Prime
Miaka 4 ya Samia madarakani, ‘umekula ng’ombe mzima, usishindwe kumalizia mkia’

Leo naungana na Watanzania wenzangu kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza miaka minne madarakani.
Kwa mtazamo wangu, hakuna shaka kwamba Rais Samia amefanya mambo makubwa na mazuri katika nyanja za siasa, uchumi na jamii. Hasa katika mabadiliko ya kisiasa, ameleta mageuzi makubwa na ya kupongezwa.
Ikiwa tungefananisha mafanikio yake na kula ng’ombe mzima, basi amebakiza mkia tu!
Je, huo mkia ni upi?
Mkia ambao bado haujamalizika ni mabadiliko madogo ya Katiba kwa hati ya dharura ili kurejesha haki mbili kuu za kikatiba ambazo ni ya kila Mtanzania kuwa huru kumchagua kiongozi yeyote wanayemtaka kwa mujibu wa Ibara ya 5 ya Katiba ya Tanzania ya 1977 na ya pili ni ya kila Mtanzania kugombea uongozi kwa mujibu wa Ibara ya 21 ya Katiba ya Tanzania ya 1977.
Kwa kuwa huu ni mwaka wa uchaguzi, sitaingia sana katika vipengele, lakini ni wazi kuwa sheria yetu ya uchaguzi iliwahi kubatilishwa na Mahakama Kuu kwa kukiuka katiba.
Serikali, badala ya kurekebisha kasoro hizo, ilifanya marekebisho ya nane ya Katiba kwa njia isiyo sahihi ili kuhalalisha ubatili huo.
Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, chini ya majaji watatu, Amir Manento, Salum Masati na Thomas Mihayo ilitamka kuwa marekebisho hayo ni batili.
Serikali ilikata rufaa na Mahakama ya Rufaa chini ya Jaji Mkuu Agustino Ramadhani pamoja na majaji wengine sita, ilithibitisha kuwa Bunge lilipaswa kuondoa marekebisho hayo. Mahakama haikufanya kazi peke yake, bali ilisaidiwa na wataalamu wa sheria walioteuliwa kama marafiki wa mahakama (Amicus Curiae), akiwemo Othman Masoud Othman, Profesa Palamagamba Kabudi na Profesa Jwan Mwaikusa (Mungu amrehemu).
Nini kifanyike?
Kama nilivyowahi kushauri, ukosoaji wa kujenga lazima uambatane na mapendekezo ya suluhisho.
Kwa sasa, Rais Samia anapaswa kuruhusu mabadiliko madogo ya katiba (minimum reforms) ili kuhakikisha uchaguzi wa 2025 unakuwa huru na wa haki.
Tunamshukuru Rais Samia kwa kufanyia marekebisho ya sheria ya uchaguzi, lakini bado kuna maeneo yenye kasoro zilizobatilishwa na Mahakama Kuu. Tunamuomba aridhie mabadiliko ya katiba ili kuondoa kasoro hizo.
Aidha, tunashukuru kwa kuondolewa kwa kipengele kinachowalazimisha wagombea wadhaminiwe na vyama vya siasa, lakini bado kuna haja ya kuweka vigezo vya ziada kwa wagombea wa urais ili kuzuia uwezekano wa mtu mmoja tajiri kuinunua nchi.
Kwa nafasi nyingine kama ya ubunge, udiwani na serikali za mitaa, kila Mtanzania mwenye sifa anapaswa kuwa huru kugombea bila kulazimika kupitia chama cha siasa.
Tunamshukuru Rais Samia kwa kubadilisha jina la Tume ya Uchaguzi kutoka NEC kuwa INEC, lakini kilichoombwa si jina jipya, bali tume huru na shirikishi. Tunahitaji mabadiliko halisi ya mfumo wa tume, si mabadiliko ya jina pekee.
Tunapendekeza pia kuwe na mazingira ya ushindani wa haki kwa vyama vyote vya siasa, huku uchaguzi ukiendeshwa kwa uwazi wa hali ya juu.
Mawakala wa vyama waruhusiwe kushuhudia mchakato wote wa kuhesabu kura hadi kwenye vituo vya kujumlishia matokeo. Kama hakuna cha kuficha, kwa vituo vya kujumlishia matokeo huru zisiruhusiwe?
Tanzania tumebarikiwa kuwa na Rais anayependa na kutenda haki. Tayari amefanikisha mengi na kilichosalia ni hatua chache za mwisho.
Binafsi nimwombe Rais Samia, kwa mamlaka yake kama kiongozi mkuu wa nchi, aruhusu mabadiliko haya madogo ya katiba ili kuhakikisha uchaguzi wa 2025 unakuwa huru na wa haki kwa kweli. Akifanya hivyo, atabarikiwa, Watanzania tutabarikiwa na nchi yetu itabarikiwa.
Mungu Ibariki Tanzania!