Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chadema yaja na Katiba mpya, free Tundu Lissu

Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu wakati akitoka katika kizimba cha Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam Jumatano, Februari 18, 2026 baada ya kesi yake kuahirishwa. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Kamati Kuu iliyoketi kwa siku mbili jijini Dar es Salaam, pia imeazimia ofisi ya makao makuu ya chama hicho Mikocheni iitwe Edwin Mtei House, wakati zile za zamani za Ufipa, Kinondoni ziitwe Bob Makani House ikiwa ni kuwaenzi waasisi hao wa Chadema.

Dar es Salaam. Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) imeazimia kuanza rasmi mikutano ya hadhara nchi nzima katika operesheni itakayojulikana kama ‘Katiba mpya, Free Tundu Lissu’.

Mbali na hilo, kamati kuu hiyo iliyoketi kwa siku mbili jijini Dar es Salaam, pia imeazimia ofisi ya makao makuu ya chama hicho Mikocheni iitwe Edwin Mtei House, huku ile ya zamani ya Ufipa, Kinondoni ikiitwa Bob Makani House, ikiwa ni kuwaenzi waasisi hao wa Chadema.

Hayo yameelezwa leo, Jumamosi Mei 2, 2026, na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, wakati akitoa maazimio 12 ya awali ya kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho, kilichoketi kwa siku mbili Aprili 28 na 29, 2026 kujadili masuala mbalimbali, ikiwemo hali ya kisiasa nchini.

Mnyika amesema operesheni itakayofanyika itakuwa na awamu mbili, ambapo ya kwanza itaanza wiki ya tatu ya Mei na itahusisha mikoa 11 katika kanda tatu za chama hicho.

Kanda hizo ni Serengeti yenye mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Mara; Victoria (Mwanza, Geita na Kagera); na Kaskazini inayojumuisha Tanga, Arusha, Manyara na Kilimanjaro.

Mikutano hiyo ya hadhara itafanyika baada ya Chadema kuruhusiwa kuendelea na shughuli za kisiasa zilizokuwa zimesimamishwa kwa amri ya mahakama.

Ujumbe rasmi katika mikutano hiyo amesema utakuwa ni vuguvugu la kudai Katiba mpya ndani ya muda mfupi na kushinikiza mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, aachiwe huru bila masharti.

Lissu anashikiliwa mahabusu kutokana na kesi ya uhaini inayomkabili kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa,  tangu alipokamatwa Aprili 9, 2025.

Mnyika amesema kamati kuu imeazimia kushinikiza kuachiwa kwake kwa Lissu  inaamini kesi hiyo ni ya kisiasa, hivyo inauomba umma na wapenda haki kusimama pamoja ili kushinikiza aachiwe huru bila masharti.

Akifafanua kuhusu Katiba mpya, Mnyika amesema kwa kipindi kirefu Watanzania wamepitia changamoto kutokana na suala hilo, hivyo Kamati Kuu inaona hawawezi kusubiri tena mchakato mrefu, bali ipatikane si zaidi ya mwaka 2027.

“Kwa sababu hiyo, Kamati Kuu imeazimia kuundwa kwa kamati ndogo itakayokuwa na jukumu la kuandaa mkakati wa kuukwamua mchakato wa Katiba mpya.

“Kamati hiyo itaandaa muswada wa sheria, kwa niaba ya wananchi, utakaoeleza utaratibu wa kukwamua, kuendeleza na kukamilisha mchakato wa Katiba mpya,” amesema.

Amefafanua kuwa muswada huo utaeleza namna ya kura za maoni zitakavyofanyika chini ya usimamizi wa chombo huru, kwa uhuru na haki.

“Kamati Kuu imeazimia kuongoza wananchi kuanzia sasa ili mchakato wa Katiba mpya uanze mara moja. Katiba hiyo ipatikane mapema, si zaidi ya mwaka 2027,” amesema.

Pendekezo hilo ni la pili kutolewa ndani ya siku 10, baada ya Tume ya Jaji Chande ya kuchunguza matukio ya wakati na baada ya uchaguzi wa Oktoba 29, 2025, kupendekeza Katiba mpya ipatikane ifikapo mwaka 2028 ili itumike katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa 2029 na uchaguzi mkuu wa 2030.


Kuwaenzi waasisi

Mnyika amesema wajumbe wa Kamati Kuu wameazimia kuyapa majina ya waasisi ofisi za chama hicho za Mikocheni na Ufipa, ikiwa ni sehemu ya kutekeleza ahadi ya viongozi ya kuwaenzi.

“Azimio hili limetekeleza uamuzi wa Mkutano Mkuu wa chama wa Januari 21, 2025 pamoja na ahadi iliyotolewa na viongozi wakati wa msiba wa mwasisi Mtei,” amesema.

Pia, amesema Kamati Kuu imeendelea kusisitiza kuwa Oktoba 29 hakukuwa na uchaguzi huru, haki na wa kuaminika.

“Kuhusu yaliyotokea Oktoba 29 na baadaye, Kamati Kuu imeazimia kuwa wale wote waliohusika kuratibu na kufadhili matukio hayo wawajibishwe bila kujali nyadhifa zao,” amesema.

Aprili 28, akitoa ufafanuzi, Mwenyekiti wa Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani Oktoba 29, Jaji Mkuu mstaafu Othman Chande, alisema ripoti yao imependekeza hatua za uwajibikaji, ikiwemo kuwajibika binafsi kwa waliohusika na makosa ya jinai au madai.

Kwa mujibu wa Mnyika, Kamati Kuu imeazimia kuundwa haraka kwa tume huru ya kufanya uchunguzi wa kina wa matukio ya Oktoba 29 na baada yake.

“Tunasisitiza kuwa tume hiyo lazima iwajumuishe watu wanaoaminika ndani na nje ya nchi ili kuchunguza matukio ya mauaji yaliyotokea. Tunatoa pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao,” amesema.

Ameongeza kuwa pamoja na kwamba maisha ya binadamu hayawezi kulipwa kwa fedha, familia zilizopoteza wapendwa wao zinapaswa kulipwa fidia kama ishara ya utu na faraja.

Mbali na hilo, amesema Kamati Kuu imeazimia kuwaongoza wananchi kudai hatua za haraka zichukuliwe, ikiwemo kupunguza utitiri wa kodi ili kushusha bei ya mafuta na kupunguza gharama za maisha.

Katika hatua nyingine, Kamati Kuu iliazimia kujaza nafasi za makatibu wa kanda zilizowazi, ikimteua Yohana Kaunya kuwa Kaimu Katibu wa Kanda ya Kaskazini, huku mchakato wa kumpata Katibu wa Kanda ya Kusini ukiendelea na utakamilika katika kikao kijacho.

“Kamati Kuu, kwa kutumia mamlaka yake chini ya Ibara ya 7(16.0) ya Katiba ya chama, imemteua Godbless Lema na Salma Kasanzu kusimamia shughuli za chama katika Kanda ya Kati kwa kushirikiana na kamati ya uongozi iliyopo hadi uchaguzi wa kuziba nafasi hizo utakapofanyika,” amesema.

Aidha, amesema Kamati Kuu imepitisha uchambuzi wa ripoti ya Jaji Chande na kuidhinisha maazimio mengine ambayo yatafafanuliwa zaidi siku zijazo.

“Nitumie fursa hii kuwatangazia wanahabari kuwa ufafanuzi wa kina wa uchambuzi wa ripoti ya Chande pamoja na maazimio mengine utafanyika Mei 5,” amesema Mnyika.