Prime
UCHAMBUZI WA MJEMA: Tusitatue matatizo ya uchaguzi kwa kujifanya hayapo

Baba wa Taifa, mwalimu Jullius Nyerere (1922-1999), aliwahi kusema hatuwezi kutatua matatizo yetu kwa kujidanganya hayapo, nami nasema tusitatue changamoto za mifumo ya uchaguzi kwa kujidanganya inatenda haki kwa wote.
Ni kwa msingi huo huo, tumeamua kutatua kilio cha muda mrefu cha kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi kwa kubadilisha jina na kuremba vipengele vya kuwapata wajumbe wa Tume, lakini kiuhalisia dosari za Tume ziko pale pale.
Tulichokifanya kubadili jina kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kuwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) haina tofauti na kuchukua soda ya Cocacola na kuiweka kwenye chupa ya Fanta na kumwaminisha mteja kuwa hiyo ni Fanta.
Tunayasema haya kwa nia nzuri kabisa na kwa uzalendo mkubwa kwa nchi yetu kwa sababu kati ya mambo ambayo yanatajwa kuwa kiini cha machafuko katika baadhi ya nchi duniani, ni uchaguzi kutokuwa huru, haki na unaoaminika.
Sote tunakubaliana kuwa Katiba ndio sheria mama, kama Katiba ikiwa mbovu basi itazaa sheria na kanuni mbovu na hiki ndicho tunachokishuhudia hapa Tanzania, kupitia Ibara ya 74 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977.
Ibara ya 74(12) ya Katiba inasema na hapa nanukuu “Hakuna mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza jambo lolote lililotendwa na Tume ya Uchaguzi katika kutekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii”.
Ibara hii ndogo ndio mchawi wetu kwa haya tunayoyashuhudia katika chaguzi zetu kwa sababu ni kichekesho cha karne kwamba Tume ambayo inapaswa kutenda haki, bila upendeleo wala ubaguzi, inawekewa kinga ya kutoshitakiwa kortini.
Maana yake ni kwamba hata Tume ikiamua kuboronga kwa makusudi na kwa utashi wake ikaamua kumtangaza mgombea kiti cha urais kuwa ameshinda ilihali hakushinda au mgombea ubunge au Udiwani basi hakuna wa kuihoji.
Tunaweka ibara hii wakati Katiba yetu hii hii Ibara ya 107A (1) inasema mamlaka ya utoaji haki hapa nchini itakuwa mikononi mwa Mahakama na hakuna chombo cha Serikali wala cha Bunge kitakachokuwa na kauli ya mwisho katika utoaji haki.
Sasa unajiuliza, hivi INEC sio chombo cha Serikali kwa muonekano wake? Kama tunasema Mahakama ndicho chombo chenye kauli ya mwisho katika utoaji haki, kwanini mwananchi haruhusiwi kuhoji pale chombo hiki kinapoboronga?
Ninafahamu uwepo wa kifungu cha 6(2) cha sheria ya INEC ya 2024 kinachosema Tume inaweza kushtaki au kushtakiwa na endapo imeshtaki au kushtakiwa, itapaswa kumtaarifu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili awe sehemu ya shauri.
Wanasheria wa masuala ya Katiba (constitutional lawyers), watuambie tangu lini sheria ikawa juu ya Katiba kama sio changa la macho tumepigwa? Hivi ni kweli wasomi wetu hawaelewi maana ya ukuu wa Katiba au Constitution Supremacy?
Ukuu wa Katiba unatamkwa katika kesi maarufu ya India ya Indira Nehru Ganghi dhidi ya Raj Narain (1976) inayopatikana kwenye andiko la Mirza Hameedullah Beg (Supremacy of the Constitution: Trends and issues) katika ukurasa wa 114.
Wanasema uhalali wa tendo lolote la serikali au mamlaka lazima lipimwe kwa kuangalia kama linaendana na matakwa ya Katiba na usiwepo mhimili wowote, iwe serikali, mahakama au bunge utakaotenda nje ya masharti ya Katiba yao.
Kama nilivyotangulia kusema, ukishakuwa na vifungu vibaya vya Katiba,mizizi yake inakwenda hadi chini na ndio maana Kanuni za Uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Novemba 27,2024 ulibeba maudhui ya ibara hiyo ya 74.
Mathalan, kifungu cha 49 cha kanuni hizo kinazuia msimamizi wa uchaguzi, msimamizi msaidizi wa uchaguzi, msimamizi wa uchaguzi au ofisa yoyote wa Serikali aliyehusika na uchaguzi huo kutowajibika kwa jinai au madai.
Kanuni hizo zilienda mbali na kuzuia maofisa hao kuchukuliwa hatua za kinidhamu au kiutawala kwa jambo lolote alilolifanya au kuacha kufanya kwa nia njema wakati wa kutekeleza majukumu yake, unajiuliza nia njema inapimwaje?
Sasa unajiuliza, hivi chombo cha kusimamia uchaguzi wa haki kinawekewaje kinga ya kutoshitakiwa kama kweli kinatekeleza majukumu yake kwa weledi na maadili? Waswahili wana usemi fumbo mfumbie mjinga lakini mwerevu ataelewa.
Kinga hii waliyowekewa Tume na watendaji wake ni sawa na tuone Jaji au Hakimu ambaye wajibu wake mkubwa ni kutenda haki kama ilivyo INEC, awekewe kinga, unajiuliza hivi anawekewa kinga ili afanye nini kibaya cha kunyima mtu haki?
Ni kutokana na kinga hizi zisizo za haki ndio maana tunashuhudia mamlaka makubwa waliyonayo wasimamizi wa uchaguzi na wasaidizi wao kuengua wagombea hasa wa upinzani kwa visababu vidogo vidogo visivyo na mashiko.
Katiba yetu ya Tanzania na sheria za uchaguzi, zimeweka sifa ya mtu kuchaguliwa kuwa Rais, mbunge au Diwani na mojawapo ni lazima awe raia wa Tanzania, ametimiza umri wa miaka 21 na ajue kusoma na kuandika Kiswahili au Kiingereza.
Sifa nyingine ni kuwa awe ni mwanachama na ni mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa, katika kipindi cha miaka mitano kabla ya tarehe ya Uchaguzi hakuwahi kutiwa hatiani katika mahakama kwa kosa lolote la kukwepa kodi.
Kwa hiyo tulitarajia mgombea ataenguliwa kugombea kwa kuegemea vigezo hivyo vya kikatiba pamoja na mgombea aenguliwe tu kama hana sifa hizo au amethibitishwa kuwa na ugonjwa wa akili, lakini sio haya tunayoshuhudia.
Mgombea anaenguliwa eti amekosea kujaza tarehe ya kuzaliwa au chama cha siasa ama eneo analoishi, lakini unakuta alijaza vizuri kabisa fomu yake na kuikabidhi kwa msimamizi, lakini inapobandikwa imeongezwa vitu vya ajabu.
Unakuta aliandika alizaliwa tarehe 15.10.1972 anakuta fomu imeongezwa inasomeka mwaka 19720 au mwezi unasomeka 101 au jina la aeneo alilotoka limeongezwa maneno, anawekewa pingamizi kisha anaenguliwa kugombea.
Ukifuatilia vizuri dosari hizi baadhi zimefanyika ndani ya ofisi za msimamizi au msimamizi msaidizi kwa malengo mahsusi ya kumtengenezea mgombea sababu ya kuenguliwa, halafu msimamizi anayefanya haya yote anawekewa kinga.
Ili kuondokana na huu uhuni wa baadhi ya wasimamizi, ni kuhakikisha sifa zile za kikatiba za mtu kugombea ndizo zinasimama, haya makosa mengine madogo madogo tena mengine ni ajali za kutengeneza,mtu apewe fursa ya kuyarekebisha.
Tuna matatizo mengine katika mfumo wetu wa uchaguzi nayo ni kuwazuia mawakala kutekeleza majukumu yao kwa uhuru na katika uchaguzi mkuu 2020 tuliona namna mawakala walivyotolewa vituoni kwa mtutu wa bunduki.
Tuliona, na hata katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024, mawakala walifanyiwa mizengwe ya kupewa barua za utambulisho na wasimamizi au wasimamizi wasaidizi na kuruhusiwa kuingia vituoni kura zilishaanza kupigwa muda mrefu.
Kuna tatizo lingine la vyombo vya Dola hasa Jeshi la Polisi, kuingilia chaguzi kwa maslahi ya chama tawala, baadhi ya polisi kutumika kuhujumu chaguzi za haki na mengine ya aina hiyo, na yote haya ndio yanaleta haja ya mabadiliko.
Hivi kwa akili ya kawaida kabisa, mwenyekiti wa Tume, Makamu wake na makamishina wa Tume wameteuliwa na Rais, na Rais huyo naye ni mgombea katika uchaguzi unaosimamiwa na wateule wake, watatenda haki?
Unakuwa na refa mchezaji halafu utegemee akutendee haki wewe mpinzani? Katika nchi zote zenye Tume Huru ya Uchaguzi ya kweli na chaguzi ni za kidemokrasia, hakuna mgombea wa urais anayeweza kushinda kwa asilimia 90.
Kuna hoja dhaifu sana inazungumzwa na wanaotetea muundo wa sasa kuwa hata nchi nyingine ni hivyo hivyo, nataka niwaambie kuwa katika nchi zenye Tume Huru ya Uchaguzi, upatikanaji wa mwenyekiti wa wajumbe ni mbingu na ardhi.
Taifa letu lisione soni kwenda kuangalia Tume Huru za Uchaguzi katika nchi za Ghana, Afrika Kusini, Namibia, Botswana, Namibia na Mauritius zinavyopatikana, zinavyofanya kazi, sheria zao za uchaguzi zikoje na uadilifu wa watumishi wa tume.
Kama nilivyotangulia kumnukuu baba wa Taifa kuwa hatuwezi kutatua matatizo yetu kwa kujidanganya hayapo, tutalitumbukiza taifa letu kwenye machafuko pale kundi linaloona linakandamizwa, litakapoamua kutumia njia za msituni kudai haki.
Kwa mtanzania yeyote anayejitambua, na aliyeona yaliyotokea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019 na 2024 na uchaguzi mkuu 2020, atakubaliana na mimi kama taifa tuna tatizo, ambalo tunalitatua kwa kujidanganya halipo.
Kupanga ni kuchagua, haya tunaweza kuyaepusha mapema kama tutahubiri haki kabla ya amani na kuhakikisha hatutungi sheria kwa kuangalia namna ya kukibakiza chama tawala madarakani, bali kuangalia maslahi ya wapiga kura.
0656600900