Prime
Gambo achutama, aomba radhi bungeni

Muktasari:
- Mbunge huyo amesema ametafakari na kuona iko haja mambo hayo kuyamaliza badala ya kupelekwa kamati ya Maadili, Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge.
Dodoma. Mbunge wa Arusha Mjini (CCM), Mrisho Gambo ameomba radhi Bunge na kufuta maneno aliyoyatoa dhidi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa.
Gambo alimtuhumu bungeni, Waziri Mchengerwa kwamba amesema uongo wakati akitoa maelezo ya Serikali dhidi ya tuhuma ambazo mbunge huyo aliziibua bungeni.
Aprili 16, 2025, Gambo akichangia bajeti ya Tamisemi alisema Jiji la Arusha wanajenga jengo la utawala gharama zake za jumla hazipungui Sh9 bilioni ambalo baadhi ya viongozi wanalipigia debe.
Mbali na jengo, Gambo ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha alisema kuna matumizi mabaya ya fedha kwenye ujenzi wa barabara ya kutoka Stand mpya kwenda Mbauda na ujenzi wa Soko la Machinga.
Hatua hiyo ilimfanya Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kumwagiza Waziri Mchengerwa kufuatilia na taarifa yake kuiwasilisha bungeni. Asubuhi ya leo Jumatano, Aprili 23, 2025, Waziri huyo akawasilisha taarifa hiyo.
Waziri huyo amesema katika maeneo yote manne ya tuhuma dhidi ya ubadhirifu wa fedha za miradi ambazo ziliibuliwa na Gambo, zimekosa mashiko kwani hakuna senti hata moja ya Watanzania ambayo ilitumika vibaya au kuliwa.
Hata hivyo, Gambo alipinga maelezo hayo jambo ambalo Spika Tulia aliamua kulipeleka Kamati ya Maadili, Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge ili kulishughulikia na ukweli ujulikane nani mkweli Gambo ama Waziri Mchengerwa.
Kabla siku haijaisha ya shughuli za Bunge, usiku wa leo Jumatano, Spika Tulia amesema kuna ombi la Gambo anataka kusema jambo.
Amesema kwa kutumia kanuni namba 70 ya kanuni za Kudumu za Bunge Tolea la Februari 2023 anampa nafasi ya kusema ambayo inasema kutokusema uongo bungeni.
Baada ya Gambo kusimama akasema: "Mheshimiwa Spika, utakumbuka ilitokea purukushani leo asubuhi. Baada ya kukaa na kutafakari nimeona niombe radhi."
Gambo amesema katika kipindi cha asubuhi kulitokea aliouita mtifuano ambao hakutaja nini maana yake.
Mbunge huyo amesema hawezi kuendelea zaidi kwani makofi ya wabunge yameonyesha wamemsamehe hivyo anaomba aishie hapo asije akaharibu.
Hata hivyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, William Lukuvi amemtaka Spika kumwelekeza Gambo aweke sawa taarifa yake, kwani kusema purukushani bila kujielekeza zaidi haikuwa na maana.
Lukuvi amesema si jambo jema kurudia maneno ambayo kiti kilishazuia lakini mbunge akarudia tena, hivyo akasema lazima afafanue vinginevyo waendelee kwenye kamati ya maadili.
Spika ametoa ufafanuzi kuhusu ombi la Gambo lakini akaomba ufafanuzi kwa mbunge huyo na alipopewa nafasi alisema katika hoja zake akizungumzia stendi mbili tofauti siyo moja.
Alipewa nafasi Lukuvi tena na kusisitiza lazima aseme kama anakubaliana na maelezo ya Serikali au purukushani maana yake nini akihoji tuhuma zinafutikaje.
Spika amempa nafasi Gambo na kumpa nafasi ya kumuongoza kwa kutumia kanuni ya 70 fasihi ya saba na nane ambapo amemtaka asimame.
Aliposimama Gambo amesema:"Na withdrawal na ninaomba radhi," hata hivyo, Spika amemtaka atumie maneno ya Kiswahili ambapo amesema: "Nafuta kauli na ninaomba radhi."
Spika amewahoji wabunge kuhusu ombi hilo na wabunge wamepaza sauti za pamoja wakisema wameafiki.