Vigogo Chadema watua Kigoma uzinduzi ‘Operesheni +255 Katiba Mpya’

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema

Muktasari:

  • Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kesho Jumatano Mei 17, 2023 kitafanya uzinduzi wa Operesheni +255 Katiba mpya, mkoani Kigoma kisha utaendelea majimbo, mikoa, wilaya na kata zote nchi nzima.

Mwanza. Mashambulizi yameanza. Hivyo ndivyo mtu anavyoweza kuelezea jinsi magari ya matangazo yenye spika zenye sauti kubwa yanavyopishana katika mitaa ya mji wa Kigoma kutangaza uzinduzi wa ‘Operesheni +255 Katiba Mpya’ ya Chadema itakayofanyika mkoani humo kesho Jumatano ya Mei 17, 2023.

Mkutano huo Chadema utafanyika katika uwanja vya Mwanga ulioko katikati ya mji wa Kigoma ambapo baada ya uzinduzi, viongozi wa chama watagawanyika katika timu mbili ikiwemo ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Makamu Mwenyekiti wa Chadema-bara, Tundu Lissu.

Mwananchi ilishuhudia magari matatu ya matangazo yaliyonakshiwa rangi ya bendera ya Chadema na maandishi yanayosomeka "+255 Katiba Mpya" yakipita katika mitaa ya mji wa Kigoma kuhamasisha wananchi kujitokeza katika mkutano huo.

Akizungumza na Mwananchi baada ya kutembelea uwanja wa Mwanga utakapofanyika uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema baada ya uzinduzi huo viongozi watafanya mikutano katika majimbo yote ya mkoa wa Kigoma.

Alisema hadi kufikia jana Jumatatu Mei 15, 2023, baadhi ya viongozi wa juu wa Chadema walikuwa wamewasili mkoani humo aliwemo Naibu Katibu Mkuu-Bara, Benson Kigaila na Naibu Katibu Mkuu-Zanzibar, Salum Mwalimu, viongozi wa Bawacha akiwemo kaimu mwenyekiti wake, Sharifa Sulleiman na viongozi waandamizi.

"Mpaka sasa mapokeo ya watu ni makubwa, watu wamekuwa na shauku sana na Chadema wanasema tutakuwepo, imetupa nguvu kuwa ujio wa Chadema Kigoma utaleta mageuzi makubwa," amesema Mrema

Amesema operesheni hiyo imeanzia mahsusi katika mji huo kisha itasambaa katika majimbo mengine ikiwemo Buyungu, Muhambwe, Buhigwe, Kigoma Kaskazini, Kasulu, Kasulu Vijijini kabla ya kusambaa katika majimbo, mikoa, wilaya na kata zote za Tanzania.

"Mwenyekiti (Mbowe) na Makamu Mwenyekiti (Lissu) watagawana majimbo, watakuwa wakihutubia huko njiani na kufanya mikutano mikubwa majimboni baada ya hapo tutaacha timu itakayozunguka kwenye kata zote za mkoa wa Kigoma kwa siku zisizopungua 30," amesema

Amesema pperesheni hiyo ni maandalizi kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa 2024, na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 huku akidai chama kinatarajia kutumia Helkopta maalum kuzunguka katika maeneo mbalimbali.

"Nzi ataruka kwa mara ya kwanza baada ya miaka saba ya ukimya! Kuna sababu mahsusi za kuleta uzinduzi huu Kigoma, zitaelezwa na Mwenyekiti wa chama siku hiyo. Lakini tunachoweza kusema ni sasa hivi tuko kwenye uchaguzi ndani ya chama kabla ya kwenda kwenye uchaguzi mkuu ujao hivyo tunatakiwa tujipange vizuri," amesema

"Tumesema bila Katiba Mpya hatutashiriki uchaguzi lakini haimaanishi tusijiandae na siku zote ukitaka kuhakikisha kushinda uchaguzi lazima ujiandae, jeshini huwa wanasema ukitaka kupigana vita na usimwage damu nyingi kabla ya vita lazima uandae majeshi vizuri. Tumeanza kujipanga," amesisitiza

Kiongozi huyo amesema viongozi wa chama wameaga katika familia zao kwa ajili ya kufanya Operesheni hiyo itakayodumu hadi Agosti 2024 huku akiwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika uzinduzi wa Operesheni hiyo katika maeneo yao.

Mkazi wa Ujiji mkoani Kigoma, Malaki John ameeleza kufurahishwa na kurejea kwa mikutano ya hadhara huku akisema ni jukwaa kwa vyama vya siasa kunadi sera zao kwa wananchi.

"Tumesikia matangazo mengi yakipita mitaani, tunaamini siku hiyo tutafika eneo la Mwanga kuwasikiliza wanataka kutuambia kitu gani," amesema John

Naye, Husna Ally amesema anaamini uzinduzi wa operesheni hiyo ni ujio mpya wa upinzani nchini ambao ulififishwa kwa zaidi ya miaka saba baada ya mikutano ya hadhara kuzuiwa.