KONA YA MSTAAFU: Maajabu haya! Sasa umri unafanywa kigezo cha kumnyima mstaafu mkopo

Mstaafu wetu aliachia ngazi kwa hiari ili ‘mchuma uondoke’ alipokuwa na miaka 48 miaka 17 iliyopita, wakati shirika alilokuwa mtumwa wake lilipoingizwa ubia, (siyo kuingia lenyewe) na kutoa nafasi kwa waajiriwa wake waliokuwa wanataka kuachia ngazi kwa hiari kufanya hivyo.
Mstaafu wetu hakuwa mzee kiasi hicho, lakini akaachia ngazi ili akafanye kile alichoamini ni ‘kuangalia mambo mengine ya maisha wakati bado ana nguvu’.
Anakiri miaka 17 baadaye leo, bado hajakiona kile alichoamini ni ‘kuangalia mambo mengine ya maisha akiwa bado na nguvu’ kilichomfanya aachie ngazi kwa hiari mchuma uondoke, sana sana ameishia kuangalia shinikizo la juu la damu, kisukari na kiharusi vikiishia kuwa ‘mambo yake mengine ya maisha’ kama vinavyojua kwamba amestaafu na Siri–kali haina mpango wa kumpa matibabu ya bure.
Katika kuhangaika kwake kutafuta mambo mengine ya maisha, akajikuta akiingia mikopo kadhaa kwenye hizi benki zetu za kisasa zilizomo nchini, zikimsaidia kutafuta kwa tochi kile kilichomfanya aache ajira kwa hiari.
Hakukiona na bado hajakiona, pamoja na kwamba kuanzia akiwa na miaka 48 hadi anafikisha miaka 60 kupata mkopo wa benki kwake haikuwa shida, huku benki zenyewe zikimgombania akope kwao.
Hauchi hauchi, unakucha na Mungu ni mwema. Mstaafu wetu akafikisha miaka 60 na akaanza kupokea pensheni yake ya shilingi alfu 50 kwa mwezi na miezi minne mitano baadaye yule mwana mwema wa Msoga akaiongeza shilingi alfu 50 nyingine na pensheni kuwa shilingi laki moja na alfu tano, ambayo miaka 17 iliyopita ilikuwa bado na heshima kubwa kiasi kwamba hata wajukuu zake hawajaanza kuzomoka kuwa ‘Laki si Pesa.’
Wasingeweza kuzomoka hivyo wakati sukari ilikuwa kilo moja ni Sh600, rudia hapo kwa msisitizo, Sh600, huku kilo ya nyama ikiwa Sh900 tu tofauti na sasa kilo ni shilingi… mama wee.. alfu kumi na mbili na hakuna mheshimiwa yeyote anayeshituka kwamba nyama kwa mstaafu sasa ni bidhaa adimu, pamoja na kusingizia maradhi ya kisukari!
Kwa nini wajukuu wasizomoke kuwa Laki si Pesa?
Umri ukasonga mbele na ndipo mstaafu wetu akajua kuwa hajui, pale zile benki za dotcom zilizokuwa zikimgombania achukue mikopo kwao wakati ana miaka 40 hadi 60 zikiweka kipengele kilichokuwa hakipo zamani, cha kumuuliza mstaafu kabla haijampa mkopo wao, ‘Una umri gani?’ na anapojibu umri wake unakaribia ule aliosema Mungu mwenyewe wa miaka 70 na baada ya hapo siku yoyote anaweza kuwa mkazi wa Kinondoni. Ghafla! Mikopo ikaanza kuota mbawa!
Yaani makunyanzi ya usoni na umri wako uliopevuka unatumiwa sasa na baadhi ya benki zetu za dotcom kumnyima mstaafu mkopo wao, usije ukawa mkazi wa Kinondoni bure wakati una mkopo ambao ndiyo itakuwa kama imetoka hiyo, ikirudi pancha, potelea mbali kwamba ni wao wenyewe wanaosema kwa kujidai kuwa ‘Age is nothing but just a number’ Kisambaa kwa msisitizo!
Yaani kuna benki za dotcom sasa hazitoi mkopo kwa mstaafu zikiepusha inachodhani kuwa anaweza akaelekea Kinondoni ghafla na akaishia na hela yao.
Inasikitisha. Yaani mstaafu ambaye aliweza kushika hela zote za nchi hii, leo ndiye pekee anayeweza kuondoka na mkopo wa mtu?
Mbona wako vijana wetu wengi tu wanaotangulia Kinondoni na mikopo ya benki zetu, kwa ajali za bodaboda na hata kutekwa? Kwa nini mstaafu ashitukiwe kukopa? Acheni hizo.
Tumuachie Mungu kazi ya kujua ampeleke mtu lini Kinondoni. Mimi mstaafu ninayetaka kukopa na miaka 75 yangu ninaweza nikaishi hadi miaka 95 na wewe ofisa mikopo unayesimamia kanuni za benki yenu kuwa msiruhusu wastaafu kukopa unaweza ukaenda Kinondoni na miaka 45, mimi unayetumia kanuni zenu kunizuia nisikope nikaenda huko na miaka 91, mpo?
Iondoeni hiyo kanuni yenu ya kuwabagua wastaafu.
Na vibubu navyo vinavyotunza hela ya wastaafu vijiongeze na kuanzisha benki ya kutoa mikopo yenye tozo nafuu kwa wastaafu. Si hela zetu kibao wanazo?
Si wanaweza kukopesha wakopaji wasio wastaafu, ikiwemo Siri-kali, hela yetu? Inashindwa nini kuanzisha benki ya wastaafu? Si wanaweza kujenga majengo ya ghorofa hata nchi jirani kwa hela yetu bila hata kutuuliza tu, huku sisi wenye hela zetu tukiishia kupokea pensheni ya shilingi laki moja kwa mwezi kwa miaka 20 sasa, huku hata wasiohusika wakishindana kuhomola hela zetu!
Ndiyo, anzisheni mara moja benki ya wastaafu itakayotoa mikopo yenye tozo nafuu kwa wenye hela zao, ambayo mstaafu ataweza kukopa hata akiwa na miaka 90, bila kuulizwa umri wake maana hela yake iko kwenu na ndiyo dhamana yake.
Kutuongeza pensheni hamuwezi, japo mnapata kodi ya majengo mnayojenga kwa hela zetu. Kodi hizo zinaishia wapi? Tuambiane.
Mna uzoefu wa kuwakopesha watu hata wasiokuwa wastaafu, mnashindwa kipi kuwafungulia benki ndogo wenye hela zao? Tunasisitiza kwa Kisambaa kingine, ‘Vox populi, vox Dei’ Sauti ya Wengi ni Sauti ya Mungu. Wastaafu bado ni wengi, Mungu atatusikia.
Kama una maoni kuhusu makala haya, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.