Bora mwanamke anayeng’aka kuliko wa ‘sawa mzee’

Niko natazama video mtandaoni, mara naona video moja ya Bunge la Afrika Kusini, mbunge mwanamke wa chama cha upinzani anasimama na kuomba muongozo kwa Spika wa Bunge, anamwambia, naomba mzungumzaji aliyepita afute moja ya maneno aliyoyasema kuhusu chama chetu kwa kuwa halikuwa la kiungwana.

Spika akatetea kwamba, neno lililotumika halikuwa na madhara yoyote na ni sahihi kutumika hasa bungeni.

Dada akawa analazimisha, spika anatetea, matokeo yake zogo likatokea, huyu anasema lile, huyu anasema hili.

Lakini baadaye wabunge walipotulia, yule mbunge akarudia tena kauli: “Naomba mzungumzaji aliyepita afute moja ya neno ambalo halikuwa la kiungwana alilolisema kuhusu chama chetu.” Na kwa mara nyingine, Spika akatetea akisema hilo neno halina shida yoyote kulitumia ndani ya Bunge.

Mbunge akauliza, una uhakika? Spika akajibu ndiyo. Mbunge akajibu “Sawa.” Kisha akanyamaza kwa sekunde mbili tatu, kisha sentensi yake iliyofuata akasema “Spika wa Bunge, wewe ni _______.” hapo kwenye deshi aliweka neno lile lile lililosemwa na mzungumzaji aliyepita.

Lakini ajabu baada ya mbunge huyu kulisema, spika akakasirika, akafura na kuanza kufoka kumwambia kwamba alifute neno hilo.

Mbunge akahoji kwa nini nilifute wakati umesema ni neno sahihi kutumika? Kwa nini iwe sahihi kwa mbunge wa chama chako kulitumia, lakini kwangu iwe shida.

Nilikuwa sitaki kuzungumzia siasa, na hata hii stori nimeisimulia kwa mrengo mwingine kabisa. Nimeisimulia kutokana na kitu nilichojifunza kwenye maisha kuhusu wanawake.

Wanaume huwa tunasema hatupendi mwanamke mwenye fujo, mwanamke anayeongeaongea sana, lakini ukweli ni kwamba, ni mara kumi kupata mwanamke mwenye fujo, mwanamke anayeongea, mkigombana hana stara, anaweza akapayuka hata mbele ya watu. Huyu akishamaliza kupayuka ndio amemaliza hana muda tena wa kuweka kinyongo wala kulala na kitu moyoni.

Mwanamke aliyemeza radio FM, na memori ya GB 123, ni mara kumi ya huyo kuliko kupata mwanamke ambaye, ukimkosea, akikuhoji, ukajitetea na akagundua utetezi wako hauna mashiko, anakujibu “sawa.”

Sawa ni jibu baya sana kutoka kwa mwanamke kuliko kukaripiwa na yeye. Na muda mwingine wala mwanamke anakuwa hana maana mbaya, pengine anasema sawa kwa sababu ameshakuelewa, au ameamua kupotezea kama unavyojua wanawake ni wastahimilivu sana.

Lakini jibu la sawa ni kama sumu, linakuua kimya kimya.

“Amesema sawa, ina maana amenisamehe au bado ana hasira na mimi. Kama amenisamehe mbona kirahisi sana, anapanga kufanya nini? Kama bado ana hasira na mimi atanifanyia kitu gani ili kulipiza au kujipoza?”

Yaani unaweza ukakaa na ‘stress’ siku nzima ukiwaza sawa yake ilikuwa ina maanisha nini. Na mara nyingi wanawake wakikujibu sawa, kuwa makini, kuna jambo linapikwa na wakiamua hawarudi nyuma.