Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chadema kujisuka upya, kusukuma ajenda ya kudai mageuzi

Wajumbe wa kamati Kuu Chadema, wakiwa katika kiko cha kamati Kuu jijini Dar es Salaam  Aprili 28, 2026. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Kamati Kuu imeazimia pia kufanya uchaguzi na kujaza nafasi za uongozi zilizo wazi na iko mbioni kutoa kwa umma uchambuzi wake wa ripoti ya Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani ya Oktoba 29.



Dar es Salaam. Kamati Kuu ya Chadema imeazimia mambo mbalimbali, ikiwemo kuanza rasmi kwa mikutano ya hadhara nchi nzima, kuweka mpango wa ukusanyaji wa fedha kwa ajili ya kuendesha shughuli za chama na kusukuma ajenda ya kudai mageuzi kupitia mabadiliko ya katiba.

Kikao hicho cha siku mbili, ambacho pia kimejadili na kuchambua ripoti ya Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani ya Oktoba 29, kilifanyika katika makao makuu ya chama hicho, Mikocheni jijini Dar es Salaam.

Hiki ni kikao cha kwanza kufanyika baada ya kusitishwa kwa shughuli za kisiasa za chama hicho Juni 10, 2025 kupitia amri ya Mahakama Kuu.

Kikao hicho kiliongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche, kutokana na Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu kuwa gerezani akituhumiwa kwa kesi ya uhaini inayomkabili.

Aprili 28, 2026, Heche alipofungua kikao hicho aliwaeleza wajumbe wa Kamati Kuu kujadili na kufanya maamuzi ya busara, yenye mwelekeo thabiti na usiotetereka, akisisitiza kuwa hatima ya chama na nchi ipo mikononi mwao kama chama kikuu cha upinzani.

Kwa mujibu wa vyanzo vya ndani, miongoni mwa mambo yaliyokubaliwa ni kufanya uchaguzi wa kujaza nafasi za uongozi zilizokuwa wazi kutokana na viongozi kujiuzulu, kuhama au kukoma kwa nyadhifa kwa sababu mbalimbali. Pia, kikao hicho kiliazimia kutoa kwa umma uchambuzi wa ripoti ya Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani ya Oktoba 29 iliyoongozwa na Jaji Mohamed Chande Othman.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo Mwananchi imezipata, wakati wowote kuanzia sasa, uongozi wa Chadema utaitisha mkutano na wanahabari kwa ajili ya kutangaza maazimio hayo na kuichambua ripoti ya Jaji Chande.

Aprili 23, 2026, akiwasilisha matokeo ya ripoti hiyo, Jaji Mkuu mstaafu Chande, alitaja vyanzo vitano pamoja na vichocheo vinne vya matukio hayo, vikiwemo kauli za wanasiasa na matukio ya utekaji, vilivyotajwa kusababisha ghasia za Oktoba 29 na baada yake.

Kwa mujibu wa vyanzo vya ndani vya chama hicho, kikao hicho pia kilimteua Yohana Kaunya kuwa kaimu katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, akichukua nafasi ya Totian Ndonde aliyejiuzulu wadhifa huo.

Mbali na hilo, wajumbe hao waliazimia kuwa baada ya mchakato wa kuziba nafasi zilizoachwa wazi za uongozi kukamilika, Chadema kiitishe kikao cha Baraza Kuu kitakachotekeleza majukumu mbalimbali kwa mujibu wa katiba ya chama hicho.

Aidha, katika kikao hicho, hoja ya maridhiano inadaiwa iliibuliwa na mmoja wa wajumbe, lakini haikufua dafu baada ya wajumbe kukataa kujadili suala hilo.

Kutokana na kutoshiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba 29 na hivyo kukosa sifa ya kupata ruzuku, kikao hicho kiliazimia kuweka mkakati bora wa upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kuendesha shughuli za chama hicho.

Alipotafutwa leo Alhamisi, Aprili 30, 2023, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), Amani Golugwa amesema chama hicho kimekamilisha siku mbili za vikao vizito vya kamati kuu vilivyojadili na kuazimia masuala mbalimbali, ambayo yatawekwa hadharani katika siku za karibuni.

Alipoulizwa kuhusu baadhi ya mambo yaliyojadiliwa, likiwemo suala la maridhiano na kujaza nafasi za uongozi, Golugwa amekiri kuwa ni miongoni mwa mada zilizopitiwa, lakini akasisitiza kuwa maelezo rasmi yatatolewa siku ya kutangaza maazimio.

“Hizo hoja zinazozungumzwa, pamoja na nyingine ulizotaja na zile zinazosikika pembeni, tutazieleza rasmi siku tutakapotangaza maazimio,” amesema.

“Kwa sasa siwezi kutoa taarifa ya kina hadi pale tutakapowasilisha taarifa rasmi katika siku chache zijazo,” ameongeza Golugwa.

Amefafanua kuwa Chadema ina utaratibu wa kuandaa kwa kina maazimio yanayofikiwa baada ya kumalizika kwa vikao, kikiwemo cha kamati kuu.

“Tunatambua kuwa Watanzania wengi wanasubiri kwa shauku kubwa kujua yaliyojadiliwa. Tunajiandaa kuwasilisha maazimio yatakayokidhi matarajio ya wengi,” amesema.

“Tunajua nchi inasubiri kwa hamu kubwa kujua yaliyojadiliwa, na tunaamini maazimio tutakayotoa yatakuwa yale ambayo wengi watatamani kuyasikia,” ameongeza Golugwa.

Kwa mujibu wa Golugwa, Chadema itajitokeza kwa jamii ikiwa na sura kuu mbili; moja ikiwa ni kupigania haki kwa kusimama kidete katika kusukuma ajenda ya haki kwa Watanzania bila kuyumbishwa wala kubembeleza.

Amesema chama hicho pia kitapendekeza na kusukuma ajenda ya upatikanaji wa Katiba mpya bora, yenye uwazi katika mchakato wa uchaguzi wa viongozi, kwa lengo la kuimarisha ustawi wa wananchi.

Amefafanua kuwa sura ya pili ya chama hicho itajikita katika kuhimiza ukweli na uwajibikaji, kwa kuhakikisha Taifa linaepukana na unafiki, upendeleo na ukosefu wa uwajibikaji na kujenga jamii inayothamini ukweli kama msingi wa uhuru na maendeleo.

“Hatutaki taifa lililojaa ujanja ujanja, uchawa na uongo. Tunataka jamii inayothamini ukweli na uwajibikaji, kwa sababu ukweli humuweka mtu huru,” amesema.

Amesisitiza kuwa Chadema inalenga kuona viongozi wanakubali kukosolewa, wanawajibika pale inapobidi na daima wanasema ukweli.

“Tunataka Taifa ambalo viongozi wanakubali kukosolewa, wanawajibika inapobidi na wanasema ukweli wakati wote. Hayo tutayasimamia kwa msimamo usioyumba na kwa kiwango cha juu,” amesema Golugwa.