Rais Samia ahusisha bei ya sukari na Gen Z
Muktasari:
- Rais Samia amezungumzia sababu inayoweza kuwaingiza vijana barabarani wakati akizindua bwawa la umwagiliaji la Kiwanda cha Sukari cha Mtibwa, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake mkoani Morogoro.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema hatari ya kutokuwepo chakula nchini, kutawaingiza barabarani vijana wa kizazi cha Generation Z.
Kauli ya Rais Samia inaakisi kilichotokea katika mataifa kadhaa ya Afrika, yakitanguliwa na Kenya ambako vijana waliozaliwa kati ya mwaka 1995 na 2009 maarufu Gen Z waliingia barabarani kuandamana kupinga muswada wa sheria ya fedha waliodai unaongeza ugumu wa maisha.
Rais Samia amesema ni jukumu la Serikali kusimamia masilahi ya makundi yote na inapoonekana kuegemea upande wa wananchi, ni kwa sababu ya jukumu hilo.
Rais Samia aliyasema hayo mkoani Morogoro alipozindua bwawa la umwagiliaji la Kiwanda cha Sukari cha Mtibwa, akiendelea na ziara mkoani humo.
Rais amesema hayo, wakati ambao Serikali imeiongeza bidhaa ya sukari miongoni mwa vyakula vinavyohifadhiwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA).
Awali, wazalishaji wa sukari walikuwa wakipewa vibali vya uagizaji bidhaa hiyo unapotokea uhaba.
Amesema inapoonekana Serikali imeegemea upande wa kundi linaloonekana kukosa nguvu haimaanishi ina masilahi huko, bali ni katika msingi wa kutekeleza jukumu la kutetea masilahi ya wote.
“Wanasema chakula ni siasa, kukiwa hakuna chakula ile Generation Z haitatulia itaingia barabarani, au ukiwapandishia sukari kilo kwa Sh7,000 hawatatulia,” alisema.
Alieleza Serikali inaposimamia kundi la wananchi wanaotaka sukari kwa bei ya uhakika na himilivu, msingi wake ni huo.
Sakata la sukari
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, akizungumza bungeni jijini Dodoma wakati wa kuwasilisha bajeti ya wizara hiyo alisema wakati wa utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2023/2024 Serikali ilikabiliwa na tatizo la upungufu wa sukari kutokana na mvua za EL-Nino na tabia za wafanyabiashara kutengeneza uhaba wa sukari kwa kutokuingiza sukari ya kuziba pengo kulingana na vibali vya uagizaji walivyopatiwa, hivyo kupandisha bei ya sukari.
Kutokana na hilo, alisema NFRA sasa itaagiza sukari nje panapotokea pengo na kuwa na sukari ya ziada.
Bashe alisema uhaba wa sukari ulitokea mwishoni mwa mwaka 2023 na mwanzoni mwa 2024, sukari ilipofikia Sh11,000 kwa kilo katika baadhi ya vijiji vilivyopo mkoani Geita.
Bei kubwa ya sukari ilimlazimu Mkurugenzi wa Bodi ya Sukari Tanzania (SBT), Profesa Keneth Bengesi kutangaza bei ya kikomo ya Sh3,200 kwa kilo. Bei ya ukomo ilianza kutumika Januari 23, 2024 na inamalizika Juni 30, 2024.
Kwa mujibu wa Profesa Bengesi mahitaji ya sukari kwa nchi ni tani 552,000 bila ziada, huku mahitaji na ziada ni tani 650,000.
Tamko kwa wawekezaji
Rais Samia jana aliwasihi wawekezaji waendelee kuwekeza kwenye teknolojia na mbinu za kisasa katika uzalishaji ili kupunguza gharama na kuongeza tija zaidi.
Aliahidi kufanyia kazi ombi la ujenzi wa Barabara ya Wami-Dawawa-Madizini lililotolewa na kiwanda cha Mtibwa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Kilimo, Bashe alisema Serikali inatoa Sh220 bilioni ikiwa ni misamaha ya kodi katika sekta ya sukari.
Misamaha hiyo alisema inalenga kuhakikisha sekta ya sukari nchini inaimarika, huku uzalishaji ukiongezeka.
Kwa mujibu wa Bashe, Serikali kwa sasa inaandaa sera ya Taifa ya fedha katika sekta ya kilimo ili kuhamasisha uwekezaji wa muda mrefu.
Alisema mahitaji ya sukari nchini kwa sasa ni tani 650,000, lakini matarajio ya uzalishaji mwaka huu ni tani 550,000.
Amesema ifikapo mwaka 2026, uzalishaji unatarajiwa kufikia tani 750,000, huku mwaka 2030 ukifika tani milioni moja.
Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Mtibwa, Seif Ally Seif alipendekeza kuboreshewa barabara kutoka Wami Dakawa hadi katika eneo la kiwanda.
Pia alipendekeza kuwapo mazingira wezeshi yanayohamasisha uwekezaji na taasisi za fedha ziongeze ukopeshaji.
Amesema yote hayo yatapaswa kubebwa na uwepo wa sera zinazotabirika za uwekezaji.
Alieleza katika mradi wa upanuzi, mitambo 47 imeshafungwa na utakapokamilika itafikia 112.
Alisema uwekezaji umefanyika kwa kuweka mitambo mipya kiwandani na wanachakata miwa tani 180,000 kwa saa, wakitarajia kufikia tani 230,000 mwaka 2027.
Wilayani Mvomero
Akizindua programu ya Tutunzane inayolenga kuwaweka pamoja wakulima na wafugaji katika Wilaya ya Mvomero, Rais Samia ametaka wenyeviti wa vijiji wadhibiti migogoro hiyo badala ya kutanguliza kunyoosha mikono kupokea fedha.
Amesema malalamiko yaliyopo ni uongozi wa vijiji kuwa wepesi wa kunyoosha mikopo kupokea fedha badala ya kutatua migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
“Mamlaka za mikoa na wilaya hakikisheni yeyote atakayeingilia uhuru wa mwenzake kwa kuingiza mifugo kwenye shamba lake, mnamchukulia hatua,” alisema.
Rais Samia amesema programu ya Tutunzane itaepusha migogoro na kutunza amani kwa wakulima na wafugaji wa maeneo mbalimbali.
Pia, ameeleza itaongeza wigo kwa wakulima na wafugaji wa kukopesheka kupitia hati watakazozipata.
Amesema wakulima na wafugaji ni kama watoto waliozaliwa kwenye familia moja, kwa kuwa wanategemeana.
Rais Samia amesema nchi huwa na nguvu zaidi iwapo kutakuwa na umoja, kwani migogoro husababisha machafuko.
Katika maelezo yake, alirejea Katiba ya Tanzania inayomtaka kila mmoja afanye mambo yake bila kuingilia haki ya mwingine.
Aliitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhakikisha inatafuta wadau hasa wa sekta binafsi kuwekeza kwenye programu hiyo kuepusha migogoro ya wakulima na wafugaji.
Hata hivyo, amesema ni vigumu kuyaepuka mabadiliko ya namna ya kulima na kufuga kwa sababu ardhi haiongezeki, huku binadamu wanaongezeka.
“Lazima tuwe wabunifu wa kuja na mbinu zitakazofanya ardhi tuliyonayo izalishe zaidi. Kama ni mkulima azalishe zaidi kwa kipande cha ardhi alichonacho vivyo hivyo kwa mfugaji,” amesema.
Alitaja uwepo wa changamoto ya mabadiliko ya tabianchi, akisema teknolojia za kisasa ni muhimu kuhakikisha wanalima, kufuga na kupata vya kutosha.
Awali, akizungumzia programu hiyo, Waziri Bashe alisema wakulima 1,066 wamesajiliwa.
Bashe alisema Sh70 milioni imeombwa na Halmashauri ya Mvomero kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.
“Tayari nimeshamwelekeza Katibu Mkuu (Gerald Mweli) kuangalia fedha hiyo na kuifikisha kwa halmashauri hiyo kwa ajili ya kutekeleza programu,” alisema.
Akizungumza katika tukio hilo, mbunge wa Mvomero, Jonas Zeelan aliomba kujengwa kwa kilomita 25 za barabara ya Magole kwenda Mvomero.
Alisema barabara hiyo inauunganisha Mkoa wa Morogoro na wa Tanga hivyo anaomba ijengwe kwa kiwango cha lami.
Pamoja na barabara hiyo, Zeelan ameomba Mvomero iwe moja ya maeneo yatakayonufaika na mradi wa maji unaotarajiwa kuhudumia Morogoro Mjini.
Mbunge huyo alieleza uwepo wa changamoto ya tembo katika Tarafa ya Mlari, akisema inawalazimu wananchi waishie kulima ufuta pekee.
“Naomba wale tembo warudishwe hifadhini na kujengwe ukuta utakaozuia wasitoke hifadhini na kuja katika mashamba ya wakulima,” alisema.
Ombi kuhusu mradi wa maji, lilijibiwa na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso aliyesema mradi huo hautafika Morogoro Mjini kabla haujawanufaisha wakazi wa Mvomero.
Kuhusu barabara, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa alisema ujenzi umeshaanza kwa upande wa Tanga na kwamba itafika hatua kipande hicho kitajengwa.