Ni aibu India kuipiku Tanzania kwa uuzaji Tanzanite
Muktasari:
Mmoja wa wanunuzi wakubwa wa madini ya vito kutoka Marekani, aliwahi kuwauliza viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini iwapo kuna migodi ya Tanzanite India kwa sababu akifika huko hupata Tanzanite bora na zenye ukubwa kuliko anayopata Tanzania.
Taarifa kwamba nchi za Kenya na India zimeipita kwa mbali Tanzania kwa kusafirisha madini ya Tanzanite yanayopatikana hapa nchini pekee na kuyauza katika soko la dunia ni jambo ambalo siyo rahisi kuliamini.
Nasema siyo rahisi kuamini kwa sababu haingii akilini hata kidogo, mtu ambaye halimi mahindi anaibuka kinara wa kuuza sokoni mahindi yako anayoyaiba shambani kwako.
Ni heri kama angekuwa anakuja kununua kwa njia ya kawaida na wewe ukanufaika.
Nilimsoma kwa makini Kamishna wa Madini katika Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Paul Masanja hivi karibuni kupitia baadhi ya magazeti nchini akisema kwamba kwa mwaka jana, Tanzania haikufikia hata nusu ya Kenya kwa mauzo ya madini hayo ya vito.
Mwaka jana pekee, Kenya ilisafirisha na kuuza nje ya nchi Tanzanite yenye thamani ya zaidi ya Dola za Marekani 100 milioni (Sh173 bilioni), dhidi ya Dola 38 milioni (Sh45.5 bilioni), zilizouzwa na Tanzania.
Katika kipindi hicho cha mwaka jana, India iliuza Tanzanite zenye thamani ya zaidi ya Dola 300 milioni za Marekani(Sh509 bilioni) kiasi cha baadhi ya wanunuzi wakubwa, hasa kutoka Marekani kujiuliza iwapo madini hayo yanachimbwa India.
Mmoja wa wanunuzi wakubwa wa madini ya vito kutoka Marekani, aliwahi kuwauliza viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini iwapo kuna migodi ya Tanzanite India kwa sababu akifika huko hupata Tanzanite bora na zenye ukubwa kuliko anayopata Tanzania.
Taarifa zinaeleza kuwa, zaidi ya asilimia 80 ya Tanzanite inayopatikana Mirerani, Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, huuzwa kwa njia za panya nje ya nchi na kwamba Serikali imeanza kuchukua hatua.
Kama nilivyosema awali, hili ni jambo la kushangaza sana. Ninajiuliza; hivi haya madini nani anayeyatorosha kwenda nchi za nje? Ni wazi kuwa watu wachache waliopewa jukumu la kusimamia sekta ya madini, wamekuwa wakishirikiana na watu wa nje kutorosha madini hayo.
Tumejua wizi wa madini haya kwa sababu tu yanapatikana pekee Tanzania. Tujiulize wizi huu wa madini yetu ukoje katika madini mengine ambayo pia yanapatikana katika nchi nyingine?
Kwa hakika, raslimali za nchi hii zinaliwa na watu wengine, huku Watanzania wakibaki mikono mitupu.
Ni wazi kuwa watu wanaotorosha madini haya hawapiti vikachani, wanapita katika maeneo ya mipaka yetu, lakini ulafi wa baadhi ya maofisa wa Serikali ndiyo imetufikisha tulipo kwa sasa.
Ni jambo la ajabu leo nchi kuendelea kuwa masikini, wakati madini na rasilimali nyingine zinanufaishe nchi nyingine.
Kuna wakati nilishuhudia waziri mmoja akipokea msaada wa wahisani waliokuwa wamejenga choo cha shule.
Kwa nini tunafikia hatua ya kujengewa vyoo wakati tuna utajiri mkubwa kiasi hiki? Ni kutokana na kushindwa kutumia vyema rasilimali zetu.
Niishauri Serikali sasa iweke mikakati ya kulinda madini yetu yasitoroshwe kwenda nje ya nchi, badala yake yawanufaishe Watanzania wenyewe.
Iunde chombo maalumu chenye askari, kitakachodhibiti utoroshaji madini nje ya nchi. Pia watu wote wanaokamatwa wakitorosha madini bila ya kupitia taratibu zinazotakiwa wafilisiwe mali zao.
Bila ya kuwa na sheria kali, madini yetu na rasilimali nyingine zitaendelea kutoroshwa.
Hatua nyingine ni kujenga soko kubwa la kimataifa la kuuza na kununua madini, ili biashara ya madini hayo ifanyike hapa nchini.
Kinachofanyika hivi sasa ni kwamba watu wanaotorosha madini kwenda nje kutafuta soko lenye bei nzuri zaidi, wakati kama tungekuwa na soko la kimataifa la madini biashara hiyo ingefanyika hapa hapa nchini.
Kama India imeweza kuanzisha soko la kimataifa la madini kwa nini sisi ambao ndio tunayachimba tusiwe ndio kituo kikuu cha kuuza madini?
Nadhani hili linawezekana isipokuwa linaweza kushindikana ama kutokana na watu wanaonufaika na kutokuwapo kwa soko hilo kama wataingiza mikono yao katika suala hili.
Najua kitu ambacho kimekuwa kikituangusha siku zote watanzania ni kukosa uzalendo. Baadhi ya viongozi wetu wanaangali zaidi masilahi yao badala ya kuangalia masilahi ya nchi.
Ni kutokana na kukosa uzalendo kwa baadhi ya viongozi wetu ndiyo maana hadi leo nchi yetu bado inangia mikatana na wawekezaji ambayo haiana tija.