Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jamii ichukue hadhari kujikinga na homa ya nyani

Muonekano wa viganja vya mkono vya mtu mwenye ugonjwa wa homa ya nyani. Picha na Mtandao

Hivi karibuni Shirika la Afya Duniani (WHO) lilibainisha ongezeko la maambukizi ya homa ya nyani, maarufu kama Mpox kwa baadhi ya nchi za Afrika, kuwa ni dharura ya afya ya umma ya kimataifa.

Jamii inapaswa kufuata mwongozo wa wataalamu wa afya ili kujikinga na janga hilo ambalo halijapatiwa dawa, zaidi ya kinga.

WHO imezitaja nchi ambazo tayari zimeshaathiriwa na ugonjwa wa homa ya nyani, ikiwemo DRC Kongo na kueleza ugonjwa huo ni wa kuambukiza na tayari umeenea nchi jirani na zile za mbali na nchi hiyo, hivyo iwepo tahadhari ya kila mmoja kujikinga na kumkinga mwenzake.

Kwa mujibu wa shirika hilo, idadi ya ripoti za ugonjwa mwaka jana iliongezeka kwa kiasi kikubwa na tayari idadi ya walioripotiwa mwaka huu imezidi jumla ya mwaka jana, ambapo watu 15,600 walisajiliwa na watu 537 walifariki.

Licha ya taarifa iliyotolewa hivi karibuni kupitia Wizara ya Afya kueleza Tanzania ni salama, ni wajibu wa kila mmoja kuchukua tahadhari binafsi na kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya kwa kile kilichoelezwa kuwa miongoni mwa dalili zake ni upele, malengelenge mikononi na miguuni pamoja na kifuani.

Baadhi ya watu hupuuza maelekezo ya wataalamu wa afya, hasa yanapozuka majanga, ikiwemo milipuko ya magonjwa, hivyo kwa tahadhari ya homa ya nyani Serikali imetoa mwongozo kwa jamii, hasa kwenye mikusanyiko ya watu, lengo likiwa ni tahadhari.

Tanzania inasifika kimataifa kwa kuweza kukabiliana na majanga ya magonjwa mbalimbali, ukiwemo mlipiko wa Uviko-19 mwaka 2020 ambapo licha ya kuripotiwa vifo, iliweza kukabiliana nao bila kuweka katazo la watu kujifungia ndani kama ilivyokuwa kwa baadhi ya mataifa duniani.

Hii ni baada ya wananchi kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya, ikiwemo kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka mara kwa mara, kutumia vitakasa mikono, pia utaratibu wa kuvaa barakoa.

Mei 2022, WHO ilitoa takwimu za watu waliokufa kwa janga la corona, ambapo takribani watu milioni 15 walifariki kote duniani na hii ni kwa nchi ambazo zilikuwa zinarikodi vifo.

Wakati wa janga hilo Serikali kupitia kwa aliyekuwa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ilitoa mwongozo kwa wanafunzi shuleni na wasafiri wa vyombo vya umma pamoja na mikusanyiko ya watu kuvaa barakoa na kunawa mikono kwa maji tiririka na magari ya abiria kutakiwa kuwa na vitakasa mikono kwa abiria wao.

Uwepo wa homa ya nyani, jamii haitakiwi kupuuza ushauri wa wataalamu wa afya, kwa kuwa WHO imenukuliwa ikisema virusi vya clades1 vinavyosababisha ugonjwa huo, vinavyosambaa DRC vimejibadilisha na kuibuka vingine vya clade 1b, ambavyo kusababisha ugonjwa mkali zaidi.

WHO katika taarifa yake ya Julai mwaka huu, imesema kulikuwa na taarifa zaidi ya 100 zilizothibitishwa kimaabara kuwa ni za maambukizi ya virusi vya clade 1b, katika mataifa ya DRC ambayo hayajawahi kuripoti Mpox.

Kama awali nilivyotangulia kusema kuwa hakuna kitisho cha ugonjwa huo wa homa ya nyani nchini, bali iwepo tahadhari kwa jamii kujikinga kwa kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya na kuacha kupuuza taarifa zinazotolewa.

Serikali kupitia Wizara ya Afya ingelikuwa vyema ikatoa maelekezo kwa halmashauri nchini kwa kushirikiana na wataalamu wa afya hospitali za mkoa na wilaya kutoa semina kata kwa kata juu ya mambo ambayo yanachangia kupata maambukizi ya homa ya nyani na kutoa chanjo.

Uwepo wa utaratibu huo unaweza kutoa muitikio mkubwa kwa wananchi kupata tiba kinga, badala ya kusubiri kuripotiwa maambukizi na hili linawezekana ikiwa tu serikali pamoja na mambo mengine italivalia njuga.

Endapo utaratibu huo utafanyika, itakuwa ni fursa pia kwa wananchi kufanya vipimo mbalimbali vya magonjwa yasiyopewa kipaumbele duniani, ikiwemo matende, minyoo ya tumbo, usubi na kichocho pamoja na kupewa dawa kinga.

Serikali imekuwa ikitoa dawa kinga, hasa kwa wanafunzi shuleni, jambo ambalo ni zuri na la kuungwa mkono, ila ni vyema wakati wa kuelekea utoaji wa dawa kinga wazazi wa wanafunzi kupatiwa elimu kabla ili kufanikisha.

Ni vyema wazazi na walezi wa watoto kupatiwa elimu kabla ya kufanyika mazoezi ya upimaji wa afya na kupatiwa dawa kinga, kwani baadhi ya watu hawana uelewa mpana juu ya kinga za magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza.

Kuna haja ya kuwatumia watoa huduma ngazi ya jamii, kutoa ushauri kwa jamii inayowazunguka kuweka mazingira yao katika hali ya usafi, ili kuepukana na ugonjwa wa homa ya nyani.