Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Pasaka huufunua upendo wa Mungu

Bwana Yesu asifiwe! Wiki inayoanza kesho Jumatatu Wakristo hapa nchini wataungana na wenzao ulimwenguni kote kuadhimisha sherehe ya Pasaka kuanzia Alhamisi Kuu, Ijumaa Kuu kisha Jumapili ya Pasaka.

Tunapoelekea kuadhimisha sikukuu hiyo ni vyema kufahamu yanayompasa Mkristo ili kusherehekea siku hiyo muhimu ipasavyo.

Pasaka ni sikukuu kubwa na yenye historia kubwa katika maisha ya wanadamu tangu mwanadamu wa kwanza Adamu hata kizazi cha leo. Ingawa sikukuu hii huonekana ya kawaida, lakini imebeba vitu muhimu sana vya ki-Mungu katika maisha ya mwanadamu.

Tunaposherehekea sikukuu hiyo haitoshi kula, kunywa na kuvaa mavazi mapya, bali inatupasa kuona wajibu wetu katika kusherehekea sikukuu hii.

1. Pasaka huufunua upendo wa Mungu kwa mwanadamu (Yoh 03:16)

Maandiko yanathibitisha kuwa Upendo wa Mungu ulifunuliwa katika maisha ya mwanadamu kupitia tendo la pasaka, Mungu alimtoa mwanawe Yesu Kristo siyo tu azaliwe, bali ayapitie mateso ili kuuthibitisha upendo wake katika kumkomboa mwanadamu.

Ni vyema kutambua kuwa tunao wajibu wa kuufunua upendo wa Mungu kwa wanadamu pia kwa kuishi maisha ya kupendana sisi kwa sisi, tena kwa upendo wa agape ambao hautazami vigezo kama Mungu alivyouonesha kwetu kupitia Pasaka.

2. Pasaka huufunua msamaha wa Mungu kwa mwanadamu. (Waefeso 01:07)

 Maandiko yanaonesha kuwa katika kifo cha Yesu kuna msamaha wa dhambi ambao wanadamu wanaupata kutoka Mungu, hii ikimaanisha kuwa Mungu alipotaka kuutangazia ulimwengu na wanadamu wote msahama wa dhambi alimtoa mwanawe kuwa pasaka.

Kifo cha Yesu kinathibitisha kuwa sasa ulimwengu umepewa msamaha wa dhambi bila kulipa gharama yoyote kama maandiko yasemavyo ni kuwa ni neema tu wala mwanadamu asijisifu kuwa amefanya lolote kustahili (Waefeso 02:08-09).

Ikiwa Mungu aliweza kutoa msamaha wa dhambi bure, je, si zaidi wanadamu kutambua jambo hili na kulienzi?

Tutambue kwamba tunao wajibu mkubwa wa kusameheana na kutohesabiana makosa na hatia kwa sababu Pasaka imekuja kutangaza msamaha.

Njia pekee sahihi yenye maana katika kusherehekea ni kuhakikisha tunasameheana na kutohesabiana makosa ili kilichofanywa na Mungu kiwe na maana zaidi kwetu.

3. Pasaka huifunua amani ya Mungu kwa wanadamu (Isaya 53:05)

Maandiko yanaeleza kuwa “adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake”; akimaanisha kuwa mateso ambayo Yesu aliyapata katika Pasaka ilikuwa kuwapatia wanadamu

 amani; na maandiko yanathibitisha kuwa ni amani ipitayo amani zote za duniani (Yoh 14:27).

Mungu hufurahia kuona mwanadamu akiishi maisha ya amani, ndiyo maana hakuona kuwa ni shida kumruhusu mwanawe kuja ulimwenguni na kuteseka, ili tu amani iwe ya kutosha kwa wanadamu. Ikiwa Pasaka ililetwa ili wanadamu waishi maisha ya amani ni vema na ni hekima kubwa kwa wanadamu kutunza amani baina ya mtu na mtu na zaidi amani ya taifa.

Ni ajabu kuona watu wanasherehekea sikukuu ya Pasaka, lakini ni wavunjifu wa amani, ukweli ni kwamba tunaweza kuienzi siku hii na kuikumbuka kwa usahihi ikiwa tutaienzi amani ya taifa letu na amani kibinafsi kwa kuepuka migogoro ya ndani (Intra-conflict) lakini pia kwa kuhubiri amani katika jamii zetu.

Wakati ambao dunia nzima inaelekea kusherehekea sikukuu ya Pasaka ni vizuri kila mmoja kujiuliza na kujitathmini kwa kiwango gani anawajibikia makusudi ya kiungu katika sikukuu hii ya Pasaka. Yaani, ni kwa kiasi gani mtu anayaenzi maisha ya msamaha au ndiyo maisha yamekuwa ya visasi?

Ni kwa kiwango gani watu wanaishi maisha ya upendo au ndio chuki inatawala maisha kuanzia ngazi ya familia, ndoa, jamii hadi katika maisha ya kisiasa na

 matokeo yake kuwa na jamii isiyo na lugha moja.

Kwa kiwango gani watu wanaienzi Pasaka kwa kuishi maisha ya amani bila kujali itikadi za chama, dini au kabila. Sherehe za pasaka zitakuwa na maana ikiwa watu wataienzi amani ya ki-Mungu bila kujali tofauti yoyote.

Palipo na maisha ya upendo hapo msamaha huonekana, palipo na maisha ya msamaha hapo maisha ya amani hudhihirika na palipo na maisha ya amani ndipo pana umoja na mshikamano; na penye umoja na mshikamano hapo ndipo penye baraka za Bwana. Tuna wajibu wa kuudhihirisha upendo wa Mungu kama alivyotupenda, kuudhihirisha msamaha kwa wengine kama yeye alivyotusamehe na kuwa na amani na watu wote bila kujali tofauti zozote na ndipo baraka za Bwana zitaonekana kuanzia ngazi ya familia hata taifa.

Mchungaji Dk Mulenda Omary ni

Askofu Mstaafu TAG – Kigoma Kusini

Mchungaji Kiongozi – TAG City Light Temple, Matosa Goba,  Anapatikana kwa namba 0673280229