Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vigogo Chadema Mwanza, wengine 167 watimkia CCM

Muktasari:

  • Joto la uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, limeendelea kupanda huku Chama Cha Mapinduzi (CCM) kisisitiza kuwa kina uhakika wa kupata ushindi wa kishindo kutokana na kazi zilizofanywa na Serikali zake.

Mwanza. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeendelea kujiimarisha kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, baada ya kupokea wanachama wapya 170 kutoka vyama vya upinzani.

Wanachama hao wapya wamepokea leo Ijumaa Mei 2, 2025 wakati wa mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla uliofanyika Viwanja vya Furahisha jijini Mwanza.

Miongoni mwa wanachama hao waliopokewa yumo Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mwanza, Peter Mtyoko pamoja na wajumbe wa chama hicho kutoka Kanda ya Victoria.

Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo ya CCM, Amos Makalla (kulia) akimtambulisha aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mwanza, Peter Mtyoko baada ya kuhamia chama hicho leo Mei 2, 2025 wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Furahisha jijini Mwanza.

Akizungumza mara baada ya kupokea, Mtyoko amesema amelazimika kuchukua hatua kama kiongozi kutokana na chama chake cha zamani (Chadema) kuendeshwa kama cha kiharakati.

"Siku mbili zilizopita nilifanya tafakari ya namna ambavyo mimi kama kiongozi natakiwa kuchukua hatua. Chama chetu nilichokuwepo kiukweli tumebaki kama chama cha kiuharakati. Tunaposema tunazuia uchaguzi usifanyike kwa mtu mwenye akili kama mimi inaweza ikakutafakarisha sana.

“Labda tumekosa ushawishi kuishawishi Serikali na kukubaliana na matakwa ambayo sisi tunatamani yawe ili tuweze kushiriki uchaguzi ambao ni wa huru na haki.

“Kama tumekosa ushawishi na matakwa yetu yakaonekana yasiyofaa tunawezaje kuzuia uchaguzi? Hivyo, nimetafakari na mwisho nimeona nijiunge na CCM kwa hiari yangu," amesema Mtyoko.

Naye, Katibu Uenezi wa Chadema Kanda ya Victoria aliyehamia CCM pamoja na Mtyoko, Andrew Masenya amesema lengo ya uanzishwaji wa vyama vya siasa ni kuleta tija, afya na ustawi wa wananchi pamoja na ushindani wa sera.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mwanza, Peter Mtyoko akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa CCM uliofanyika uwanja wa Furahisha jijini Mwanza leo Ijumaa Mei 2, 2025.



Hata hivyo, amesema kuwa Chadema kimetoka kwenye lengo hilo kwa sasa.

"Ndugu zangu tumeondoka (Chadema) kwa sababu hatuwezi kuishi kwenye chama ambacho kimehama katika misingi ya kushindanisha kwa sera, imefika wakati kinapambana na Jeshi la Polisi,” amesema Andrew.

Awali, akihutubia mamia ya wanachama wa CCM, Makalla amesema kutokana na maboresho yaliyofanywa katika Sheria za Uchaguzi uchaguzi mkuu wa Oktoba, 2025 utakuwa huru na haki na anayeshinda kwa haki atatangazwa mshindi.

"Katika hili naomba niende kinyume na wale wanaoamini kuwa demokrasia ya kweli ama uchaguzi huru na haki ni pale tu chama tawala kinaposhindwa. Demokrasia ya kweli ni pale hata pale chama tawala kinaposhinda kwa kwa kishindo," amesema Makalla,

Amesema wanaamini kwa kazi walizozifanywa na Serikali ya CCM ni ushahidi na ushindi wa wazi kwa chama hicho, huku akiahidi kuwa kuelekea uchaguzi huo, Falsafa ya 4R zilizoasisiwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, zitatumika kikamilifu.

"Tunawaahidi kuwaletea Ilani ya Uchaguzi kwa mwaka 2025-2030 nzuri zaidi kuliko zilizopita. Itakuwa Ilani itakayokonga nyoyo za Watanzania na ambayo imefanyiwa kazi kikamilifu. Itakuwa Ilani inayokwenda kujibu changamoto za Watanzania na kuongeza matumaini ya wananchi wetu,” amesema Makalla.