Prime
Mapito ya Komu na tafsiri ya kisiasa

Dar es Salaam. Mwanasiasa mashuhuri nchini Tanzania na kada wa zamani wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Anthony Komu, ametangaza kurejea rasmi katika chama chake cha awali, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Akizungumza baada ya kujiunga tena na chama hicho, Komu amesema anaamini mwelekeo wa sasa wa Chadema wa kurudi kwa wananchi ni sahihi na unaotia matumaini.
Kwa kurejea kwake, Komu anakuwa mwanasiasa wa pili mashuhuri kujiunga tena na Chadema ndani ya kipindi cha siku 27. Hii ni kufuatia kurejea kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa, katika uzinduzi wa kampeni ya "No Reform, No Election" uliofanyika mkoani Mbeya Machi 23, 2025.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wanaeleza kuwa huenda Chadema imeamua kuwaruhusu makada wake wa zamani kurejea ili kuendeleza harakati zao za kisiasa kupitia chama hicho. Wengine wanaona hatua hii kama mkakati wa kujaza pengo la uongozi wa juu, kufuatia baadhi ya viongozi wenye mvuto kutokuwa na msimamo wa wazi kuhusu kuendelea kubakia ndani ya Chadema.
Akizungumza na Mwananchi baada ya kupokelewa Chadema, Komu alisema ‘kutulizwa kama nyama ya ndafu’ na uongozi uliopita ni sababu iliyomsukuma kukihama chama NCCR Mageuzi.
Ndafu ni nyama ya mbuzi ambayo ni maarufu kwa kabila la Wachaga huandaliwa kwa kuokwa na kupambwa kiaina na viungo vya karoti, vitunguu na nyanya maalumu kwa kuliwa kwenye sherehe mbalimbali zikiwamo harusi na ‘Send- off.’
Lakini itakumbukwa pia kada huyo anayo historia ya kuhama na kurejea ndani ya chama hicho.
Mara ya mwisho aliondoka baada ya kuhojiwa na Kamati Kuu ya Chadema akiwa Mbunge wa Moshi Vijijini, kufuatia tuhuma za kuhusika na mpango uliodaiwa kuwa na nia hasi dhidi ya kada mwenzao, Boniface Jacob, ambaye kwa wakati huo alikuwa Meya wa Manispaa ya Ubungo.
Akizungumza na Mwananchi baada ya rejea Chadema na kupokelewa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche, Komu amesema hakufurahishwa na uongozi uliopita wa Chadema.

“Mimi si ndafu kama walivyoniona baadhi ya viongozi waliopita. Niliona kuna mazizi mengine jirani yanayohitaji mchango wangu, ndipo nikaamua kuondoka na kujiunga na NCCR-Mageuzi,” alisema Komu.
Hata hivyo, wakati Komu akiyasema hayo, mchambuzi wa masuala ya siasa, Said Msonga anasema changamoto ya Komu ni kuwa mguu moja ndani mwingine nje.
Anasema kwa wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema watu wa aina hii, hutia mashaka ya kudumu ndabi ya chama kimoja kwa muda mrefu.
“Wanachukuliwa kama watu ambao hawana utulivu na hawana malengo thabiti na msingi katika eneo wanalo hudumu na huwa wanawatilia mashaka kwamba wanaweza kuwa naye leo lakini ni rahisi kuhamia chama kingine kesho,” amesema Msonga.
Amesema mara nyingi vyama vya siasa vinatakiwa kuwa na viongozi wenye msimamo na kuweka imani nao, muda na jitihada zao kuhakikisha wanafanya kazi.
“Vyama vina itikadi zinazotofautiana kile kinacho hubiriwa na Chadema ni tofauti na vyama vingine, mtu akiwa anahama hama anashindwa kuendana na vyama vingine,” amesema mchambuzi huyo.
Kwa mtazamo wa Msonga, anasema Komu ni mwanasiasa wa muda mrefu ingawa kipindi cha kati alikuwa haonekani kwenye majukwaa huenda sasa ameamua kurejea ndani ya Chadema akitazama wanasiasa aliokuwa nao nyakati zile, wamerejea akiwamo Dk Slaa.
“Kinachoonekana uongozi wa juu wa Chadema ni kama bado unatafuta kupata watu wenye uzito kuifanya taasisi ionekane, pamoja na kwamba wana Mwenyekiti Lissu na Makamu wake John Heche, lakini ukiangalia hakuna wengine na bado kuna ombwe, tofauti na uongozi uliopita,” amesema mchambuzi huyo.
Kulingana na maelezo ya Msongo anasema uongozi wa Lissu unapambana kutafuta watu wa kukipa hadhi chama kama kinavyostahili ni jambo ambalo inawezekana ameombwa na uongozi uliopo.
“Mazingira hayo yanaweza kuwa na matokeo kwa ujio wa Komu ingawa Komu wa miaka ile hawezi kuwa Komu wa sasa, lakini hivi sasa watamtumia kama mtu muhimu kama umma utaona ni karata ya kushawishi watu wa kufanya uamuzi,” amesema Msonga.
Amesema uongozi wa Lissu unapambana baada ya kuona viongozi waliokuwa chini ya Mbowe wanapiga hatua ya kurudi nyuma na hata wakizungumza wanaonekana kutokubaliana na msimamo wake.
Mchambuzi wa masuala ya siasa na jamii, Bubelwa Kaiza, amemuelezea Komu kama mwanasiasa ambaye kwa kipindi cha miaka 33 ya mfumo wa vyama vingi, amewahi kuwa ndani ya NCCR-Mageuzi pamoja na Tundu Lissu, ambaye sasa ni Mwenyekiti wa Chadema.
“Wote waliwahi kuwa NCCR-Mageuzi, lakini baada ya kutofautiana, Komu alihamia Chadema mwaka 2008. Mwaka 2020 alirudi tena NCCR-Mageuzi, na sasa anarudi Chadema. Inaonekana haoni tofauti kubwa ya kisera kati ya vyama hivi viwili,” amesema Kaiza.
Kwa mujibu wa Kaiza, huenda uamuzi huo umetokana na mtazamo wa kwamba NCCR-Mageuzi imepungua nguvu, hivyo akaona ni bora kurejea Chadema ambako anaamini anaweza kushirikiana na watu katika kutekeleza mipango ya kisera.
“Komu si mgeni kwenye siasa, amekuwa kwenye ulingo huu kwa muda mrefu. Ingawa haonekani kuwa na nia ya kwenda chama tawala, ameendelea kuhama kutoka Chadema kwenda NCCR-Mageuzi na sasa anarudi tena Chadema,” alisema Kaiza.
Kwa upande wake, Komu anasema licha ya kujiunga na NCCR-Mageuzi, maisha yake ya kisiasa hayakwenda kama alivyotarajia.

Alijikuta akikumbwa na changamoto mbalimbali, zikiwemo kesi alizodai kuwa zilitungwa, zikihoji uhalali wa uanachama wake ndani ya chama hicho.
"Nilipokea barua kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ikieleza kuwa mimi si mwanachama halali wa NCCR-Mageuzi. Mizengwe mingi ilifuata, ingawa baadaye hali ilitulia, bado mambo hayakuwa shwari," amesema Komu.
Anasema baada ya kugundua kuwa ndani ya NCCR-Mageuzi alikuwa ametengwa kama "ndafu" na uongozi kushindwa kutambua mchango wake, aliamua kuwa huu ndio wakati sahihi wa kurejea Chadema.
"Baada ya Tundu Lissu na John Heche kushika hatamu za uongozi, walinialika. Kwa kuwa sikuwa na uhusiano wa moja kwa moja na chama kingine, nikaona ni vyema nirejee Chadema kushirikiana nao kuendeleza harakati zetu," amefafanua Komu.
Kwa mujibu wa Komu, anataka umma utambue kuwa bado hajastaafu siasa na ameamua kurudi Chadema ili aendelee kutoa mchango wake kadri atakavyohitajika, kwa lengo la kuhakikisha Watanzania wanaishi maisha bora.
"Naamini kabisa chini ya uongozi wa Lissu na Heche, ninaweza kutumika. Na kama ulivyoshuhudia wakati wa mapokezi, Makamu Mwenyekiti John Heche alinitambulisha kwa sifa nyingi, ishara kwamba umma una imani nami na kuna mchango ninaoweza kutoa kwa maendeleo ya chama," amesema Komu.
Aamesema aliondoka Chadema mwaka 2020 baada ya kuona dalili za chama kuanza kuwapuuza wananchi na kuweka kipaumbele kwa kundi fulani la watu waliokuwa karibu na uongozi.
"Uongozi wa sasa una dhamira ya dhati ya kurudisha chama kwa wananchi. Hatima ya nchi hii iko mikononi mwa wananchi. Ni wao wataamua aina ya uchaguzi, namna nchi itakavyotawaliwa, na nani ataiongoza," alisema Komu.
Operesheni ya ‘No Reform No Election’
Komu amesema operesheni hiyo inalenga kuwapa wananchi mamlaka halali ya nchi yao kama Katiba ya mwaka 1977 inavyobainisha kuwa mamlaka hutokana na wananchi kupitia sanduku la kura.
"Nina imani kuwa kampeni hii ya ‘Bila Mabadiliko, Hakuna Uchaguzi’ itakuwa na manufaa makubwa ikiwa itawafikia wananchi. Jambo muhimu ni wananchi kuelewa kwamba wao ndio chanzo cha mamlaka na bila wao, hakuna mabadiliko yatakayowezekana," alisisitiza Komu.
Kuhusu hali ya kisiasa ya sasa, Komu anaamini bado ana mchango wa kutoa, hasa baada ya kuona kuwa alipokuwa nje ya Chadema, hakutumika ipasavyo kulingana na uwezo wake wa kisiasa na ushawishi alionao.