Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Askofu Kassala ahimiza malezi sawa kwa watoto, aonya ubaguzi

Askofu Jimbo Katoliki la Geita, Flavian Kassala.

Muktasari:

  • Marehemu Sussana ameacha watoto wanane, wajukuu 77, vitukuu 125 pamoja na kilembwe kimoja.

Geita. Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita, Flavian Kassala ametoa wito kwa wazazi na walezi nchini kutimiza wajibu wao wa malezi na usimamizi bora wa watoto bila ubaguzi.

Askofu Kassala amesema kutokana na maendeleo ya kiuchumi na teknolojia, kwa sasa imeibuka jamii hatarishi ambapo baadhi ya watu hawapendi kuzaa huku wengine wakitelekeza watoto baada ya kuwazaa.

Askofu huyo ametoa rai hiyo leo Mei 29, 2026 wilayani Chato mkoani Geita, katika ibada ya mazishi ya aliyekuwa mama mzazi wa Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli, Mama Sussana Ngolo.

Amesema wazazi wanapaswa kutambua kuwa licha ya sayansi kuruhusu utoaji salama wa mimba, kitendo hicho ni ukatili dhidi ya watoto kabla ya kuzaliwa na pia ni kinyume na mapenzi ya Mungu.

“Tunayo jamii ambayo ni hatarishi kwa sasa. Wapo wasiopenda kuzaa na ukifuatilia kwa undani si wote ni watoto yatima, mwingine utakuta anazaa na kumtelekeza mtoto. Tunao wengine waliotupwa siku ya kwanza ya maisha yao, ndiyo maana nyumba za kulelea watoto yatima zinaongezeka,” amesema Askofu Kassala.

Ameongeza kuwa licha ya Mama Sussana kuwa mtoto pekee katika familia yao, alijitahidi kuwalea watoto wote 15 aliojaliwa na hivyo taifa likapata viongozi na watu wachapakazi.

Pia, amesema hatma ya watoto ipo mikononi mwa Mungu, hivyo wazazi hawapaswi kuwa na ubaguzi katika malezi yao.

Ibada ya mazishi imeongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza, Renatus Nkwande, akisaidiana na Askofu Kassala pamoja na Askofu wa Jimbo Katoliki la Bunda, Simon Masondole.

Katika tukio hilo, Makamu wa Rais, Balozi Dk Emmanuel Nchimbi ameongoza waombolezaji huku viongozi wengine waliohudhuria ni Makamu wa Rais mstaafu, Dk Philip Mpango, Waziri Mkuu mstaafu Kassim Majaliwa, Naibu Waziri Mkuu mstaafu Dk Doto Biteko, Spika wa zamani wa Bunge na Rais wa Mabunge Duniani, Dk Tulia Ackson  na viongozi wengine wa Serikali.

Akisoma historia ya marehemu kwa niaba ya familia, Marko Magufuli amesema Sussana alizaliwa Juni 1, 1936 katika Kijiji cha Matale Ng’ombe, Kata ya Misasi wilayani Misungwi mkoani Mwanza akiwa mtoto pekee katika familia.

Amesema mwaka 1954 aliolewa na Joseph Magufuli na baadaye mwaka 1958 walifunga ndoa katika Kijiji cha Sungusila, Kata ya Sungusila wilayani Geita.

Katika maisha yake, marehemu alijaliwa watoto 15, kati yao wanawake wanane na wanaume saba. Pia alikuwa mchapakazi aliyefanya shughuli za kilimo na kuhifadhi watu 38 nyumbani kwake, hali iliyowafanya watoto wake kujifunza uchapakazi akiwemo aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Pombe Magufuli.

Marehemu alianza kuugua mwaka 2018 akisumbuliwa na maradhi ya kiharusi, kisukari na shinikizo la damu.

Amesma katika kipindi hicho alikuwa akipatiwa matibabu katika hospitali mbalimbali nchini ikiwemo Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya Muhimbili na Hospitali ya Bugando.

Imeelezwa kuwa asubuhi ya Mei 25, 2026 hali yake ilibadilika na kupelekwa Hospitali ya Wilaya ya Chato ambapo alipatiwa matibabu na hali yake kuonekana kuimarika kabla ya kuruhusiwa.

Hata hivyo, jioni ya siku hiyo hali yake ilibadilika tena na kufariki dunia majira ya saa 1:40 usiku.