Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NIKWAMBIE MAMA: Akina Yuda wasaliti ni wengi tu!!



Katika maisha hakuna kitu muhimu zaidi ya kula. Najua kuna watu watanipinga kwa hoja kwamba hakuna kitu muhimu kama kazi, wengine watasema kujitambua, kupumua na wapo watakaosema kusali. Sikatai, yote ni muhimu ila yanategemea kuwapo kwa mlo.

Pia, wajue kuwa kula ni moja ya matendo yasiyo na hiyari. Uwe mgonjwa au mwenye afya, uwe tajiri au masikini, uwe mgonjwa au uwe na afya ni lazima ule.

Binadamu huishi maisha aliyofunzwa na aliyojifunza. Watu wanavaa nguo baada ya kufunzwa tangu utotoni. Wanaendesha magari, wanajenga makazi na wanafunga ndoa baada ya kujifunza maisha bora ya kibinadamu.

Lakini kula ni jambo alilolijua kila mmoja bila kufundishwa wala kujifunza. Mtoto alipozaliwa tu, alijikuta akinyonya maziwa ya mama bila kuelekezwa na yeyote. Ukubwani akajifunza kutafuta chakula, lakini hakujifunza kula.

Ndio maana mimi hupenda zaidi mifano ya wanyama na watoto. Hawa hawana unafiki wala hawajui kuigiza, linaloonekana kwa nje ndivyo lilivyo ndani yake.

Simba hawezi kukutishia kukukimbiza, bali akifanya hivyo anamaanisha. Na ukiona mtoto anakuchukia, basi tafuta haraka sababu yake ili ujirekebishe. Mtoto aliyehudhuria sherehe ya Mfalme na Nguo ya Ajabu anatuthibitishia ukweli huu. Tunaambiwa Mfalme mjivuni alikusanya mafundi washoni, akawataka wamtengenezee vazi la ajabu.

Alitaka vazi lenye kuonekana na watu wema na wenye akili tu. Mafundi wote wakachemka, lakini fundi mgeni akachangamkoa fursa.

Aliingia na msaidizi wake na kumwonesha Mfalme vitambaa visivyokuwepo: “Unataka hiki cha rangi ya fedha au hiki cha dhahabu?” Mfalme kwa kutaka aonekane kuwa na akili, akachagua “dhahabu” ingawa hakukiona.

Basi kwa saa sita wakali hao wakawa wanakimbizana: “Vuta huko... kata hapo...” huku wakishona hewa. Hatimaye wakatabasamu kwa pamoja na kumvalisha Mfalme vazi lisiloonekana. Na yeye kwa kutotaka kuonekana mbumbumbu, aliwasifu mafundi wake kwa kazi nzuri.

Mfalme alipotokeza hadharani ukumbi ulipigwa na kimya cha mshangao, kisha zikafuata shangwe za kinafiki kumshangilia alivyopendeza.

Lakini mtoto aliyeambatana na mama yake aliuliza kwa mshangao: “Mbona Mfalme yupo uchi?” Wadaku waliosikia mapema waling’aka: “Mtoeni huyo mtoto mjinga!” Lakini punde walianza kuulizana: “Mwenzangu unaona nguo yoyote pale?” Jibu likawa “Hapana”!

Hapa ndipo tunapokubaliana kuhusu unyofu wa watoto. Ndio maana ushahidi wa mtoto hauna shaka, kwani wana roho safi na hawana unafiki.

Kwenye jambo lolote linalohusu kula (au riziki) hapakosekani unafiki, fitina na majungu. Kuna wavivu wanaokwazwa na maendeleo ya wachapa kazi.

Kwa kutotaka mabaya yao yaonekane, ni lazima watafanya lolote ili kubadilisha mambo. Kwenye madaraka, kiongozi yeyote anapaswa kujua kuwa yeye ni binadamu, kuna atakaowaridhisha kwa utendaji wake, lakini pia wapo atakaowakwaza.

Kama binadamu, kiongozi anapaswa kuyapima yote katika mzani mmoja. Ayashughulikie mapungufu yake kama jinsi anavyoshughulika na mafanikio. Asisahau kuwa heshima anayoipata ina tofauti kwa kila mmoja.

Wapo wakweli na waigizaji wanaofanana kama mchele na chuya kwenye kapu moja. Adui mkubwa wa mtu ni yule anayekula naye. Hivyo adui mkubwa wa kiongozi anaweza kuwa miongoni mwa watu wake wa karibu zaidi.

Mifano ipo wazi, Rais Tolbert wa Liberia aliuawa na mtu wake wa karibu, Samuel Doe. Rais Thomas Sankara wa Burkina Faso aliuawa katika mapinduzi yaliyoongozwa na rafiki yake wa karibu sana, Blaise Compaoré.

Katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Patrice Lumumba alipigania uhuru wa taifa lao kwa moyo wote. Lakini baada ya uhuru, washirika wake wakageuka wapinzani wake.

Akasalitiwa na kuuawa. Rwanda pia ilipitia kipindi kigumu wakati wa Rais Juvénal Habyarimana. Ingawa mazingira ya kifo chake yanaendelea kujadiliwa na wanahistoria, tukio hilo lilihusisha mvutano mkubwa wa makomredi.

Kundi la watu watu waliokuwa karibu sana na mamlaka walijisimika ndani ya mfumo wa uongozi. Mara nyingi maadui wa viongozi hawaji kwa sura ya adui. Hujificha nyuma ya tabasamu, sifa na viapo vya uaminifu.

Hapo Uganda, Milton Obote alipinduliwa na jenerali wake mwenyewe, Idi Amin. Ingawa hakuuawa wakati huo, tukio hilo linaonesha jinsi watu wa karibu wanavyoweza kubadilika ghafla wanapoona fursa ya madaraka.

Amin alikuwa sehemu ya mfumo wa Obote, lakini mwisho akawa sababu ya kuanguka kwake. Somo hapa si kuhusu kifo pekee, bali usaliti unaoweza kutokea ndani ya nyumba moja.

Tunaposoma mifano hii, tusikimbilie kuwalaumu wasaliti peke yao. Wakati mwingine viongozi nao hufanya makosa makubwa ya kuikwepa mifumo ya haki na kujitengenezea mifumo yao isiyo rasmi. Kiongozi hasikilizi tena ushauri wala malalamiko ya umma, bali hukubali kuongozwa na wasiri wake pekee.

Hapo hata walinzi wake watashindwa kumkinga dhidi ya ‘chawa’ wanaompaka mafuta kwa mgongo wa chupa.

Maneno ya Mbunge wa Baraza la Wawakilishi kuhusu “Yuda Msaliti” yanaweza kuwa na ukweli. Japokuwa amerusha “jiwe gizani”, lakini mambo hayo yanawezekana.

Ndio maana methali nyingi za Kiafrika zinasisitiza umuhimu wa kujichunguza. Kuna msemo unaosema, “Nyumba huungua kwa cheche iliyo ndani.”