Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Walichokisema Heche, Sugu, Lema na Boni Yai mkoani Geita

Muktasari:

  • Operesheni ya Katiba mpya ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) imeendelea mkoani Geita.

Dar/Geita. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, John Heche, amesema Watanzania wanaweza kuishi maisha mazuri ikiwa watapata viongozi kupitia mfumo unaoeleweka na wenye kuzingatia maslahi ya wananchi.

Mbali na Heche, wajumbe wa kamati kuu wao wamesema chama hicho kitaendelea kuwapigania wananchi huku wakiwaomba wawaunge mkono.

Viongozi hao wamesema hayo leo, Jumapili Mei 17, 2026, katika mkutano wa uzindizi wa Operesheni ya Katiba Mpya na “Free Tundu Lissu” uliofanyika viwanja vya Nyankumbu mkoani Geita.

Heche amesema Kanda ya Ziwa ilipaswa kuwa na vituo vikubwa vya utafiti wa teknolojia ya madini pamoja na viwanda vya kuongeza thamani ya madini hayo, hali ambayo ingeifanya Tanzania kuwa kivutio cha kimataifa.

Amesema msingi huo ungechangia upatikanaji wa ajira nyingi kwa wananchi, lakini cha kushangaza ni dhahabu inayozalishwa nchini hupelekwa nje bila kuongeza thamani hapa nchini akisema India ndiyo nchi inayoongoza kwa kuuza Tanzanite duniani, licha ya madini hayo kupatikana Tanzania pekee.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na maendeleo Chadema,akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Shule ya msingi Uwanja iliyopo kata ya Nyankumbu, Manispaa ya Geita.

Heche amesema kuwa mwaka 1978, China ilikuwa miongoni mwa nchi maskini, lakini ndani ya kipindi cha miaka 47 imepiga hatua kubwa kiuchumi na kuwa moja ya mataifa tajiri duniani, huku zaidi ya watu milioni 400 wakitoka kwenye umaskini.

Kwa upande wa Tanzania, amesema umaskini unaendelea kuongezeka kutokana na mifumo mibovu ya uongozi.

“Watanzania wanataka kufurahia maisha yao sasa, siyo kuendelea kuahidiwa maisha mazuri mbinguni pekee. Tunataka wananchi waanze kuona na kufaidi maisha mazuri hapa duniani, walale vizuri na waishi kwa hadhi,” amesema Heche.

Amewataka viongozi wa dini kuwaeleza wananchi ukweli kuhusu uwezo wa nchi kujenga uchumi imara, huku akisisitiza kuwa hawaungi mkono mfumo unaotegemea kuagiza karibu kila bidhaa kutoka nje ya nchi badala ya kuzalisha ndani.

Katika hatua nyingine, Heche amesema chama hicho hakitatishwa na vitisho vinavyotokana na kushikiliwa gerezani kwa Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu.

Amesisitiza kuwa wataendelea kudai kuachiwa kwake huru ili arejee kuongoza chama hicho.

“Tumekuwa tukitishwa ili tukae kimya, lakini hatutanyamaza. Tutaendelea kudai haki na tunachotaka ni Tundu Lissu aachiwe huru,” amesema.

Pia amesema Chadema inapanga kufanya maandamano nchi nzima kwa lengo la kushinikiza ajenda zao muhimu, ikiwamo upatikanaji wa Katiba mpya na kuachiwa huru kwa Tundu Lissu.

“Maandamano hayo yatakuwa makubwa na ya kihistoria, lakini yatafanyika kwa kufuata taratibu zote za kisheria. Lengo letu ni kudai Katiba mpya pamoja na kuachiwa huru kwa mwenyekiti wetu,” amesema.


Wenyeviti wa kada

Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi maarufu ‘Sugu’ amesema tatizo la Tanzania kushindwa kupiga hatua si mtu mmoja, bali ni mfumo mzima. Alisema ili kupata suluhu ya changamoto hizo, Watanzania wanapaswa kuungana kwa pamoja kuondoa mifumo mibaya.

Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa,Chadema Joseph Mbilinyi'Sugu' akihutubia wakazi wa Nyankumbu Manispaa ya Geita.

“Wafanyabiashara, watumishi, wakulima na makundi mengine tuwe kitu kimoja; itakuwa rahisi kuvuka katika mapito tunayopitia,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani, Boniface Jacob maarufu Boni Yai, amesema kuhusu yaliyotokea wakati na baada ya Oktoba 29, 2025, wanachohitaji ni uwajibikaji kwa kila aliyehusika.

“Ili nchi yetu iwe salama, ni lazima wote waliohusika wawajibishwe,” amesema.

Naye Mwenyekiti wa Kanda ya Magharibi, Dickson Matata amesema inasikitisha kuona wananchi wa Geita wanaendelea kuishi maisha magumu licha ya mkoa huo kubarikiwa kuwa na rasilimali nyingi za madini.

Wanachama wa Chama cha Demokrasia na maendeleo Chadema, toka kata ya Nyankumbu Manispaa ya Geita,wakiskiliza viongozi wa Chama hicho leo.

“Katika maeneo mengi, hata huduma ya maji safi na salama hakuna. Yote haya yanatokea kwa sababu wananchi mmeamua kuwaacha viongozi wasiokuwa na nia njema; mmekuwa wema kupita kiasi na mnakaa kimya,” amesema.

Matata amesema umefika wakati kwa wananchi kuamka na kufanya mabadiliko ya kweli ili waweze kunufaika na utajiri waliobarikiwa na Mwenyezi Mungu.

Mjumbe wa Kamati Kuu na mlezi wa kanda ya kati, Godbless Lema, amesema dhambi kubwa duniani ni uoga, akisisitiza kwamba binadamu hudumu milele kupitia alama na mchango anaouacha katika jamii.