Halahala kidole na jicho...huku kwa elimu vipi?

Ni jambo la kujivunia kuona Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwekeza katika elimu. Hii inaonesha kuwa pamoja na malengo yetu kuwa mengi, elimu imepewa kipaumbele cha kwanza, kwani ni chanzo cha maarifa. Mtu anaweza kukosa fahari kwa sababu hana fedha, lakini anaweza kuishi maisha matamu zaidi ya fahari akiwa na elimu. Maisha matamu huzidi fahari, kwani fahari ni mama wa ujinga.
Serikali yetu inaendeleza sera ya Elimu kwa Wote. Hakuna ubaguzi wa rangi, jinsia, kabila wala dini katika elimu. Ilipingana vikali dhidi ya kasumba za baadhi ya jamii kwamba wanaosoma ni watoto wa kiume tu. Ikapingana pia na imani kuwa wanaopaswa kujifunza ni watoto na vijana tu, na ndiyo maana tukaona elimu ya watu wazima ambapo wazee wanajifunza kusoma, kuandika na kuhesabu.
Kama vile haitoshi, katika awamu yako mama, Serikali imeazimia kutoa elimu bure kwa wote. Wananchi walio wengi wana hali duni kimaisha, hivyo inawawia vigumu kupambana na maadui wakubwa kama ujinga, umasikini na maradhi. Kwa kuliona hilo, Serikali yako ikaamua kutoa ruzuku kwenye maeneo hayo. Pongezi kwa kuwekeza vizuri kwenye ujenzi wa shule mpya na kuziendeleza zile za kata.
Lakini hapa ndipo ninapotaka kukupa neno Mheshimiwa. Wakati wa awamu ya tano, Mheshimiwa JPM aligundua upigaji katika ujenzi wa barabara. Baada ya bajeti ya ujenzi kupitishwa na makandarasi kupatikana, isingelikuwa rahisi kupiga fedha na kujenga barabara chini ya kiwango cha bajeti husika. Ikagundulika kuwa baadhi ya makandarasi walibuni mbinu mpya ya kupunguza milimita chache za kima cha ujazo wa lami ili kujipatia fedha za ziada.
Tunajua kwamba nyumba haikamiliki bila kuwa na choo. Vivyo hivyo katika ujenzi wa shule, hakuna shule itakayoitwa shule bila kuwa na vyoo. Litakuwa ni jambo la ajabu iwapo mchora ramani atakumbuka kuchora madarasa, ofisi, maktaba, maabara na viwanja vya michezo, akasahau vyoo. Kwa akili yangu ndogo nauona huu kuwa upigaji mpya. Nimeanza kuona masoko mapya na zahanati zikifunguliwa kwa hotuba za “Tuna upungufu wa matundu ya vyoo...”
Jambo lingine lililo kikwazo kwenye elimu ya bure ni michango isiyo na idadi shuleni. Kama nilivyosema awali, elimu bora huenda sambamba na vyoo.
Lakini pia tusisahau kuwa njaa ni mwana malegeza. Hakuna mtoto atakayeelewa somo akiwa na njaa. Iwapo Serikali iliamua kuweka ruzuku kwenye elimu, kivipi ilisahau kujumlisha chakula kwenye ruzuku hiyo?
Bila shaka tofauti ya elimu ya bure na elimu ya kulipia ni ada na gharama nyingine. Tunaridhika na jitihada za Serikali kumkwamua mtoto wa masikini asitofautiane kielimu na mtoto wa tajiri.
Kwenye shule za kulipia, ada anayolipa mzazi ndiyo inayobeba gharama za sare, usafiri, chakula, masomo ya kawaida na ya ziada, mitihani, matibabu na malazi. Hainiingii akilini ninapoona mzazi masikini akilipia gharama zote hizo katika elimu ya bure.
Gharama hizi zinatofautiana baina ya shule na shule. Kuna wanaotoza Sh1,000 kwa masomo ya ziada (twisheni), na wengine mpaka Sh5,000 kwa siku. Kadhalika kiasi kama hicho kwenye chakula na mitihani.
Hatujawahi kupata nafuu ya elimu ya bure tangu tulipomwandikisha mtoto. Kila siku mtoto aendayo shuleni huwa ni kizaazaa kwa wazazi, kwani nao wanabangaiza nauli za kuendea kutafuta riziki na kodi ya nyumba.
Nafikiri Serikali inaweza kumtua mzigo mzazi masikini. Iagize chakula moja kwa moja kutoka kwa mkulima. Ingefanya mpango wa kupeleka chakula hicho shuleni ili kuepuka tozo za wafanyabiashara.
Mitihani irudufiwe kwa mashine za shuleni.
Watoto wapatiwe bima ya afya ya pamoja, badala ya kila mzazi kuhangaika na mtoto wake anapoumwa. Mbona enzi zetu tulikuwa na vituo vya afya tangu shule za msingi? Angalau kwa kuanzia ingesaidia maana mzazi angehudumia mambo machache.
Athari za kuwasomesha watoto kwa staili ya “bora liende” zitakuja baadaye. Tutakosa wazalendo watakaosimamia nchi yao; hii itawafanya watoto wetu kuwa mamluki wa wageni watakaokuja na uchu wa kuwamiliki.
Pia, hatutakuwa na wataalamu watakaofanya kazi kwa faida ya nchi; Taifa letu litakuwa tegemezi kwa kila kitu maana watu wake watakuwa wajinga. Vilevile tutazidiwa na ongezeko la wahalifu, kwani watu hawatakuwa na namna nyingine ya kuishi.
Tunaapoona mtoto akijaza matusi kwenye karatasi ya mtihani wa kuhitimu, tujue kuwa hiyo ni ishara tosha kwamba “ameshakata kamba”. Anadhani kuwa hatuna namna ya kumkamata na kumuadhibu. Na kweli ataishi maisha yake na hatarudi kama mwanajamii.
Hii ni hatari kubwa, kwani ni rahisi kutokea yaliyotokea Liberia na Kongo. Watu wabaya waliwakusanya vijana kama hao kwa urahisi sana, wakawapa silaha za kuwachinjia wazazi na walimu wao.
Naishauri sana Serikali yako ichukulie suala hili kwa uzito unaostahili. Ikilichukulia poa na mambo yakiharibika, ni vigumu sana kuyarudisha kwenye mstari wake. Jitihada zozote za kuyasawazisha ni lazima zigharimu maisha ya watu wengi zaidi. Waswahili walituasa kutahadhari kabla ya hatari, na huu ndio wakati wa kuchukua hatua.