia.

Mwalimu hawezi kufundisha kwa ufanisi bila vitabu vya kutosha, vifaa vya maabara na zana nyinginezo.

Pili, kukosekana kwa ruzuku kunaathiri huduma za msingi kama chakula kwa wanafunzi wa bweni, usafi wa mazingira na matengenezo ya majengo ya shule.

Kwa mfano, shule inayowahifadhi wanafunzi wa kutwa inaweza kushindwa kutoa chakula cha mchana, hali inayowafanya watoto kukaa njaa na kushindwa kuzingatia masomo.

Zaidi ya hayo, matundu ya vyoo yasipokarabatiwa huleta hatari ya mlipuko wa magonjwa, hivyo kuhatarisha afya za wanafunzi. Katika mazingira ya aina hii, utoaji wa elimu unakuwa jambo la muhali.

Kwa nchi yoyote inayotaka kuwa na uchumi wa viwanda, teknolojia ya kisasa, na utawala bora, hakuna njia ya mkato ila kupitia elimu.

Huwezi kupata wataalamu wa afya, wahandisi, walimu, majaji, au viongozi bora bila kuwa na mfumo thabiti wa elimu unaohitaji uwekezaji mkubwa wa kibajeti.

Tukumbuke kila shilingi inayowekezwa kwenye elimu ni sawa na kupanda mbegu ya maendeleo ya taifa.

Uwekezaji huu unapaswa kuwa wa kimkakati.

Serikali inapaswa kuongeza bajeti ya elimu kila mwaka, kuhakikisha fedha zinatolewa kwa wakati, na kuweka mifumo ya ufuatiliaji ili kuhakikisha matumizi sahihi ya fedha hizo.

Vilevile, sekta binafsi, taasisi za kiraia, na mashirika ya kimataifa yanapaswa kushirikiana na Serikali kufadhili elimu kupitia programu maalumu kama vile ufadhili wa masomo, ujenzi wa shule, au mafunzo kwa walimu.

Madhara ya kutowekeza vya kutosha kwenye elimu huanza kuonekana polepole, lakini hatimaye huathiri kila mtu.

 Vijana wasioelimika huongeza idadi ya wasio na ajira, wanaoangukia kwenye uhalifu, mimba za utotoni, na uzembe kazini. Taifa lenye raia wengi wasioelimika haliwezi kuwa na nguvu kazi yenye tija wala uongozi wenye maono.

Watoto wa familia masikini ndio wanaoumia zaidi pale serikali inaposhindwa kutoa ruzuku, kwa kuwa hawawezi kumudu michango mbadala ya kuendesha shule.

Hivyo, pengo la kielimu kati ya walionacho na wasionacho huongezeka, jambo ambalo linaweza kuchochea mgawanyiko wa kijamii na kisiasa.

Nisisitize hakuna taifa lililoendelea bila kuwekeza kwa dhati katika elimu. Tusipowekeza leo, tutajikuta kesho tukikabiliana na kizazi kisicho na ujuzi, kisicho na maadili, na kisicho tayari kuchukua nafasi ya uongozi au uzalishaji.

Serikali na jamii kwa ujumla hatuna budi kuhakikisha elimu inapewa kipaumbele cha juu katika mipango ya maendeleo.

Fedha za ruzuku ni kama damu katika mwili wa shule, tusipokuwa na bajeti ya kutosha, shule haziwezi kuishi, na bila shule haiwezekani kuwa na taifa lenye ustawi.

Tusijihujumu. Kuna maeneo mengi tunaweza kupunguza matumizi yasiyo na ulazima, tukaelekeza bajeti ya kutosh kwenye maendeleo ya sekta ya elimu.