Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kilimo cha miwa ni zaidi ya sukari, tunajipangaje?

Wakati Rais Samia akihitimisha ziara yake mkoani Morogoro hivi karibuni, alionesha dhamira yake ya dhati kutaka kurejesha hadhi ya mkoa huo, kwa kuhakikisha viwanda vingi vinafufuka na kuongeza ajira kwa wananchi.

Shauku ya rais Samia ilichochewa zaidi na kile alichokiona wakati akikagua miradi ya bwawa la umwagiliaji la Mtibwa, viwanda vya sukari, kikiwemo cha Mkulazi.

Ni kweli kwamba, viwanda hivi ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuongeza uzalishaji wa sukari nchini na kupunguza utegemezi wa sukari ya nje.

Katika hotuba yake, Rais Samia aliipongeza sekta ya viwanda kwa juhudi zake za kuongeza ajira na kuchangia katika pato la taifa.

Hata hivyo, pamoja na pongezi hizo za Rais Samia kwa sekta ya viwanda vya sukari, hakutakuwa na maana ikiwa hatujaingalia vema sekta ya kilimo cha miwa ambacho kwa maoni yangu, ndiyo chanzo cha viwanda vyetu kuzalisha sukari kwa wingi.

Miwa ya sukari ni zao muhimu la biashara hapa nchini ambalo wastani wake wa uzalishaji kwa wakulima wadogo wanaotegemea mvua ni kati ya tani 70-80 kwa hekta.

Hivyo jitihada za shirika la Kimataifa la uhifadhi wa asili na mazingira (IUCN), likishirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) Kibaha, Chuo cha Sukari cha Taifa na Kampuni ya sukari Kilombero kutoa elimu bure kwa wakulima wa miwa ili kuongeza tija na thamani ya kilimo hicho, lazima ziungwe mkono.

Kwa mujibu wa ofisa miradi wa taasisi ya SUSTAIN Samwel Kajiba zao la miwa linahitaji ikolojia ya mvua kati ya milimeta 1100 na 1500 zenye mtawanyiko mzuri na wastani wa joto 29+ ili kukomaa vizuri na kutoa sukari nyingi.

Aidha wakulima wanapaswa kufahamu kwamba, zao la miwa linahitaji eneo linaloweza kufikika kwa urahisi kwa majira yote ya mwaka ili kurahisisha upelekaji pembejeo shambani

Miongoni mwa elimu inayohitajika kutolewa na wataalamu hao, ni pamoja na utayarishaji wa shamba la miwa ambao aghalabu unategemea msimu wa upandaji.

Katika hatua hii wataalamu wanasema kuwa, maandalizi ya shamba yahusishe utengenezaji wa miundombinu ya barabara na mifereji ya kutoa maji shambani lakini yasihusishe uchomaji moto.

Pia inaelezwa katika utayarishaji wa shamba la miwa inayotarajiwa kutumika kwa ajili ya kuzalishia sukari, uzingatie umbali wa angalau mita 60 kutoka kwenye vyanzo vya maji na wakulima wahakikishe mashamba hayo hayavamii maeneo ya hifadhi.

Kwa ujumla kilimo cha miwa kina faida nyingi ambazo zinaweza kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii hapa nchini.

Tukianza na uzalishaji wa sukari ya ndani ambao hupunguza utegemezi wa sukari kutoka nje, hivyo kuhakikisha upatikanaji wa sukari nchini na kudhibiti mfumuko wa bei.

Kwa upande wa ajira, sekta ya sukari inawezesha kutoa ajira kwa wakulima, wafanyakazi wa viwandani, na wafanyabiashara wadogo wanaohusika katika usambazaji na uuzaji wa sukari.

Mbali na hayo, kilimo hiki huchochea ukuaji wa viwanda vingine vinavyotegemea sukari kama malighafi.

Tukianza na sukari gulu; Sukari gulu ina virutubisho vingi ikilinganishwa na sukari nyeupe, ikiwa ni pamoja na madini ya chuma, kalsiamu, na potasiamu.

Katika zao la miwa, wataalamu wanasema baada ya sukari gulu kuna molases; Molases ni bidhaa ya ziada ya mchakato wa uzalishaji wa sukari na hutumika kama malighafi kuu katika utengenezaji wa bioethanol, ambayo ni nishati safi.

Bioethanol inayotokana na miwa ni nishati safi inayopunguza utegemezi wa mafuta ya petroli ambayo yanachangia uchafuzi wa hewa, kwa upande wa kwanza.

Lakini Bioethanol inaweza kutumika kama nishati mbadala kwa ajili ya kupikia, hivyo kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, na hivyo kuchangia utunzaji wa mazingira kwa upande mwingine.

Vile vile uwekezaji katika uzalishaji wa bioethanol utachochea maendeleo ya teknolojia na miundombinu ya nishati mbadala nchini iwapo elimu kama hii itawafikia wakulima walio wengi.

Nimalizie kwa kusema kuwa, kilimo cha miwa kina nafasi kubwa ya kuchangia maendeleo endelevu nchini Tanzania, kwa kuleta faida kiuchumi, kijamii, na kimazingira. Nishati safi inayotokana na miwa, kama tuliyoitaja hapo juu, ni mfano bora wa jinsi kilimo hiki kinavyoweza kusaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kuboresha maisha ya Watanzania kwa jumla.