Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chadema yakomalia hoja yake ya kuahirisha uchaguzi mkuu 2025

Muktasari:

  • Lissu amesema kususia kila jambo watakaloletewa na Serikali ni moja ya njia ya kushinikiza kupatikana mifumo huru ya uchaguzi itakayotoa haki kwa wananchi

Rukwa. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),Tundu Lissu amesema kususia kila jambo watakaloletewa na Serikali ni moja ya njia ya kushinikiza kupatikana mifumo huru ya uchaguzi itakayotoa haki kwa wananchi kupata viongozi wanaowataka.

Amesema ili wafanikiwe azma hiyo ni lazima kila mmoja wao ashiriki harakati hizo huku akisisitiza kuzunguka nchi nzima kufikisha ujumbe kwa kila Mtanzania,  ingawa haitakuwa rahisi lakini anaamini wakiwa wamoja wanaweza kuvuka.

Lissu amezungumza hayo leo Machi 26,2025 kwenye  mkutano wa hadhara uliofanyika Sumbawanga Mjini, mkoani Rukwa kwenye mwendelezo wa kampeni ya kutoa elimu kwa wananchi juu ya kampeni ya ‘No reforms no Election’ inayolenga kuishinikiza Serikali kubadili mifumo huru ya uchaguzi.  

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),Tundu Lissu.

“Chochote wanachopendekeza tukisusie, kila watakachotuletea tukikatae na nimeangalia sheria za nchi sijaona sehemu kama tukikataa kwenda kupiga kura ni dhambi  au tumevunja sheria, lakini  ukweli wa Mungu ni kwamba hata kwa Katiba hii inawezekana kuahirisha uchaguzi,”amesema.

Amesema Katiba imesema kama kuna dharura  uchaguzi unaweza kuahirishwa kwa mwaka mmoja hata kama Bunge litakuwa limevunjwa likisubiri uchaguzi, ikitokea dharura Katiba inasema Bunge litaitishwa wabunge walewale kwenda kujadili dharura iliyojitokeza.

“Bunge hilo litapewa mwaka mmoja kwa Katiba hii tuliyonayo,  kama ukisema kuahirisha uchaguzi haiwezekani basi tutabadilisha Katiba yenyewe ili iruhusu tuahirishe uchaguzi hata kama hakuna dharura kwa kuwa imetengenezwa na binadamu hakuna kinachoshindikana,” amesema.

Lissu katika maelezo yake alitolea mfano kwa kudai Tanganyika ilikufa siku moja na iliuawa na Bunge kwa siku moja baada ya Rais Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Abeid Karume mwaka 1964 kusaini makubaliano ya Muungano.

 “Siku tatu baadaye Bunge likiwa mapumziko liliitishwa Dar es Salaam kwa dharura ilikuwa siku ya Jumamosi wala haikuwa siku ya kazi waliitwa kujadili muswada wa kuunganisha Tanganyika na Zanzibar na walipitisha saa hiyohiyo na Tanganyika kwisha kwa siku moja na Bunge hilihili,” amesema Lissu.

Lissu amesema chama hicho ni kimbilio hivyo wananchi ni lazima wajitolee kuunga mkono msukumo huo kwa kuchangia kiasi cha fedha ili kuwasaidia viongozi kuwafikia Watanzania maeneo yote nchini.

Awali, katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ amesema madai ya kudai mifumo huru ya uchaguzi itakuwa na tija, hasa mtu akishinda kwa haki kwenye sanduku la kura atangazwa bila kutumia vurugu.

“Ndiyo maana tunaomba tuungwe mkono na Watanzania wote bila kujali ni wafanyakazi, wafanyabiashara, wakulima na wafugaji ili kuhakikisha tunafanikisha jambo hili ili kupata viongozi kwa nguvu za umma kwa kuwa makundi yote tunaingiliana,” amesema.

Katika hatua nyingine, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, John Heche akiendelea na Kampeni hiyo mkoani Njombe amesema shabaha yao ya kutoa elimu hiyo ni kutaka kubadilisha maisha ya Watanzania kupitia utajiri wa rasilimali zilizopo.

“Tumekosa viongozi wasiokuwa na maono Tanzania badala ya kufundisha watu wetu na kuruhusu benki zetu ziwe rafiki kwa vijana waweze kufanya kazi na kutoa ajira na mzunguko wa fedha, lakini watu wa nje kila kitu wanapewa,” amesema.

Heche amesema wanahitaji kuungwa mkono na Watanzania ili waweze kubadilisha maisha ya Watanzania, huku akisisitiza kuwa haiwezekani unaenda Ludewa mkoani Njombe kuna chuma, lakini nchi inaagiza vyuma nje ya nchi.

“Tulishauri tukiwa bungeni lakini hatukusikilizwa, kama wangefanyia kazi na kuunganisha na rasilimali zingine kila mwananchi angekuwa na uwezo wa kupata bima ya matibabu bila shida yeyote,”amesema