Othman aahidi kukomesha ufisadi, ukahaba Zanzibar
Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman akihutubia mkutano wa hadhara wa kunadi sera zake uliofanyika Makunduchi
Muktasari:
- Mbali na hilo, Othman ameahidi kukomesha vitendo vya ukahaba vilivyopo kisiwani humo ili kurejesha ustaharabu wa kisiwa.
Unguja. Mgombea urais wa Zanzibar, kwa tiketi ya ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman amesema endapo akiingia madarakani Oktoba 29, 2025, ataanza kusafisha vitendo vya ufisadi vinavyodaiwa kuwepo visiwani humo.
Amesema vitendo vya kifisadi vilivyopo visiwani humo vinasababisha athari mbalimbali ikiwemo wananchi kukosa haki zao, kudhulumiwa ardhi zao, changamoto ambayo amesema imekithiri Pemba na Unguja.
Othman ameeleza hayo leo Ijumaa Oktoba 10, 2025 akihutubia mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanyika uwanja wa Mtende Jimbo la Makunduchi, Mkoa wa Kusini Unguja.
“Siku zote nasema ahadi yangu ni kuirejesha Zanzibar mikononi mwenu, jambo la pili nitasafisha ufisadi uliojengewa mizizi, ili nchi hii iendeshwe kistaarabu.
“Jambo la tatu, nataka nchi isimame katika maadili na silka zake, lakini jingine ni kumwezesha mwananchi, kama kuna uwekezaji basi uwe wa mwanzo kama huna maarifa Serikali itakupa maarifa,” amesema Othman.
Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Ismail Jussa akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Makunduchi
Katika hotuba yake, Othman ambaye ni Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, alirejea ahadi yake ya kuwaondolea tozo Wazanzibari katika bidhaa mbalimbali ikiwa kuwa ahueni ya maisha.
“Tumeshasema katika nchi hii kitu chochote kikiwemo chakula cha mtoto hadi mtu mzima, hakitakuwa na kodi wala tozo. Haya yanawezekana, ndio maana kila siku napokea ujumbe mfupi unaounga mkono ahadi hii,” amesisitiza.
Mbali na hilo, Othman ameahidi kukomesha vitendo vya ukahaba vilivyopo kisiwani humo, ili kurejesha ustaharabu wa kisiwa.
“Nitakalolifanya ni kila mwananchi kitambulisho cha Mzanzibari si cha Mzanzibari mkaazi. Sisi hatuna shida na mgeni bali, aje kwa heshima na akae kwa heshima na wao tutawapa vitambulisho.
“Nipeni kura zenu nikaifanye kazi hii, si mtanichagua na wasaidizi wangu (madiwani, wabunge, wawakilishi?)” ameeleza Othman.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Ushindi ya ACT Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa amewashukuru wananchi wa Makunduchi kwa kujitokeza kwa wingi katika mkutano huo, akisema wameonyesha njia.
“Ndugu zangu Wazanzibari mwaka huu, tukipoteza nafasi hii ya kuiondoa CCM Oktoba 29, fursa hii haiji tena. Ndio maana nawaambia uchaguzi huu, si wa CCM na ACT, bali ni uchaguzi kuamua kuinusuru Zanzibar au…. Sasa Mzanzibari kaa ujiulize usiongozwe kwa jazba.
“Sisi tumetimiza wajibu wetu, nyie wananchi jiulizeni mtaongozwa na ushabiki wa kisiasa au mtakumbuka kwa Zanzibar ni nchi yetu…wakati wa kupiga kura?” amehoji Jussa ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Zanzibar.
Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano kwa Umma wa ACT Wazalendo, Salim Biman amewataka Wazanzibari kujitokeza kupiga kura Oktoba 29, akisema safari hii hakutakuwa na changamoto ya kura kudaiwa kuibiwa.