Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

OMO: Nawashukuru wote walionipigia kura, sina cha kuwalipa

Muktasari:

  • Othman maarufu ‘OMO’ ametoa shukurani hizo leo Jumanne Novemba 11, 2025 wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wanachama, wananchi wa Wilaya za Chakechake na Micheweni, Pemba katika mwendelezo wa ziara yake ya siku saba kisiwani humo.

Pemba. Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman amewashukuru Wazanzibari wote waliompigia kura, licha ya kutoshinda nafasi ya urais wa Zanzibar, akisema hana cha kuwalipa.

Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), yalionyesha mgombea wa CCM, Dk Hussein Mwinyi alipata kura 448,892 sawa na asilimia 74.8 akifuatiwa na Othman kura 139,399 sawa na asilimia 23.22.

Othman, maarufu ‘OMO’ ametoa shukurani hizo leo Jumanne Novemba 11, 2025 alipokuwa akizungumza kwa nyakati tofauti na wanachama, wananchi wa wilaya za Chakechake na Micheweni, Pemba katika mwendelezo wa ziara yake ya siku saba kisiwani humo.

OMO aliyekuwa akipeperusha bendera ya kuwania nafasi hiyo kupitia Chama cha ACT Wazalendo katika uchaguzi huo, uliofanyika Oktoba 29 amewashukuru wananchi na wanachama wa chama hicho kisiwani Pemba, kwa kuvumilia changamoto mbalimbali katika mchakato huo.

“Sina cha kuwalipa wanachama na viongozi waliopambana. Kiukweli cha kuwalipa hatuna kutokana na kazi ngumu mlioisimamia licha ya vitisho, tulifanya kampeni za kuwaeleza Wazanzibari kwa umoja wao watuchague,”amedai.

“Viongozi na mawakala wa ACT Wazalendo mlifanya kazi kubwa kwa moyo mmoja, nawaomba endeleeni kulinda amani na kumshukuru Allah kwa usalama mlioupata baada ya uchaguzi huo,” ameeleza.

Katika maelezo yake, Othman ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar aliyemaliza muda wake, amesema licha ya rasilimali ndogo walizokuwa nazo, lakini walifanikiwa kutekeleza mipango yote ya kampeni.

Umoja ndio silaha

Katika hatua nyingine, Othman amewataka wanachama wa chama hicho, kuendeleza umoja wao akisema ndio silaha ya ushindi.

 “Leo kuna chama kimepatwa na wasiwasi mkubwa, licha ya changamoto zilizojitokeza katika uchaguzi bado tupo imara.  Wameanza kujiuliza kuna nini ndani ya ACT Wazalendo,” amedai Othman.

Amesisitiza umoja wa wanachama ndani ya chama hicho, ndio silaha muhimu ya kisiasa itakayowawezesha kukiondoa Chama cha Mapinduzi (CCM) madarakani.

Awali, Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa amesema mazungumzo yoyote yatakayofanyika lazima yahusishe kudai haki ya Wazanzibari, akisisitiza viongozi wa chama hicho hawatachukua uamuzi wowote bila kuwashirikisha wanachama.

“Nawaombeni mtuamini sisi viongozi wenu. Chochote tutakachofikia kwenye mazungumzo, hatutaamua bila kurudi kwenu,” amesema Jussa ambaye alikuwa Mwenyekiti wa kamati ya ushindi wa ACT Wazalendo.