Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Lissu achambua uongozi wa Rais Donald Trump

Muktasari:

  • Baada ya Trump kuapishwa Januari 20, 2025, kuwa Rais wa 47 wa Marekani, alitangaza mabadiliko makubwa katika utawala wake, ikiwa ni pamoja na hatua kali dhidi ya wahamiaji wasio na vibali na sera mpya za kiuchumi na kimataifa.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, amesema kuwa mabadiliko ya sera yanayofanywa na Rais wa Marekani, Donald Trump, ni ishara kwamba Tanzania inapaswa kujifunza kuachana na utegemezi wa mataifa ya nje kwa sababu hali hiyo ni hatari.

Amesema katika siku 30 tu za kwanza za utawala wake kwa muhula wa pili, Trump ameanza kufanya mabadiliko yenye athari kubwa, hasa katika sekta ambazo Tanzania ilikuwa ikitegemea misaada, kama vile afya, kilimo na miundombinu ya barabara.

Hata hivyo, Februari 6, 2025, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa alipokuwa bungeni, alizungumzia mabadiliko hayo ya sera na kusisitiza kuwa Serikali ya Tanzania imejipanga kujenga uchumi unaojitegemea.
"Ni kweli kwamba serikali yetu inaheshimu sera za mambo ya nje na tunatekeleza mikataba kwa mujibu wa makubaliano na nchi husika. Hata hivyo, tumeanza kuona mabadiliko katika sera za baadhi ya nchi zenye uwezo mkubwa kama Marekani, na mabadiliko haya yanaweza kuathiri mataifa mbalimbali, ikiwemo Tanzania," alisema Majaliwa.

Baada ya Trump kuapishwa Januari 20, 2025, kuwa Rais wa 47 wa Marekani, alitangaza mabadiliko makubwa katika utawala wake, ikiwa ni pamoja na hatua kali dhidi ya wahamiaji wasio na vibali na sera mpya za kiuchumi na kimataifa.

Miongoni mwa uamuzi ulioishangaza dunia ni kuvunjwa kwa Shirika la Marekani la Misaada ya Kimataifa (USAID), ambalo lilikuwa likiendesha operesheni zake duniani kote.

Hatua hiyo imewaathiri maelfu ya wafanyakazi waliokuwa wakihudumu katika shirika hilo na pia nchi zinazoendelea, ikiwamo Tanzania, ambazo zilikuwa zinategemea misaada yake.

Akichambua hali hiyo, alipofanya mahojiano maalumu na Mwananchi hivi karibuni nyumbani kwake Tegeta jijini Dar es Salaam, Lissu amesema mabadiliko yanayofanywa na Trump yanatoa fundisho kubwa kuhusu hatari ya utegemezi kwa mataifa mengine.
“Tunahitaji kujifunza kuwa utegemezi ni hatari kwa nchi na hata kwa mtu binafsi. Unapowategemea wengine mambo yanapotokea katika mataifa hayo, hata kama hayakuhusu moja kwa moja, yatakugusa,” amesema kiongozi huyo.

amesisitiza kuwa Tanzania lazima ijifunze kujiimarisha kiuchumi ili iweze kustahimili mabadiliko ya kimataifa.

Hata hivyo, ameifafanua kuwa kujitegemea hakumaanishi kuacha kushirikiana na mataifa mengine, bali kuwa na uwezo wa kujisimamia pale mabadiliko yanapotokea.

“Ni muhimu kuwa na uwezo wa kusimama kwa muda fulani, ingawa huwezi kujitegemea kabisa muda wote, kwa sababu hata mataifa makubwa kama China hayawezi,” amesema Lissu.

Ameongeza kuwa athari za Urais wa Trump zinahusu dunia nzima, si kwa maana hasi pekee, bali pia kwa maana pana ya mabadiliko ya kimfumo.

Ametaja mfano wa USAID, akisema kuvunjwa kwa shirika hilo ndani ya muda mfupi ni jambo lenye athari kubwa.

“USAID ilianzishwa mwaka 1961 na Rais John F. Kennedy kama hatua muhimu katika masuala ya uhusiano wa kimataifa. Ilikuwa sehemu ya juhudi za Marekani kusaidia ujenzi wa Ulaya baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, na kwa muda mrefu imekuwa msaada mkubwa kwa nchi zinazoendelea,” amesema.

TLissu amesema mpango wa miaka 50 ulikuwa mradi mkubwa wa Marekani wa kuijenga upya Ulaya baada ya Vita vya Pili vya Dunia, na kufanikiwa kwake kulifanya taifa hilo kuwa kinara wa dunia.

“Sasa Trump ndani ya mwezi mmoja ametangaza kufuta USAID, shirika lenye bajeti kubwa linaloendesha operesheni zake kote ulimwenguni. Katika nchi kama Tanzania, sekta ya afya imekuwa ikifaidika kwa miaka mingi na fedha hizo, hasa katika mapambano dhidi ya Ukimwi na miradi mikubwa ya malaria,” amesema.

Kwa mujibu wa Lissu, msaada wa USAID haujaimarisha sekta ya afya pekee bali pia miundombinu ya barabara, akitolea mfano barabara ya lami kutoka Tunduma hadi Sumbawanga iliyojengwa kwa msaada wa watu wa Marekani.

“Hela za watu wa Marekani ziko kila sehemu hapa Tanzania, na zinatolewa kupitia USAID. Kufutwa kwa shirika hilo kumesababisha maelfu ya wafanyakazi walioajiriwa kupitia miradi yake kukosa ajira,” amesema.


Athari za Trump ukilinganisha na viongozi wa zamani

Lissu amesema kuwa athari za Trump kwenye mradi wa USAID ni kubwa. Aidha, amesema kuwa Rais huyo anafanya mambo ambayo hakuna kiongozi mwingine wa hadhi yake aliyewahi kuyafanya.

“Nafahamu historia ya Marekani na marais wake kwa kiasi fulani. Hakuna Rais mwingine kama Trump anayefanya mabadiliko makubwa kwa mtazamo wa sera za nje, labda tujirudishe kwenye enzi za waanzilishi wa taifa hilo kama George Washington, John Adams, na Thomas Jefferson, ambao walikuwa na msimamo wa kutotaka Marekani kujiingiza katika migogoro ya Ulaya,” amesema.

Kwa mujibu wa Lissu, sauti ya waanzilishi hao wa taifa la Marekani inasikika kupitia sera za Trump, ambaye anatanguliza maslahi ya Marekani na kujiondoa katika masuala ya Ulaya.

Amesema Marekani imekuwa mdhamini wa ulinzi wa bara hilo tangu Vita Kuu ya Pili ya Dunia, ikiwa na majeshi makubwa zaidi ya nchi yoyote ya Ulaya na kuweka ngome za kijeshi katika maeneo mbalimbali.

Lissu amesema kwa mara ya kwanza, Trump ametangaza kuwa jukumu la ulinzi na usalama wa Ulaya libaki kwa mataifa hayo yenyewe. Kuhusu vita ya Ukraine na Russia, Lissu amesema Trump anadai kuwa ataimaliza kwa sababu, bila msaada wa kijeshi wa Marekani, Ukraine haitaweza kuendelea na vita hiyo.

“Bila Marekani kuitangaza Ukraine kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO mwaka 2008, hali ingekuwa tofauti. Sasa Trump anasema anaimaliza vita hiyo,” amesema.

Kwa mujibu wa Lissu, mataifa ya Ulaya yanapitia mtikisiko mkubwa kwa sababu taifa lililokuwa likiyasaidia kwa miaka mingi sasa linajiondoa.

“Marekani imekuwa taifa lenye nguvu kubwa duniani tangu kuvunjika kwa Umoja wa Kisovyeti mwaka 1991. Kwa zaidi ya miaka 30, dunia imekuwa chini ya utawala wa Marekani kama taifa lenye nguvu pekee, ingawa sasa China ni taifa lenye nguvu kubwa kiuchumi na linazidi kufanya biashara kuliko Marekani,” amesema kiongozi huyo.

Ameongeza kuwa, “Uchumi ukiwa mkubwa, hata nguvu za kijeshi huwa karibu. Hata hivyo, Russia nayo imerudi kwenye ubora wake na uthibitisho ni vita vya Ukraine, ambavyo imepigana dhidi ya NATO yote na kuweza kuhimili mashambulizi.”