Kinachomsubiri mgombea urais wa NCCR Mageuzi

Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha NCCR-Mageuzi, Haji Khamis. Picha na Maktaba
Muktasari:
- NCCR-Mageuzi kimemteua Haji Ambari Khamisi kuwa mgombea wake wa urais, akishirikiana na Joseph Selasini kama mgombea mwenza. Khamisi, mwanasiasa mkongwe, ameahidi kurejesha heshima ya chama hicho kama ilivyokuwa 1995 chini ya Agustino Mrema.
Dodoma. Machi 29, 2025, katika Ukumbi wa Mtakatifu Gasper, jijini Dodoma, chama cha NCCR-Mageuzi kilitangaza wagombea wake wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu, tukio lililozua msisimko mkubwa kwa wajumbe na wanachama wake.
Nafasi hiyo walimtwisha Haji Ambari Khamisi, ambaye alichaguliwa kupeperusha bendera ya chama hicho ikiwa ni saa chache baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi. Mgombea mwenza wake akapitishwa mwanasiasa wa siku nyingi wa chama hicho, Joseph Selasini.
Selasini pia kwenye kikao hicho alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti kwa upande wa Tanzania Bara, nafasi aliyokuwa akiitetea na alikuwa mgombea pekee.
Kwa hali hiyo, Haji anakuwa mtu wa tatu kutajwa katika nafasi hiyo na sasa atakwenda kupambana na wagombea wengine ambao ni Samia Suluhu Hassan (CCM) na Doyo Hassan Doyo (NLD). Mwingine ambaye pia ameonesha nia ya kutaka kugombea nafasi hiyo ni Doroth Temu wa ACT-Wazalendo.
Haji Ambari Khamisi ni nani
Haji Ambari Khamisi ni mwanasiasa mkongwe katika siasa za vyama vingi na mara nyingi ametajwa kuwa mtu mwenye msimamo mkali, asiyeyumbishwa na mpenda mageuzi.
Khamisi (62) ni mzaliwa wa visiwa vya Zanzibar, aliyeanzisha harakati za kisiasa akiwa na Chama cha Wananchi (CUF) kabla ya kujiunga na NCCR Mageuzi, ambacho amekitumikia kwa muda mrefu sasa.
Khamisi amewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho kwa upande wa Zanzibar wakati huo chama kikiwa chini ya uongozi wa James Mbatia, ambaye mwaka 2022 aliondolewa madarakani.
Ni mtu aliyepitia milima na mabonde akiwa ndani ya NCCR Mageuzi, hasa alipoingia mgogoro na Mbatia, hadi alipotangaziwa kufukuzwa uanachama.
Amewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD.
Jinsi alivyopanda
Wakati mgogoro ukiendelea chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa wakati huo, Joseph Selasini, Khamisi alijikuta akihusishwa katika mvutano huo.
Yeye pamoja na Mweka Hazina, Susan Masele, walikabiliwa na azimio la kuondolewa baada ya wajumbe 47 kati ya 81 wa Halmashauri Kuu kupendekeza wafukuzwe.
Sababu iliyotolewa kwa hatua hiyo ilikuwa ni kuhusika kwake katika mpango wa kumwondoa madarakani mwenyekiti Mbatia, jambo alilokiri, akisema lilikuwa la lazima ili kukinusuru chama.
Hata hivyo, uamuzi huo ulibatilishwa na uamuzi wa Septemba 24, 2022, uliofanywa na mkutano mkuu wa chama hicho.
Kugombea urais
Hii si mara ya kwanza kwa kiongozi huyo kuteuliwa kuwa mgombea kwenye uchaguzi. Mwaka 2010 alijitosa pia kugombea nafasi ya Rais wa Zanzibar, ingawa hakufanikiwa kupenya.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu, Machi 312, 2025, Khamisi anasema kitendo kile kimemfanya awe anaitwa rais katika mitaa mbalimbali ya Manispaa ya Zanzibar, ingawa hakushinda kwenye uchaguzi huo.
Mwaka 2020, aliteuliwa tena na chama chake kuwa mgombea mwenza wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya mgombea Yeremia Maganja, aliyekuwa amekabidhiwa kijiti cha kuongoza.
Kwenye mikutano kadhaa aliyoihutubia, Khamisi alisimamia msimamo wa utu na mara nyingi kampeni zake zilizungumzia amani na watu kuacha uonevu, mambo aliyosema yangeweza kulisogeza Taifa kwenda mbele zaidi.
Namna alivyoteuliwa
Haikuwa kazi ngumu, na dalili za yeye kupewa nafasi ya kuwa mgombea wa kiti cha urais zilionekana mapema hata kabla ya kuanza kwa mkutano huo. Ingawa mara nyingi ilisemwa atakabidhiwa kijiti hicho, mgombea mwenza wake atakuwa Selasini kabla ya uchaguzi mkuu uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.
Kweli upepo ulienda hivyo, na wakiwa wanaendelea na mkutano wao, Selasini alionekana hadharani kumpigia debe Khamisi.
Mara chache Selasini alionekana kuzungumza na wajumbe kuhusu yeye kuwa mgombea mwenza, lakini mwenyekiti awe mgombea urais, mazungumzo ambayo yalianza kusambaa kwa haraka. Muda ulipofika wa kutajwa nani agombee nafasi hizo, alitajwa, na wajumbe wakakubaliana kwa kauli moja.
Alivyojinasibu
Baada ya kutangazwa kuwa atapeperusha bendera ya NCCR Mageuzi, mwenyekiti huyo aliwapa tumaini wanachama na viongozi wenzake kwamba atafanya kile kilichotokea 1995, wakati chama hicho kilipomsimamisha Agustino Mrema (marehemu), aliyechukuana vikali na hayati Benjamin Mkapa wa CCM.
“Siendi kugombea kwa kujifunza, nakwenda kuirudisha heshima ya NCCR Mageuzi ya mwaka 1995. Tumepoteza malengo, lazima malengo yetu yatimie sasa. Naomba mnipe ushirikiano mimi na wagombea wengine kuanzia ngazi ya udiwani na wabunge,” aliwaambia wajumbe wa mkutano huo pamoja na wanachama.
Hata hivyo, mteule huyo anasisitiza kuwa chama hicho hakiendi kusimama na vyama vingine, bali kitasimama kwa kujitegemea na kamwe hawako tayari kudanganywa kama ilivyotokea miaka ya nyuma.
Mlima unaomsubiri
Wanachama wa NCCR Mageuzi ni kama watu waliopoteza tumaini baada ya kukosa hata mbunge mmoja kwenye chaguzi kadhaa, wakati kilikuwa ni chama kikuu cha kwanza kwenye upinzani.
Kutokana na hilo, wanachama wanatamani kurudisha makali hayo, lakini kubwa ni kujaribu kuona kama anaweza kuvitumia viatu vilivyovaliwa na Mrema.
Mbali na hilo, atatazamwa kama mtu jasiri anayetegemewa kutokana na kuongoza harakati zinazoelezewa kuleta mafanikip ndani ya chama hicho cha NCCR – Mageuzi.
Kwenye ushindani
Licha ya ukweli kuwa NCCR Mageuzi ndiyo baba wa mageuzi kwenye siasa za vyama vingi, kwa sasa hakihesabiki kama chama kinachoweza kutoa ushindani baada ya kuonekana kama kimepoteza mvuto.
Wanachama wake waliokuwa na mvuto na ushawishi wakati huo, wengi walitimkia vyama vingine na wengine kurudi chama tawala, hivyo kubaki na wachache na wale ambao hawana uzoefu mkubwa.
Ngome ya chama hicho ilikuwa mikoa ya Kigoma, Kilimanjaro na sehemu ya Kanda ya Ziwa, lakini kikawika zaidi jijini Dar es Salaam. Hata hivyo, maeneo hayo kwa sasa hayavumi kama mwanzo.