Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KONA YA MZAZI: Tusiwabagaze yatima, ni faraja kwa familia

Muktasari:

  • Watoto wanaopoteza wazazi hupitia nyakati ngumu, hivyo wanahitaji uangalizi wa karibu wa kutoka kwa ndugu

Dar es Salaam. Kupoteza mzazi ni moja ya matukio yenye maumivu makubwa katika maisha ya mtoto. Katika familia nyingi za Kitanzania na Kiafrika kwa ujumla, watoto wanaopoteza wazazi wao hupewa malezi na ndugu wa karibu kama vile bibi, babu, wajomba, shangazi au kaka na dada wakubwa.

Mfumo huu wa kifamilia umeendelea kuwa nguzo muhimu ya ustawi wa watoto wengi yatima. Hata hivyo, swali linaloendelea kujitokeza ni kama malezi haya yanakidhi kikamilifu mahitaji yao.

Mtaalamu mmoja wa saikolojia anasema  watoto wanaopoteza wazazi hupitia nyakati ngumu, hivyo wanahitaji uangalizi wa karibu wa kutoka kwa ndugu.

Kwangu mimi hii ni hoja mujarabu, kwa sababu  kama mtoto anapata chakula, mavazi na elimu, bado atahitaji upendo, usalama wa kihisia na mtu wa kumfariji.

Nasema hivyo kwa sababu mtoto anayepoteza mzazi anahitaji zaidi mahitaji ya msingi sambamba na mtu wa kumsikiliza, kumtia moyo na kumfanya ajione bado ana thamani ndani ya familia.

Katika mazingira mengi, ndugu wanaowalea watoto hao hujitahidi kuwapa makazi na malezi mazuri licha ya changamoto za kiuchumi na jukumu hilo si rahisi, lakini lina umuhimu mkubwa kwa familia.

Ni kweli kwamba changamoto kubwa ni kuhakikisha watoto wote wanapata upendo sawa bila kujisikia kutengwa, watoto wanaoishi na ndugu mara nyingine hujihisi kama wageni ndani ya nyumba hasa wanapolinganishwa na watoto wa mwenyeji.

Baadhi ya watoto yatima hukumbana na ubaguzi wa kimya kimya ndani ya familia wanazoishi. Kuna watoto wanaolelewa vizuri kabisa, lakini wapo wanaonyimwa nafasi sawa katika elimu, mavazi au hata kufanya jambo fulani kwenye ile familia anayolelewa. Hali hii huwaathiri sana.

Wengi wao huwa wanajihisi kama hawapendwi au hawana sauti ndani ya familia hali inayowafanya wakue wakiwa na huzuni, hasira au kujitenga. Wengine hupoteza ari ya masomo na kujiona hawana mwelekeo mzuri wa maisha.

Kwa upande mwingine, wapo watoto wengi wanaofanikiwa kutokana na malezi ya ndugu waliowapokea kwa moyo wa upendo na uwajibikaji.

Mwalimu Grace Mushi niliyezungumza naye kuhusiana na hili aliniambia kuwa ameshashuhudia watoto yatima wakifanya vizuri darasani wanapopata mazingira mazuri ya malezi.

“Mtoto akijisikia anakubalika ndani ya familia mpya, hata maendeleo yake shuleni yanakuwa mazuri. Upendo na kupewa nafasi ya kujieleza vina mchango mkubwa,” anasema Mwalimu Grace.

Anasisitiza kuwa shule pia zinalo jukumu la kuwasaidia watoto hao kwa kuwapa ushauri nasaha na kuwafuatilia kwa karibu wanapopitia mabadiliko makubwa ya maisha.

Mbali na changamoto za kihisia, suala la uchumi pia huathiri malezi ya watoto wanaoishi na ndugu baada ya wazazi kufariki dunia.

Familia nyingi hupokea watoto hao bila maandalizi ya kifedha, hali inayoongeza mzigo wa matumizi ya kila siku. Wakati mwingine watoto hulazimika kufanya kazi za nyumbani kupita kiasi au kuacha shule kutokana na ukosefu wa uwezo wa kifedha.

Anasema ndugu na jamaa wanapaswa kushiriki kuzisaidia familia zinazowalea watoto yatima badala ya kuacha jukumu lote kwa ndugu wachache.

Familia inayopokea mtoto yatima inahitaji kutiwa moyo na kusaidiwa. Tukifanya hivyo tunawapa watoto hawa nafasi bora ya kukua katika mazingira yenye matumaini.

Wataalamu wa malezi wanasema jambo muhimu si tu mtoto kupewa sehemu ya kuishi, bali kuhakikisha anapata mazingira yanayomjenga vema kusudi asijisikiwa kuwa ni mkiwa. Kwa sababu mtoto anahitaji kusikilizwa na kuonyeshwa kuwa bado ana thamani licha ya kumpoteza mzazi.

Maisha yetu ya sasa, malezi ya watoto wanaoishi na ndugu baada ya wazazi wa kufariki dunia, yanaendelea kuwa sehemu muhimu ya mshikamano wa kifamilia.

Hata hivyo, ili malezi haya yakidhi kikamilifu mahitaji ya mtoto, yanahitaji zaidi ya huruma. Yanahitaji upendo wa kweli, usawa, uvumilivu na msaada wa hali na mali.

Mwisho wa yote, mtoto anayepoteza mzazi hahitaji kuhurumiwa tu, bali kupewa nafasi ya kuendelea kuota ndoto, kuaminiwa na kukua katika mazingira yanayomfanya ajione salama na mwenye thamani kama watoto wengine.