Sarakasi za uchaguzi mkuu Sudan Kusini kuhitimishwa Desemba
Muktasari:
- Uchaguzi huo uliotakiwa kufanyika tangu mwaka 2022, unatarajiwa mara hii licha ya nchi hiyo kuwa ukingoni mwa vita vya wenyewe kwa wenyewe kutokana na mivutano kati ya Rais Salva Kiir na Makamu wake Riek Machar.
Juba. Tume ya Uchaguzi nchini Sudan Kusini imetangaza rasmi kuwa uchaguzi mkuu wa Rais na wabunge unaosubiriwa kwa hamu, ambapo utafanyika Desemba 22, 2026.
Hatua hii inakuja baada ya shughuli hiyo kukwama na kuahirishwa mara kadhaa tangu nchi hiyo ipate uhuru mwaka 2011.
Hata hivyo, tangazo hilo limepokewa kwa hisia tofauti na tahadhari kubwa, huku kukiwa na hofu ya nchi hiyo kutumbukia tena kwenye mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.
Kwa mujibu wa RFI, waangalizi wa kimataifa wameonya kuwa mzozo unaoendelea kufukuta chini kwa chini kati ya vikosi vya Serikali na vile vya upinzani unaweza kuvuruga mchakato huo.
Hali ya kisiasa na kiusalama nchini humo imezidi kuwa tete huku mkataba wa amani wa mwaka 2018 uliotakiwa kuhitimisha uhasama kati ya Rais Salva Kiir na hasimu wake wa kisiasa, Makamu wa Rais Riek Machar, ukionekana kusuasua kwa kiasi kikubwa katika utekelezaji wake.
Matokeo yake, taifa hilo changa zaidi barani Afrika limebaki kwenye lindi la umasikini uliokithiri na malalamiko ya ufisadi wa kiwango cha juu.
Kulingana na makubaliano ya awali ya mchakato huo wa amani, Sudan Kusini ilipaswa kufanya uchaguzi mkuu tangu mwaka 2022. Hata hivyo, kutokana na changamoto za kiusafirishaji na kiusalama, ulisogezwa mbele hadi mwaka 2024, kabla ya kuahirishwa tena hadi mwishoni mwa mwaka huu wa 2026.
Licha ya kuweka hadharani tarehe hiyo ya Desemba 22, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi nchini humo, Abednego Akok Kacuol, ameweka wazi kuwa bado kuna milima mirefu ya kisheria na kisiasa inayopaswa kuvukwa ili kufanikisha azma hiyo.
Akok amebainisha kuwa vipengele kadhaa vya mkataba wa amani, ambavyo ni nguzo kuu ya kuwepo kwa uchaguzi huru na wa haki, bado havijatekelezwa kikamilifu.
Kikwazo kingine kikubwa kinachotishia kuwepo kwa uchaguzi huo ni uhaba mkubwa wa rasilimali fedha na miundombinu ya kiusalama.
Mwenyekiti huyo amefichua kuwa hadi sasa tume yake imepokea kiasi cha dola milioni 21 tu za Kimarekani, kati ya dola milioni 250 zinazohitajika ili kuendesha zoezi hilo nchi nzima.
Wachambuzi wa siasa za kikanda wanasema kuwa bila kupatikana kwa fedha hizo na bila kuwepo kwa maridhiano ya dhati ya kiusalama kati ya Salva Kiir na Riek Machar, tarehe hiyo inaweza kuwa ndoto nyingine inayoelea hewani kwa wananchi wa Sudan Kusini ambao wana kiu ya kuichagua Serikali wanayoitaka.