CCM tayari ishapanga ushindi
Muktasari:
Hiyo maana yake nini? Kwamba CCM iko tayari kucheza faulo, kufanya ujanja na kujificha ili mwamuzi asione. Hili suala la mwamuzi kuona lina ukakasi kidogo, kwani kwa CCM hata mwamuzi akiona ataambiwa ajifanye kipofu, atie nta masikio yake na abadilishe matokeo
CCM tayari wameshapanga ushindi wa urais mwaka huu, fawahisha (waziwazi) wanasema kuwa watashinda hata kwa bao la mkono. Gazeti la Mwananchi limelidadavua “bao la mkono” kuwa ni lile goli lililofungwa kwa kuupiga mpira kwa mkono kinyume na taratibu za mpira, lakini hukubaliwa kwa kuwa mwamuzi anakuwa hajaona.
Hiyo maana yake nini? Kwamba CCM iko tayari kucheza faulo, kufanya ujanja na kujificha ili mwamuzi asione. Hili suala la mwamuzi kuona lina ukakasi kidogo, kwani kwa CCM hata mwamuzi akiona ataambiwa ajifanye kipofu, atie nta masikio yake na abadilishe matokeo. Hali hiyo inatokea kila mara katika ngazi zote za uchaguzi na bila shaka wapinzani wanalielewa hilo mpaka nao mara hii wanasema kuwa hakuna kulala wala kula, mpaka kieleweke.
Kwamba watayalinda masanduku ya kura kwa kucha na meno, mawakala watakaa vituoni mpaka matokeo yatangazwe na yabandikwe ubaoni/kutani. Kizuri ni kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye ameeleza mikakati ya chama hicho mapema, hivyo wapinzani wanapaswa waichukue kauli hiyo kama faida, wafahamu kwamba kuna mizengwe inaandaliwa, ni ya namna gani au ipi au itakuwa vipi, hiyo ni kazi yao kuibainisha.
Katika uchaguzi wa mwaka 2010, haikueleweka ni mbinu gani za ushindi zilitumiwa, bali watu wakabaki kulalamika na kudhani kuwa kuna ghushi katika karatasi za kupigia kura, eti ukiweka hapana baadaye inajibadilisha kuwa ndiyo.
Lakini vitendo vya kuondoka na masanduku ya kura na kwenda kuyachakachua hivyo ni maarufu na hata ule mtindo wa kumtisha msimamizi na kumpa maagizo kuwa ahakikishe kuwa mgombea fulani anashinda, nao ni mtindo maarufu.
Ingawa Nape amekanusha kuwa hajasema kama CCM itashinda hata kwa goli la mkono, hivyo, ila alikiri kuwa amesema watashinda hata kwa kidole. Swali la kujiuliza, je, ushindi wa kidole ni upi?
Hicho ni kitendawili kinachotaka mteguzi akitegue. Ni kwa mambo kama hayo ndiyo maana watu wenye mazingatio wanataka Tume Huru ya uchaguzi. Uhuru wa Tume unapatikana pale tu itakapokuwa haiteuliwi na serikali iliyopo madarakani wala haiwajibiki kwa serikali. Anayemlipa mpiga zumari ndiye anayechagua wimbo.
Inaonyesha kuwa slogani ya Uchaguzi Huru na wa Haki ni maneno tu ndiyo maana aliyekuwa Mwenyeketi wa Tume ya Uchaguzi ya Kenya mwaka 2007, Samwel Kivuitu, alifanya alichofanya. Na kama hicho alichotenda Kivuitu vilevile alikitenda aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar mwaka 1995, Zuberi Juma Mzee.
Kwanini ikawa rahisi kuyatenda waliyoyatenda? Kwa sababu hawakuwa huru, hivyo ndiyo kusema kuwa NEC na ZEC haziko huru. Kwa sababu watendaji wake wakuu wote wanateuliwa na rais. Je, vipi utaukata mkono unaokulisha? Jibu ni haiwezekani labda uwe tayari kufa na njaa.
Ni sababu hizo ndizo zilizowafanya wanamageuzi kutaka marekebisho ya Katiba yaingize kipengele cha kuwapo Tume Huru ya Uchaguzi.
Awali wadau hasa wa vyama vya upinzani walisema kuwa hawatashiriki uchaguzi wa mwaka huu kama kutakuwa hakuna tume Huru ya Uchaguzi. Kauli hiyo sasa hivi mwangi wake ni mdogo kwa sababu tayari wapinzani wameshatambua kuwa mbinu hiyo haifui dafu katika kuhakikisha mageuzi ya kisiasa yanatokea nchini.
Mara ya mwisho waliposusa ilikuwa wakati wa Bunge la Katiba, walitoka bungeni na kulichofuata sote tunakijua. Mapendekezo ya Katiba yakapita bila kuzingatia maoni ya wajumbe kutoka vyama vya upinzani.
Kauli hiyo ya goli la kidole na nyingine nyingi zitakazotoka inabidi zifuatiliwe kwa makini, kuna jambo nyuma yake. Ingawa ni vigumu kushindana na tembo ‘kukutuka’ lakini yawezekana kumdhibiti asisambaze kinyesi ovyo.
Ni mwandishi mwandamizi wa gazeti la Mwananchi. hshamte@tz.nationmedia.com