Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kauli za wanasiasa wahamao, mjadala unaotikisa siasa za Tanzania



Dar es Salaam. Katika historia ya siasa za Tanzania, uhamaji wa wanasiasa kutoka chama kimoja kwenda kingine sasa imekuwa kama jambo lililozoeleka.

Hata hivyo, mjadala unaozidi kushika kasi si kuhusu uhamaji wao, bali ni kauli zinazotolewa na wahusika kabla, wakati na baada ya uhamaji huo, ambazo mara nyingi huonekana kukinzana waziwazi na hivyo kuibua mijadala mikubwa ya kisiasa na kimaadili.

Katika enzi hizi za mitandao ya kijamii, siasa zimeingia katika hatua mpya ambayo kila kauli ya mwanasiasa hubaki kama kumbukumbu ya kudumu.

Hali hii imefanya kila mwanachama wa chama cha siasa na hususan viongozi pindi akihama kutoka chama kimoja kwenda kingine na baadaye kurejea tena, huibua kumbukumbu za kauli zake za awali na wananchi hufanya rejea ya hotuba za zamani na kuzilinganisha na misimamo yake pindi arejeapo tena kwenye chama chake cha awali.

Hata hivyo, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Ibara ya 20, inatoa uhuru kwa mtu kujiunga au kujiondoa katika chama cha siasa.

Hata hivyo, katika uhalisia wa kisiasa nchini, mgombea yeyote anayetaka kushiriki uchaguzi analazimika kupitishwa na chama cha siasa kilichosajiliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, jambo ambalo limeendelea kuzua mjadala kuhusu kiwango cha uhuru wa kisiasa kilichopo nchini.

Wadau na wachambuzi wa siasa wanaeleza kuwa hali hiyo imekuwa chanzo cha mjadala mpana kuhusu namna mfumo wa kisiasa nchini unavyoweza kupanua au kuminya demokrasia.

Wapo wanaoona ulazima wa wanasiasa kuwa ndani ya vyama vya siasa kama mfumo unaotoa utaratibu thabiti wa kisiasa, huku wengine wakiona kuwa mfumo huo huwalazimisha wanasiasa kubaki ndani ya vyama hata pale wanapokosa nafasi au kutoridhishwa na mazingira yaliyopo ndani ya vyama hivyo.

Mwandishi wa habari mkongwe nchi Tanzania, Jesse Kwayu anaweka mjadala huu katika muktadha mpana zaidi wa kimfumo, akieleza kuwa mfumo wa kisiasa ndiyo chanzo kikuu cha misukosuko inayowakumba wanasiasa na kuwalazimu kubadili kauli mara kwa mara wanapokumbana na changamoto za kisiasa.

“Jambo la wanasiasa kuhama vyama na kubadili kauli zao ndiyo maana ya siasa. Tatizo ni namna mfumo wa demokrasia ya vyama vingi unavyominya siasa zenyewe. Katika mfumo ambao hakuna haki katika uchaguzi, mfumo wa siasa unakuwa umevurugika,” anasema Kwayu.

Anasema hoja ya msingi si uhamaji wa wanasiasa, bali changamoto za kimuundo kama mapingamizi ya wagombea, kuenguliwa kwa sababu za kiufundi na utegemezi wa vyama vinavyosajiliwa.

Kwa mtazamo wake, kama kungekuwa na uhuru mpana wa kugombea nafasi za uongozi mfano ubunge bila vikwazo, mjadala kuhusu uhamaji wa wanasiasa na kauli kinzani za wanasiasa hao huenda ungekuwa mdogo zaidi.

Mchambuzi mwingine wa siasa, Azaveli Lwaitama ambaye ni mwanazuoni mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), anaweka msisitizo katika mazingira ya mtu binafsi na mahitaji yake ndani ya siasa.

“Kitu muhimu ni hoja za wakati mtu anahama chama. Siasa ya kuingia na kutoka chama inatawaliwa na mazingira ya wakati huo. Hili halipaswi kuangaliwa kwa ujumla,” anasema.

Anasisitiza kuwa wanasiasa hawafanani, kwa sababu kila mmoja ana sababu zake. Wapo wanaojiunga na vyama kwa matarajio ya kupata nafasi za uongozi, wengine kwa maslahi ya kisiasa au kiuchumi, huku wengine wakiondoka kutokana na migogoro ya ndani ya chama.

Hivyo, anasema si sahihi kuwahukumu wote kwa kipimo kimoja cha usaliti au uaminifu, bali kila tukio linapaswa kuchambuliwa kwa muktadha wake.


Historia ya uhamaji na kauli zilizoibua mijadala

Tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini mwanzoni mwa miaka ya 1990, wanasiasa wameendelea kujiunga na kujiondoa katika vyama mbalimbali vya siasa.

Miongoni mwa mifano ya awali ni Makongoro Nyerere na Steven Wasira, ambao waliwahi kujiondoa ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga na NCCR-Mageuzi kabla ya kurejea tena CCM.

Tukio hilo lilionyesha kuwa uhamaji wa kisiasa ni sehemu ya historia ya demokrasia ya Tanzania tangu siku za mwanzo za mfumo wa vyama vingi.

Aidha, katika kipindi hicho, wanasiasa wengi waliokuwa CCM waliondoka na kujiunga na vyama vipya vilivyoanzishwa kati ya mwaka 1992 na 1993 kufuatia mageuzi ya kisiasa yaliyokuwa yakifanyika nchini wakati huo.

Mbali na hao, wapo pia waliolazimika kuondoka katika vyama vyao kwa kufukuzwa. Mfano ni Zitto Kabwe, aliyeondolewa Chadema mwaka 2015 na baadaye kuanzisha chama cha ACT-Wazalendo.

Kauli zake za muda mrefu kuhusu mageuzi ya mfumo wa kisiasa zilihusishwa na msimamo wake wa kutaka mabadiliko ndani ya chama, jambo lililoibua mjadala kuhusu tofauti kati ya msimamo wake na ule wa viongozi wa chama waliodai kusimamia misingi ya chama hicho.

Maalim Seif Sharif Hamad alihama CUF mwaka 2019 baada ya mgogoro wa muda mrefu wa uongozi na kujiunga na ACT-Wazalendo. Kauli zake kuhusu haki ya Zanzibar na demokrasia zilijadiliwa upya baada ya mabadiliko hayo, zikionesha namna misimamo ya kisiasa inavyoweza kutafsiriwa upya kulingana na mazingira mapya.

Mwaka 2015 uliweka alama kubwa katika historia ya siasa za Tanzania baada ya Mawaziri Wakuu wawili wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye, kuondoka CCM na kujiunga na Chadema.

Kauli zao za awali zilizoonyesha uaminifu kwa CCM zilirejea mitandaoni baada ya uhamaji wao, jambo lililochochea mjadala kuhusu uaminifu wa kisiasa, mabadiliko ya misimamo na uadilifu wa viongozi hao.

Lowassa na Sumaye, waliowahi kushika nafasi za juu za uongozi nchini, walijenga hoja kwamba CCM ilikuwa imeshindwa kuiongoza nchi kufikia maendeleo yaliyotarajiwa na kuwataka wananchi kuiamini Chadema.

Hata hivyo, baada ya kipindi hicho cha kisiasa, wote walirejea CCM na kauli zao zikabadilika tena, wakianza kusifia baadhi ya mambo ambayo hapo awali walikuwa wakiyakosoa.

Kauli maarufu ya Lowassa ya “Nimerudi nyumbani, sitaki maswali,” ilizua mjadala mpana kuhusu uadilifu wa kisiasa, mfumo wa vyama na nafasi ya mwanasiasa binafsi ndani ya siasa za Tanzania.

Katika miaka iliyofuata, Lazaro Nyalandu aliondoka CCM na kujiunga Chadema mwaka 2017 kabla ya kurejea CCM mwaka 2022, kauli zake pia zilijadiliwa kwa kina katika medani za kisiasa.

Vilevile, Esther Bulaya alihama CCM na kujiunga Chadema mwaka 2015, akibadili msimamo wake dhidi ya chama hicho tawala kabla ya kurejea tena CCM mwaka jana.

Kauli yake ya “CCM ni kama Barcelona” ilienea kwa kasi mitandaoni na kuendelea kutumiwa kama mfano wa kauli zinazobadilika kulingana na mazingira ya kisiasa.

Pamoja naye, Esther Matiko na Nusrath Hanje waliondoka Chadema na kujiunga CCM.  Kauli zao zilionekana kukinzana na misimamo waliyoisimamia awali walipokuwa Chadema kabla ya mgogoro uliotokana na nafasi za ubunge wa viti maalumu kufuatia uchaguzi wa mwaka 2020.

Katika siku za karibuni, Peter Msigwa na Joseph Selasini pia walikihama Chadema. Selasini alikimbia NCCR-Mageuzi na Mchungaji Msigwa alijiunga na CCM, mwaka jana.

Baada ya uhamaji huo, misimamo yao ilionekana kwenda kinyume na baadhi ya hoja walizokuwa wakizitetea walipokuwa Chadema.

Msigwa, aliyekuwa mmoja wa viongozi waandamizi wa Chadema, alikihama chama hicho baada ya mvutano uliohusiana na uchaguzi wa ndani wa chama uliofanyika miezi michache kabla ya uchaguzi Mkuu wa Tanzania uliofanyika Oktoba 29, 2025 na kujiunga na CCM, ambako alianza kukikosoa chama chake cha awali.

Hotuba zake za zamani alipokuwa akikikosoa chama cha CCM alipokuwa Chadema, zilianza kusambazwa tena mitandaoni.

Baadaye alinukuliwa akisema, “Nilikuwa gizani kwa muda wote niliokuwa Chadema, sasa nuru imenifikia na nimeujua ukweli.”

Hata hivyo, katika hatua nyingine ya kisiasa, Mchungaji Msigwa alirejea tena Chadema na kutoa kauli mpya zinazoikosoa CCM, jambo lililoendeleza mjadala kuhusu mabadiliko ya misimamo ya kisiasa kwa wanasiasa hawa.


Je! Kauli na ahadi za wanasiasa ni matokeo ya mazingira?

Mjadala mkubwa unaoendelea ni iwapo kauli za wanasiasa zinapaswa kuchukuliwa kama ahadi za kudumu au kama matamko yanayotokana na mazingira ya kisiasa ya wakati huu uliopo.

Kwa wananchi wengi, kauli kinzani huonekana kama ishara ya kukosekana kwa uaminifu wa kisiasa.

Hata hivyo, wachambuzi wa siasa wanasema siasa ni mchakato unaobadilika kutokana na sababu mbalimbali, hivyo kauli za wanasiasa zinapaswa kuchambuliwa kwa kuzingatia muktadha wake.

Kwa upande wake, Mhadhiri na mchambuzi wa siasa, Dk Onesmo Kyauke anasema tatizo la kuhama hama kwa wanasiasa linachangiwa na kufanana kwa mwelekeo wa vyama vya siasa nchini.

“Ukiangalia CCM inasema inaamini katika Ujamaa, lakini ukiisoma Katiba yake utakuta mambo mengi yanafanana na vyama vingine. Wote wanaamini katika ubinafsishaji na masuala mengine mengi yanayofanana,” anasema.

Kuhusu utata wa kauli za wanasiasa, Dk Kyauke anasema ni jambo la kawaida kwa mwanasiasa kubadili mtazamo anapokihama chama.

“Mtu anayehama chama mara nyingi huanza kuzungumza hoja zinazolingana na chama alichohamia. Hilo si jambo la ajabu katika siasa,” anasema.

Anafafanua kuwa hata katika mataifa mengine kama Marekani, watu huhama vyama vya siasa, lakini vyama vyao hutofautiana zaidi kwa misingi ya kiitikadi.

“Unaweza kukuta chama kimoja hakiamini katika utoaji mimba, wakati kingine kinaamini. Hivyo si rahisi kwa mwanasiasa kuhama kutoka chama kimoja kwenda kingine chenye msimamo tofauti kabisa wa kiitikadi,” anasema.

Kwa mujibu wake, vyama vingi vya siasa nchini vinafanana kwa kiwango kikubwa katika sera na mwelekeo wa jumla.

“Ukisoma katiba za vyama vingi utakuta vinafanana kwa kiwango kikubwa sana. Tofauti zao mara nyingi huwa kwenye mikakati na vipaumbele vya utekelezaji, si katika misingi mikuu ya itikadi,” anasema.

Anasema kufanana huko kwa itikadi kunachangia kwa kiasi kikubwa uhamaji wa wanasiasa kutoka chama kimoja kwenda kingine.

Hata hivyo, anaamini kuwa kama vyama vingekuwa na tofauti kubwa za kiitikadi, wanasiasa wengi wangekuwa na uwezekano mkubwa wa kubaki katika vyama vinavyoakisi imani zao.

Kuhusu kauli zinazotolewa baada ya uhamaji wa kisiasa, Dk Kyauke anasema mwanasiasa hapaswi kuhukumiwa moja kwa moja kwa kubadili msimamo baada ya kuhamia chama kingine.

“Unapobadili chama, mara nyingi unalazimika pia kubadili hoja ili ziendane na mazingira na msimamo wa chama ulichojiunga nacho,” anasema.

Mitandao ya kijamii imeongeza kasi ya mjadala huu kwa kurejesha kauli za zamani na kuzilinganisha na matukio ya sasa. Hali hiyo imewafanya wanasiasa kuwa chini ya rekodi ya kudumu ya maneno yao, jambo linalotajwa na wengi kuwa fundisho kwa viongozi wa kisiasa kulinda na kupima kauli zao kwa umakini katika zama hizi za teknolojia.