Uandikishaji, uboreshaji daftari la kudumu unavyozidi kuchanja mbuga

Wananchi wakiwa katika foleni ya uandikishaji Jimbo la Chambani Pemba. Picha na Salim Hamad
Muktasari:
- Tayari baadhi ya mikoa imeshakamilisha uboreshaji na mingine inaendelea.
Pemba/Pwani. Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga Kura unaendelea kulingana na ratiba iliyotolewa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC). Tayari baadhi ya mikoa imeshakamilisha kazi hiyo, huku mingine ikiendelea na mchakato.
Katika Mkoa wa Pwani, inakadiriwa kuwa zaidi ya Sh100 milioni zitatumika kuwalipa maofisa waandikishaji 131 watakaofanya kazi hiyo ndani ya Halmashauri ya Mji wa Kibaha.
Kazi hiyo inatarajiwa kuanza rasmi kesho, Alhamisi Februari 13, 2025, itaendelea hadi Februari 19, 2025.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo kwa maofisa hao leo Jumatano, Februari 12, 2025, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Dk Rogers Shemwelekw amesema maandalizi ya kutosha yamefanyika ili kuhakikisha kazi hiyo linaendeshwa kwa ufanisi bila changamoto.

"Hatutaki malalamiko, hasa kuhusu malipo. Kiasi cha malipo yenu kimeelezwa wazi na iwapo kuna yeyote atalipwa pungufu, anipigie simu moja kwa moja," amesema Dk Shemwelekwa.
Amesisitiza kuwa kazi hiyo ni ya kitaifa, hivyo maofisa waandikishaji wanapaswa kuitekeleza kwa umakini mkubwa ili kuepuka matatizo ya kisheria.
"Zingatieni viapo vyenu, tumieni lugha nzuri kwa wananchi ili kuwe na mazingira mazuri ya ushirikiano, na hakikisheni kuwa hakuna upendeleo wa aina yoyote," ameongeza.
Aidha, amewaonya maofisa hao kuepuka vitendo vyovyote vinavyokwenda kinyume na sheria, huku akiwataka kufuata miongozo waliyopewa ili zoezi likamilike kwa ufanisi na kwa wakati muafaka.
Kwa upande wake, mmoja wa maofisa waandikishaji, Yaled Salanje amesema ingawa hii ni mara yake ya kwanza kushiriki katika kazi hiyo, mafunzo aliyopata yamempa mwongozo wa kutosha ili kuifanya kwa ufanisi.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Mkoa wa Pwani Dk Rogers Shemwelekwa akifunga mafunzo kwa waandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura. Picha na Sanjito Msafiri
“Natoa wito kwa wakazi wa Kibaha wajitokeze kuboresha taarifa zao ili wawe na haki ya kupiga kura wakati utakapowadia," amesema Salanje.
Nao baadhi ya wananchi, akiwamo Naomi Samson, amesema changamoto wanayokumbana nayo ni ucheleweshwaji wa mchakato wa uandikishaji.
"Waandikishaji wanapaswa kuzingatia muda ili kuepusha usumbufu kwa wananchi ambao wana shughuli nyingine za kufanya," amesema.
Changamoto Kisiwani Pemba
Wakati uboreshaji wa daftari ukiendelea, baadhi ya wananchi Kisiwani Pemba wamelalamikia kutoyaona majina yao kwenye vituo walivyotarajia.
Hata hivyo, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imewataka mawakala na wasimamizi wa vituo hivyo kuwaelekeza wananchi namna ya kuangalia majina yao katika vituo vingine ili kuepusha sintofahamu.
Kamishna wa ZEC, Idrisa Haji Jecha, alipokuwa akitembelea vituo vya uandikishaji Kisiwani Pemba leo Jumatano, Februari 12, 2025, amesema wakati mwingine taarifa za mpiga kura zinaweza kusajiliwa kwenye kituo kingine tofauti na kile alichotarajia.
"Nawasihi mawakala na wasimamizi wa vituo kuwaelekeza wananchi ipasavyo ili waweze kupata majina yao bila usumbufu. Hatutaki kusikia kuwa mtu mwenye sifa ameshindwa kuandikishwa kwa sababu ya uzembe," amesema Jecha.
Mkazi wa eneo la Mkoani, Hawadh Juma, amethibitisha kuwa alikosa jina lake katika kituo alichokwenda awali, lakini baada ya kupewa maelekezo sahihi alikipata kwenye kituo kingine.
Katika hatua nyingine, Kamishna Jecha aliwataka mawakala wa vyama vya siasa kuhakikisha wanatunza kumbukumbu sahihi na kutoa taarifa za kweli ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima.
"Mawakala wanapaswa kuwa waangalifu wanapohifadhi taarifa na kuzifikisha kwa viongozi wao, kwani usahihi wa taarifa hizo utasaidia kuhakikisha mchakato wa uandikishaji unafanyika bila matatizo," amesema.
Masheha na wasimamizi wa vituo wameombwa kuendelea kuwahamasisha wananchi kushiriki katika uandikishaji ili kuhakikisha wanapata haki yao ya kikatiba.
Juma Hamad Abdalla na Rashid Salum, wakuu wa vituo vya uandikishaji Wilaya ya Chakechake, wamesisitiza kuwa watazingatia maelekezo ya tume ili kuhakikisha zoezi linaendeshwa kwa uwazi na kwa mujibu wa kanuni.
Kwa upande wake, Khamis Abdalla Salim, wakala wa ACT-Wazalendo, amesema mpaka sasa uandikishaji unaendelea vyema na hakuna mwanachama wao aliyekosa haki yake ya kujiandikisha.
Kauli kama hiyo pia ilitolewa na Saleh Daudi Saleh, wakala wa NRA, ambaye amesisitiza kuwa wataendelea kushirikiana na wahusika ili kufanikisha zoezi hilo kwa ufanisi.