Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ushiriki wa Marekani utamaliza vita DRC?

Muktasari:

  • Mjadala umeibuka kuhusu ushirikiano wa kimkakati kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Marekani katika sekta ya madini muhimu.

Dar es Salaam. Tangu mwanzoni mwa 2025 kumekuwa na mjadala kuhusu uwezekano wa ushirikiano wa kimkakati kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Marekani katika sekta ya madini muhimu.

DRC, Taifa lenye utajiri wa rasilimali kama kobati, lithium, urani, shaba, dhahabu na madini mengine adimu, imekuwa ikitafuta washirika wa kimataifa kuwekeza katika sekta ya madini kwa maendeleo yake ya kiuchumi.

Mazungumzo kati ya Marekani, ambayo pia inajadili mkataba wa madini na Ukraine yamekuwa mjadala jijini Kinshasa, DRC kwa wiki kadhaa.

“Marekani iko tayari kujadili ushirikiano katika sekta hii kwa mujibu wa ajenda ya kipaumbele kwa Marekani katika utawala wa Trump (Donald, Rais wa Marekani)” amesema msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.

Amesema DRC ina sehemu muhimu ya akiba ya madini adimu duniani yanayohitajika katika teknolojia za kisasa.

Amesema Taifa hilo kubwa duniani limekuwa likifanya kazi kuhamasisha uwekezaji wa sekta binafsi ya Marekani nchini DRC ili kuendeleza rasilimali za madini kwa njia uwajibikaji na uwazi.

Marekani ikitafuta mbinu za kupunguza utegemezi wa China katika upatikanaji wa madini yanayotumika kwenye teknolojia za kisasa, uwezekano wa makubaliano kati ya mataifa hayo mawili umekuwa mjadala mpana.


Asili ya mazungumzo ya ushirikiano

Pierre Kalambayi, Mwenyekiti wa Kamati ya Seneti ya DRC inayoshughulikia ulinzi, usalama na ulinzi wa mipaka, Februari 21, 2025 kupitia mwakilishi wake, alituma barua kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio na maofisa wengine wa Marekani, akialika uwekezaji wa Marekani katika rasilimali za madini za DRC ili kusaidia kuimarisha ‘utulivu wa kikanda.’

Pendekezo hilo linahusishwa na Marekani kuwekeza katika madini ya DRC, huku ikisaidia kuimarisha usalama wa Taifa hilo, hasa katika vita dhidi ya waasi wa M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda.

Japokuwa Rwanda mara kadhaa imekuwa ikikanusha kuliunga mkono kundi hilo.

Hata hivyo, maofisa wawili wa DRC walibainisha kuwa mpango huo haukuidhinishwa na Serikali Kuu au Rais wa Taifa hilo.

Ingawa kuna mipango kadhaa inayoendelea, bado iko katika hatua za awali. Kwa sasa, hakuna kampuni kubwa ya madini ya Marekani inayofanya kazi DRC, huku sekta ya madini ya Taifa hilo ikitawaliwa na kampuni za China.

Licha ya changamoto hizo, Marekani imeonyesha nia ya kushirikiana na DRC katika sekta ya madini muhimu, ikilenga kukuza maendeleo ya uwajibikaji na uwazi ya rasilimali za madini za DRC, sambamba na ajenda ya ‘Marekani Kwanza’ ya utawala wa Trump.

Vyanzo kutoka Ikulu ya DRC, Wizara ya Madini ya nchi hiyo na maofisa wa Marekani vililiambia Shirika la Habari la Reuters kuwa, kuna juhudi kadhaa zinaendelea, ingawa ziko katika hatua za awali.

Inaelezwa ujumbe wa DRC ulipangwa kukutana na Kamati ya Mambo ya Nje ya Baraza la Wawakilishi la Marekani Machi 6, lakini mkutano uliahirishwa.

“Nadhani jambo hili bila shaka litaamsha hamasa Marekani na tayari limevuta hisia,” alisema Jason Stearns, mtaalamu wa masuala ya DRC kutoka Chuo Kikuu cha Simon Fraser, Canada.


Je, kuna faida DRC itapata?

DRC inajulikana kama moja ya nchi zenye utajiri mkubwa wa rasilimali asilia, lakini imekumbwa na changamoto za kiuchumi na migogoro ya kisiasa kwa miongo kadhaa.

Kwa Marekani kuwekeza katika madini ya DRC kunaweza kusaidia kuongeza mapato ya Serikali kupitia kodi na mirabaha ya madini, kutengeneza nafasi za ajira na kuimarisha miundombinu ya uzalishaji.

China inadhibiti sehemu kubwa ya mnyororo wa ugavi wa madini muhimu yanayotumika katika teknolojia za kisasa, ikiwa ni pamoja na betri za magari ya umeme na vifaa vya elektroniki.

Kwa sababu hiyo, ushirikiano na DRC unaweza kuwa fursa kwa Marekani kupata madini hayo moja kwa moja kutoka Afrika, hivyo kupunguza udhibiti wa China katika sekta hiyo.

Eneo la Maziwa Makuu limekumbwa na migogoro ya muda mrefu, hasa mashariki mwa DRC, ambako waasi wa M23 wamekuwa wakifanya mashambulizi.

Iwapo Marekani itawekeza katika jeshi la DRC kupitia mafunzo na vifaa vya kijeshi, kuna uwezekano wa kupunguza athari za waasi hao na kurejesha utulivu eneo hilo.

Hata hivyo, hali hiyo haitamaliza migogoro ya kisiasa iliyopo sasa.


Uwezekano wa kuibuka migogoro ya kisiasa

Mazungumzo hayo yamezua sintofahamu katika siasa za ndani ya DRC.

Maofisa kutoka chama cha rais wa zamani wa DRC, Joseph Kabila, waliitwa kufika mbele ya mwendesha mashitaka wa kijeshi Jumatatu Machi 10, jambo linaloashiria mvutano wa kisiasa kutokana na hatua za waasi kusonga mbele mashariki mwa nchi hiyo.

Sababu halisi ya mwaliko huo haikufahamika wazi, alisema Jean Mbuyu, wakili wa maofisa hao na aliyewahi kuwa mshauri wa usalama wa Kabila. Hali hii inaashiria mivutano inayotokana na mgogoro wa M23 na ushirikiano mpya unaoweza kuibuka kati ya DRC na Marekani.

Baadhi ya viongozi wa upinzani wanahisi makubaliano hayo yanaweza kutumiwa vibaya kwa masilahi ya kisiasa badala ya kuleta maendeleo kwa taifa.

Kwa upande mwingine, China imewekeza mabilioni ya Dola katika sekta ya madini nchini DRC na ina mikataba mikubwa ya uchimbaji madini na serikali ya taifa hilo.

Endapo Marekani itaingia katika soko la madini la DRC, kuna uwezekano wa kushuhudia mvutano wa kidiplomasia kati ya China na Marekani, jambo linaloweza kuwa na athari kwa uchumi wa DRC na uhusiano wake kimataifa.

Ingawa msaada wa kijeshi kutoka Marekani unaweza kusaidia kupambana na waasi wa M23, historia imeonyesha msaada wa kijeshi pekee hauwezi kumaliza mizizi ya migogoro inayotokana na sababu za kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Pia, ushirikiano huo unaleta maswali kuhusu mustakabali wa siasa na uchumi wa eneo zima la Afrika Mashariki na Kati.

Endapo Marekani itawekeza katika madini ya DRC na kusaidia kurejesha utulivu eneo hilo, nchi jirani kama Uganda, Burundi na Tanzania zinaweza kupata faida za moja kwa moja kupitia biashara na usafirishaji wa madini hayo kwenda nje ya Bara la Afrika.

Hata hivyo, ikiwa makubaliano hayo yatasababisha kuzorota kwa uhusiano kati ya DRC na China, kutakuwa na athari kwa biashara za kimataifa na uwekezaji unaoendelea katika sekta ya madini.

Zaidi ya hayo, uhusiano kati ya DRC na Rwanda unaweza kuingia katika hatua ngumu zaidi ikiwa Marekani itaamua kuiunga mkono DRC kwa misingi ya kijeshi.


Matarajio ya Marekani

Marekani inaona hilo kama fursa ya kupambana na utawala wa China katika sekta ya uchimbaji madini ya nchi hiyo.

“Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inashikilia sehemu muhimu ya madini ya dunia yanayohitajika kwa teknolojia za kisasa. Marekani iko tayari kujadili ushirikiano katika sekta hii unaoendana na mpango wa ‘America First’ wa utawala wa (Donald) Trump,” alisema msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani katika mahojiano na gazeti Financial Times.

Machi 8, 2025 Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ililithibitishia Shirika la Habari la Reuters nia yake ya kuingia katika mkataba wa madini muhimu, ikibainisha kuwa DRC ina sehemu kubwa ya madini muhimu ya dunia yanayohitajika kwa ajili ya teknolojia za kisasa.

Jeshi la DRC kwa sasa linapigana na kundi la waasi la M23 mashariki mwa nchi hiyo. Serikali inadai kuwa waasi wakisaidiwa na Rwanda, wameteka maeneo ya uchimbaji madini katika eneo hilo na kuvuna madini yenye thamani.

Rwanda imekana mara kadhaa kuhusika katika eneo hilo, lakini Umoja wa Mataifa na Marekani wanasema inaliunga mkono vuguvugu la uasi na kuhamasisha uchimbaji wa madini.

Rais wa DRC, Felix Tshisekedi, hivi karibuni aliiomba Serikali ya Trump kutafakari kuhusu mkataba wa haki na nchi yake yenye rasilimali nyingi.

“DRC inavutiwa na ushiriki wa Marekani katika eneo la mashariki kama njia ya kumaliza mapigano,” alisema waziri wa habari wa nchi hiyo katika mahojiano na tovuti ya habari ya ‘Semafor’ mwishoni mwa juma.