INEC yapuliza kipyenga kingine uandikishaji wapigakura

Muktasari:
- Yatangaza ngwe ya pili ya uboreshaji wa daftari la kudumu la mpigakura katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, huku kikiwanyooshea kidole mawakala na viongozi wa vyama vya siasa kuacha kuingilia mchakato huo.
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji wa Rufaa, Jacobs Mwambegele ametangaza ngwe ya pili ya uboreshaji wa daftari la kudumu la mpigakura litakaloanza Mei 1 na kutamatika Julai 4, 2025.
Mchakato huo umefunguliwa baada ya kukamilika mzunguko wa kwanza, ulioanza Julai 20,2024 hadi Machi 25,2025 ikiwa ni utekelezaji wa masharti ya kifungu 16 (5) cha sheria ya uchaguzi wa Urais, Wabunge na Madiwani sheria namba moja ya mwaka 2024, inayoitaka INEC kufanya maboresho hayo mara mbili baada ya uchaguzi mkuu na kabla ya kuteua wagombea.
Akizungumza wakati anatangaza ufunguzi wa uboreshaji wa daftari hilo mzunguko wa pili jijini Dodoma leo Jumatatu, Aprili 14, 2025, Jaji Mwambegele amesema tume hiyo imeshakamilisha maandalizi ya daftari hilo la uboreshaji kwa awamu ya pili.
“Tume imeshakamilisha maandalizi ya daftari la kudumu la mpigakura awamu ya pili litafanyika kuanzia Mei Mosi mwaka huu hadi Julai 4, 2025 uboreshaji utakuwa katika mizunguko mitatu,” amesema.
Akitaja mizunguko hiyo itakavyokuwa, Jaji Mwambegele amesema mzunguko wa kwanza utahusisha mikoa 15, kwa wakati mmoja na utafanyika kwa muda wa siku saba kuanzia Mei Mosi 2025 hadi Mei 7, 2025.
“Vituo vya uandikishaji 3,808 vitatumika, mikoa itakayohusika katika mzunguko wa kwanza ni Geita, Kagera, Mara, Shinyanga, Mwanza, Simiyu, Rukwa, Tabora na Katavi. mingine ni Kigoma, Iringa, Ruvuma, Mbeya, Njombe na Songwe,” amesema.
Mzunguko wa awamu ya pili Jaji Mwambegele amesema utahusisha mikoa 16 kwa wakati mmoja na utafanyika kwa muda wa siku saba kuanzia Mei 16, 2025 hadi Mei 22, 2025 ambapo vituo 3,321 vitatumika.
“Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Morogoro, Pwani, Singida, Dodoma, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Mjini Magharibi, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Kaskazini Pemba na Kusini Pemba,” amesema.
Mzunguko wa tatu katika uboreshaji wa daftari hilo la kudumu la mpigakura, kwa mujibu wa Jaji Mwambegele utahusisha vituo 130 vilivyopo kwenye magereza yaliyopo Tanzania Bara, na vituo 10 vilivyopo kwenye vyuo vya mafunzo Tanzania Zanzibar.
“Shughuli itafanyika kwa wakati mmoja na ni siku saba, kuanzia Juni 28, 2025 hadi Julai 4, 2025,” amesema.
Jaji Mwambegele amesema uboreshaji wa daftari la kudumu la mpigakura kwa awamu ya pili utafanyika kuanzia ngazi ya Kata, Tanzania Bara na ngazi ya Jimbo kwa Tanzania Zanzibar na jumla ya vituo 7869 vitahusika.
“Kati ya hivyo vituo 657 viko Tanzania Bara, na vituo 210 viko Tanzania Zanzibar katika awamu ya pili ya uboreshaji tunatarajia wapiga kura wapya milioni 1.3 wataandikishwa, wapigakura milioni 1.9 wataboresha taarifa zao, na wapiga kura148,624 watafutwa kwenye daftari kwa kukosa sifa za kuendelea kuwa kwenye daftari,”amesema Jaji Mwambegele.
Mambo yatakayo husisha katika uboreshaji
Akijata mambo hayo, Jaji Mwambegele amebainisha kuwa kuandikisha wapigakura wapya, ambao ni raia wa Tanzania wenye umri wa kuanzia miaka 18 na zaidi.
“Kutoa kadi mpya kwa wapigakura waliopoteza au kadi zao kuharibika, kutoa fursa kwa wapigakura kurekebisha majina yao na taarifa nyingine, kuhamisha taarifa za wapigakura waliohama kutoka kata au jimbo walikojiandikisha awali,” amesema.
Mambo mengine, kuondoa taarifa za wapiga kura waliopoteza sifa za kuwemo kwenye daftari hilo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kifo.
“Vituo vitafunguliwa saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12 Jioni kila chama cha siasa kimepewa nakala ya orodha ya vituo vyote vya kuandikisha wapigakura vitakavyotumika katika uboreshaji wa awamu ya pili,” amesema.
Kulingana na Jaji Mwambegele wamegawa nakala hizo kwa vyama vya siasa ili kuviwezesha kupanga na kuweka mawakala katika shughuli ya uandikishaji.
“Kila chama kitaruhusiwa kuweka wakala mmoja kwenye kituo cha kuandikisha wapigakura kwa lengo la kushuhudia utekelezaji wa shughuli ya uandikishaji ikiwemo kutambua wanaokuja kituoni kama wana sifa au laa,”amesema
Jaji Mwambegele amesisitiza kwa kunukuu kifungu cha 11, sheria namba moja ya sheria ya uchaguzi wa urais, wabunge na madiwani ya mwaka 2024 amesema tume hiyo ina jukumu la kuandaa daftari la awali la mpigakura na kuliweka wazi kwa umma.
“Lengo la kuweka wazi ni kutoa fursa kwa wananchi kukagua na kufanya marekebisho ya taarifa za wapigakura na kuweka pingamizi dhidi ya wapigakura waliomo kwenye daftari hilo na hawana sifa,” amesema.
Amesema daftari la awali la wapigakura litabandikwa kwenye vituo vyote vilivyotumika kwenye uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpigakura awamu ya kwanza na mfumo utakao tumika kuhakiki ni kwa mpiga kura kuja kwenye kituo mwenyewe.
“Pili mpiga kura kupitia simu yake ya kiganjani kupiga namba *152*00# na kufuata maelekezo yatakayomwezesha kuhakiki taarifa zake na tatu kupiga simu namba 800112100 na kupewa maelezo yatakayo mwezesha kuhakiki taarifa zake,”amesema
Onyo kwa viongozi
Amesema mawakala au viongozi wa vyama vya siasa hawaruhusiwi kuingilia mchakato wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpigakura kituoni.
“Niwaombe viongozi wa vyama vya siasa na wadau wa uchaguzi kwa ujumla kuzingatia sheria za uchaguzi, kanuni za uboreshaji, maelekezo ya tume na kusimamia miiko na mipaka ya uendeshaji wa shughuli ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpigakura,” amesema.
Jaji Mwambegele amesema kwa anayehitaji kuweka pingamizi anatakiwa kwenda kwenye vituo cha kuandikisha wapigakura vilivyopo kwenye kila kata katika halmashauri husika.